RC Makonda aeleza mazingira ya kutekwa Bilionea Mo Dewji

October 11, 2018 2:26 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Vyombo vya dola vinaendelea kuwasaka wazungu wawili waliohusika kumteka bilionea huyo.
  • Amewatahadharisha watu wote wanaotoa taarifa zisizo sahihi kuhusu tukio hilo na kuwataka wananchi kuwa watulivu na kuziacha mamlaka kufanya kazi.
  • Amewaomba wamiliki wa hoteli, nyumba za kupangisha (apartments), viongozi wa serikali za mitaa na wananchi kushirikiana na vyombo vya dola katika uchunguzi huo.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema vyombo vya dola vinaendelea kuwasaka wazungu wawili waliohusika kumteka bilionea Mohammed Dewji mapema leo asubuhi.

Makonda amewaomba wamiliki wa hoteli, nyumba za kupangisha (apartments), viongozi wa serikali za mitaa na wananchi kushirikiana na vyombo vya dola katika uchunguzi huo.

Kwa mujibu wa Makonda, taarifa za awali zimesema kuwa  Dewji ametekwa asubuhi ya leo (Oktoba 11, 2018) na raia wawili wa kigeni wakati akiingia katika hoteli ya Collesseum iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam kwaajili ya kufanya mazoezi.

“Gari moja lilikuwa ndani na la pili lilikuwa nyuma likimfuatilia Mo. Wakati  amepaki, gari la pili liliingia walishuka wazungu wawili wakamkaba, wakamtupia simu yake chini na kumwingiza kwenye gari,” amesema.

Wakati watekaji hao wanatoka, Makonda amesema walikuta geti la pili limefungwa na kulazimisha walinzi kufungua.

“Walilazimisha kufungua geti kwa kupiga risasi hewani na baadaye walishuka na kufungua geti wenyewe na kukimbia na Mo,” amesema.

Sehemu ya hoteli ya Collesseum iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam ambako tukio la kutekwa kwa Bilionea Mohammed Dewji limefanyika leo asubuhi. Picha| Nuzulack Dausen.

Makonda amesema hadi sasa vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kufanya uchunguzi ikiwemo kuwahoji walinzi wa hoteli hiyo ambao watasaidia kupatikana kwa taarifa za msingi zikiwemo namba za magari yaliyotumika kufanya utekaji.

Makonda, ambaye ni Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama wa mkoa, amesema kwa kawaida Mo huwa hatembei na walinzi wakati anaenda mazoezini kwa kuwa kuna usalama na amani.

Aidha, amewatahadharisha watu wote wanaotoa taarifa zisizo sahihi kuhusu tukio hilo na kuwataka wananchi kuwa watulivu na kuziacha mamlaka kufanya kazi yake na zitatoa taarifa sahihi kwa wakati.

“Usitoe taarifa yoyote ambayo huna uhakika nayo. Msemaji  wa Jeshi la Polisi ni Mambosasa na viongozi wa juu pamoja na IGP Sirro na Msemaji wa mkoa ni mimi; wewe ambaye huna taarifa sahihi huna sababu ya kuanza kupost kwenye mitandao,” amesema.

Enable Notifications OK No thanks