Rais Samia: Serikali kuendeleza uwekezaji bandari Zanzibar
- Ni pamoja na ujenzi wa bandari ya Wete na Kizimkazi.
- Bandari ya Shumba mjini Pemba na Micheweni zinafikiriwa kujengwa.
Dar es Salaam, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake itaendelea kuongeza uwekezaji katika ujenzi wa bandari visiwani humo ili kuchochea shughuli za kiuchumi zitakazoleta maendeleo ikiwemo utalii, biashara, pamoja na uchumi wa bluu.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza lwakati wa ufunguzi wa hoteli ya Bawe Island iliyopo Kisiwa cha Bawe Zanzibar leo Januari 7, 2025, amesema mbali na mazingira mazuri ya uwekezaji yanayowekwa Serikali yake inatekeleza miradi itayochangia maendeleo endelevu katika sekta ya utalii na miundombinu.
“Kuna uwekezaji katika bandari ya makontena na mizigo Malindi, bandari kavu ya Maruhubi, uwekezaji katika bandari ya makontena Fumba na bandari ya makontena mkoani Pemba, lakini vilevile kuna bandari mpya ya kisasa ya abiria na mizigo Maruhubi mpiga duri na uwekezaji katika miundombinu ya kushusha mafuta ya gesi,” ameeleza Rais Samia.
Muonekano wa Hoteli ya Kitalii ya Bawe Island the Cocoon Collection iliyopo katika Kisiwa cha Bawe. Picha/ Ikulu Tanzania/X.
Rais Samia ameongeza kuwa zipo bandari zinazohitaji kukamilishwa ikiwa ni pamoja na bandari ya jumuishi ya Manga Pwani na bandari zinazofikiriwa kujengwa kama vile bandari ya Shumba mjini Pemba, Micheweni, pamoja na bandari ya Wete.
“Katika jitihada za kuendelea kuifungua Pemba kiuchumi kutakuwa na ujenzi wa bandari ya wete pale Pemba, kubwa zaidi ndugu zangu ni ujenzi wa bandari ya Kizimkazi, hii Kizimkazi inaenda kubadilika kuwa nyingine, sasa hapa dokta umemeliza na mimi nitakupa kila ushirikiano,” amesema Rais Samia.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hussein Ali Mwinyi, wakati wa ufunguzi wa Hoteli. Picha/ Ikulu Tanzania/X.
Hata hivyo, Rais Samia ameeleza kuwa kumarika kwa miradi mingine kama huo uliofunguliwa leo utategemea zaidi uamuzi na jitihada za Serikali ya Zanzibar kuimarisha viwanja vya ndege.
“Kila mmoja wetu ni shahidi wa ufanisi na huduma bora zinazotolewa katika uwanja wa ndege terminal (III) pale uwanja wa ndege wa Abeid Aman Karume , wasafiri wanaokuja na kuondoka zanzibar wanafurahi na huduma zinazotolewa, hivyo tuongeze jitihada,” amesema Rais samia.
Mradi wa hoteli ya Bawe Island Cocoon Collection umegharimu dola za Marekani Sh42 milioni na ni mojawapo ya miradi 115 inayotekelezwa Zanzibar ukitarajiwa kutoa ajira 400 kwa Watanzania.