Rais Samia, Ramaphosa wafungua ukurasa mpya wa ushirikiano

March 17, 2023 2:21 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kwa kulinda  mahusiano  yaliyoasisiwa na kuongeza njia mpya za ushirikiano.
  • Kuondolewa kwa vikwazo, ni miongoni mwa njia itakayochochea mahusiano kuimarika.


Dar es Salaam. Nchi za Tanzania na Afrika Kusini zimeazimia kuendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kwa kuongeza wigo wa ushirikiano katika nyanja za kiuchumi, siasa na diplomasia, ulinzi na usalama pamoja na masuala ya kijamii.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa aliyekuwa akizungumza na wanahabari mara baada ya mkutano wa ndani na mwenzake Samia Suluhu Hassan aliyepo ziarani nchini humo, amesema ni tamanio lake kuona nchi hizo zikishirikiana katika nyanja nyingi zaidi.

“Historia yetu tajiri inatuunganisha kama Waafrika na inachangia katika kuimarisha mahusiano baina yetu.

“Tunaamini kuwa ziara hii ya kiserikali itaimarisha zaidi uhusiano wa kisiasa na kiuchumi baina ya nchi zetu mbili ni lazima kutumia fursa hii kutizama  maeneo mengine zaidi ya ushirikiano,” amesema Ramaphosa.

Rais Ramaphosa amebainisha kuwa ili kukamilisha hilo mataifa hayo hayana budi kushughulikia vikwazo vyovyote na kuunda mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili.


Soma zaidi


Tanzania na Afrika Kusini zimekuwa na uhusiano katika nyanja mbalimbali kwa muda mrefu ambapo ushirikiano huo uliasisiwa na juhudi za Tanzania katika kupigania uhuru wa taifa hilo la kusini mwa Afrika.

Aidha, Tanzania ni mshirika muhimu wa kibiashara na taifa hilo kwani kwa mujibu wa taarifa kutoka Serikali ya Afrika Kusini.

Biashara baina ya mataifa hayo iliongezeka kutoka Randi bilioni 6.8 ambazo ni sawa na Sh876 bilioni mwaka 2021 hadi Randi bilioni 8.7 (Sh1.11 trilioni) mwaka 2022.

Ushirikiano huo wa kibiashara umewezesha makampuni zaidi ya 250 kutoka Afrika Kusini kuwekeza katika nyanja mbalimbali nchini Tanzania.

Rais Samia akihitimisha ziara hiyo leo amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Afrika Kusini kama ambavyo imekuwa ikifanya na kuongeza kuwa inatarajia kuondoa vikwazo ambavyo vimekuwa vikikwamisha ukuaji wa ushirikiano katika baadhi ya sekta.

Ziara hiyo ya kikazi ya  Rais Samia nchini Afrika ya Kusini ni ya kwanza tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Tanzania miaka miwili iliyopita.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW