Rais Samia: Moshi haijakidhi vigezo kuitwa jiji

October 16, 2021 5:03 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Kwa vigezo vya Serikali, asema mji huo haujakidhi vigezo.
  • Asema labda mji huo uunganishwe na Vunjo kufanikisha hilo.
  • Aitaka Moshi isubiri kwanza ujenzi wa barabara.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Mji wa Moshi bado haujakidhi vigezo vya kuwa jiji lakini ameahidi ya kuwa Serikali italifanyia kazi suala hilo. 

Rais Samia aliyekuwa akizungumza leo Oktoba 15, 2021 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi mkoani Kilimanjaro amesema hilo litawezekana ikiwa baadhi ya maamuzi yatafanyika ikiwemo kuunganisha mji wa Vunjo ambao nao utaka kupandishwa hadhi kuwa halmashauri ya wilaya.

“Mji wa Moshi unadaiwa kuwa jiji lakini Vunjo wanataka kuwa halmashauri lakini ukitoka Moshi kwenda Vunjo siyo zaidi ya kilomita 20 au 25. Aidha Vunjo ivunjwe jiji litanuke au tufanyeje?,” amehoji Rais Samia na kuongeza kuwa “kuna vigezo ambavyo tukiangalia bado mji wa Moshi haujafikia.”

Hata hivyo, amesema Serikali itaangalia namna ya kufanikisha suala hilo ili mji huo uwe jiji.

Kiongozi huyo mkuu wa nchi alikuwa akijibu maombi yaliyotolewa na viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro ambao wameiomba Serikali iipandishe Moshi kuwa jiji na Vunjo kuwa halmashauri. 

“Kuna swala la vigezo ambalo tukiangalia bado Mji wa Moshi haujafikia, lakini niwaambie Serikali italifanyia kazi,” ameahidi Rais Samia.

Hadi sasa, Tanzania ina majiji sita ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga na Dodoma.

Kwa mujibu wa Serikali, sifa ambazo zinatakiwa ili mji uitwe jiji ni pamoja na uwezo wa kujitegemea kwa asilimia 95 kwa mapato ya ndani na uwepo wa maeneo ya kihistoria, maeneo ya utalii, makao makuu ya mkoa na kituo cha shughuli za kimataifa.

Rais Samia pia amewasisitiza wakazi wa Kilimanjaro kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona. Picha Ikulu Tanzania.

‘Na barabara subirini kwanza’

Pia Rais amewataka viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro wakiwemo wabunge wavute subira kuhusu suala la ujenzi wa barabara katika maeneo kwa sababu mkoa huo una hali nzuri ya barabara ikilinganishwa na maeneo mengine.

“Sasa ndiyo haya ya Wabunge wenu wa Kilimanjaro, kila mtu analilia barabara ya lami kilomita saba wakati maeneo mengine ya Watanzania kuna vumbi kilomita 200. Moshi mtasubiri kidogo kwa sababu barabara zinapitika,” amesema Rais Samia.

Amesema kwa sasa kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kujenga na kuboresha barabara za vijijii ili kurahisha shughuli za usafirishaji wa mazao na bidhaa mbalimbali.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW