Majaliwa aagiza ujenzi machinjio ya vingunguti kukamilika Juni

May 17, 2021 1:57 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Amesema hadi kufikia Juni 30, 2021 kazi zote za ujenzi ziwe zimekamilika.
  • Aagiza wafanyabiashara waruhusiwe kuanza kutumia machinjio hiyo. 
  • Ujenzi wake umefikia asilimia 95 na utagharimu Sh12.9 bilioni. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameagiza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa machinjio ya kisasa yaliyopo Vingunguti jijini hapa kabla ya Juni 30 mwaka huu na kuruhusu ianze kufanya kazi wakati wakimalizia ujenzi.

Amesema kuwa mpaka sasa asilimia 95 ya ujenzi wa mradi huo imekamilika ikiwemo mitambo ya kuchinjia na eneo la maji taka wakati tangi la kuhifadhia maji, chumba baridi cha kuhifadhia nyama na kuweka sakafu eneo la nje ya kiwanda ambapo mpaka kufikia Juni 30, 2021 kazi zote zitakuwa zimekamilika.

“Mstahiki Meya na Mkurugenzi, tunahitaji machinjio haya ili tuweze kuanza kazi, lakini pia Jiji na ushiriki wa wafanyabiashara mifugo zungumzeni kila siku ili mfikie hatua kwamba lini muanze, tunataka tuondoke kwenye eneo hili la zamani, kamilisheni hizo asilimia tano zilizobaki,” amesema Majaliwa alipofanya kukagua ujenzi wa machinjio hayo leo Mei 17, 2021.

Mtendaji huyo mkuu wa Serikali amesema kuwa ni vyema wafanyabiashara wakaanza kutumia machinjio hayo ya kisasa na yeyote anayetaka kutumia aruhusiwe ili kuwazoesha namna inavyofanya kazi.

“Miitambo ipo tayari, ni vyema tukawazoesha  ili muweze kujua taratibu, mwenyekiti unaweza kuwa unaandaa baadhi ya ng’ombe wakawa wanakuja kwenye machinjio mapya,” amesema Waziri Mkuu.


Soma zaidi: 


Amesema haitopendeza siku yakufunga machinjio ya zamani inapofika, uhamisho uwe ni wa ghafla na iwe kazi mpya kwa watendaji watakaohusika na machinjio hayo.

Pia ameagiza Halmashauri ya Jiji kuhakikisha mifereji ya maji taka na yale ya mvua yatakayokuwa yakitoka katika machinjio hayo kuwekewa mifereji maalumu ya kwenda mtoni badala ya kwenda kwenye makazi ya watu.

Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Jumanne Shauri amesema mradi  huo  utagharimu Sh12.9 bilioni na  utakapokamilika utasaidia kupanua wigo wa masoko ya nje na kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na ng’ombe na mbuzi.  

Machijio hayo yatakuwa na uwezo kuchinja ng’ombe 1,000 ndani ya saa 24 kiasi ambacho ni kikubwa mara mbili zaidi ya machinjio ya zamani ambayo uwezo wake ni hadi ng’ombe 400 kwa saa 24.

Enable Notifications OK No thanks