Rais Samia: Mhandisi Mfugale alikuwa mahiri, mzalendo wa kweli
Rais Samia Suluhu Hassan, akiongoza kutoa heshima za mwisho katika jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam leo Julai 2, 2021. Picha| Ikulu.
- Ni aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Patrick Mfugale.
- Ameagwa leo na Watanzania mkoani Dar es Salaam.
- Amesema alikuwa mzalendo aliyeipenda nchi yake.
Mwanza. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewaongoza waombolezaji wa Mkoa wa Dar es Salaam kumuaga aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Patrick Mfugale na kumtaja kuwa alikuwa mahiri na mzalendo wa kweli.
Mfugale alifariki dunia Juni 29, 2021 saa 5 asubuhi katika hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.
Mwili wa Mfugale umeagwa leo Ijumaa Julai 2, 2021 katika viwanja vya Karimjee kabla ya kusafirishwa kwenda Ifunda mkoani Iringa kwa mazishi yatakayofanyika nyumbani kwake Julai 5, 2021.
Akizungumza wakati wa kuaga mwili wa kiongozi huyo katika viwanja vya Karimjee jijjni Dar es Salaam, Rais Samia amesema amepokea taarifa hizo kwa masikitiko kwa kuwa kabla ya kifo chake alikuwa mzima wa afya.
Rais Samia amesema Mhandisi Mfugale aliaga dunia Juni 29, 2021 baada ya kuugua kwa muda mfupi ambapo kifo hicho kimeacha simanzi na pengo kubwa katika familia na Serikali.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema familia imempoteza mtu muhimu waliyempenda na Taifa limepoteza Mhandisi mahiri na mzalendo wa kweli.
“Kwa niaba ya Serikali nitumie fursa hii kutoa pole kwa mke wa marehemu Mfugale, watoto wake, ndugu, jamaa na marafiki kwa msiba huu. Naelewa machungu yenu ni makubwa mno lakini yote haya ni mapenzi yake Mwenyezi Mungu,” amesema Rais Samia.
Amesema mara ya mwisho alionana na Mhandisi Mfugale pale alipotembelea daraja la JPM la Kigongo-Busisi na kwamba alimkuta akiwa makini na kumpatia maelezo ya kina kuhusu ujenzi wa daraja hilo.
Mfugale alimwonyesha matumaini yake jinsi ya kulijenga na kulikamilisha daraja hilo, bahati mbaya Mungu amemchukua kabla matumaini yake kutimia.
Baada ya kutoa heshima ya mwisho katika viwanja vya Karimjee, mwili wa marehemu Mfugale umepelekwa nyumbani kwake Kimara Temboni. Kesho Jumamosi Julai 3, 2021 atafanyiwa misa takatifu kanisani na mwili wake utasafirishwa kwenda Ifunda mkoani Iringa kwa ajili ya maziko yatakayofanyika Julai 5, 2021.
Awali watoto wa marehemu Mfugale wamemwelezea baba yao kuwa alikuwa mtu wa imani, mpole na aliyewaelekeza katika njia sahihi.
Latest