Rais Samia: Mfumo wa haki jinai umevurugika
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma, Naibu Spika Mussa Zungu, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchini, Mahandisi Hamadi Masauni, Katibu Mkuu Kiongozi Dk Moses Kusiluka, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Zena Said pamoja na Wajumbe wa Tume ya kuangalia Jinsi ya Kuimarisha Taasisi za Haki Jinai, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma Januari 31, 2023. Picha | Ikulu.
- Amesema mfumo huo unapaswa kurekebishwa.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema kwa kipindi cha miongo kadhaa mfumo haki jinai umekuwa na changamoto nyingi hivyo Serikali imeamua kuunda tume ya kutathmini mfumo wa utoaji haki na kimaadili katika taasisi za Serikali ikiwemo Jeshi la Polisi na Mahakama.
Amesema aliyekuwa akizungumza leo Januari 31, 2023 Ikulu, Chamwino jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi tume ya kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini amesema tume hiyo itafanya kazi ya kubaini upungufu uliopo na kuja na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha utoaji haki nchini.
“Tukaliangalie Jeshi la Polisi ambalo mara nyingi kama utazungumza na watu 100 basi 70 watalinyooshea kidole,” amesema na kuongeza kuwa,
“Pia, ofisi ya mashtaka tuangalie kwenyewe kukoje na kuna kasoro zipi kuna nini haswa kilichoharibu hii taasisi. Tuiangalie Takukuru kwa sababu kubadilisha tu mkuu wa taasisi haisaidii watamdanganya tu wafanye wanavyotaka.”