Rais Samia: Maandamano Oktoba 29 yalitaka kupindua nchi
- Asema tukio lililotokea ni la kutengenezwa na walioratibu walidhamiria kuangusha dola ya nchi.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kulikuwa na jaribio la kuipindua nchi na kuondoa dola iliyopo madarakani katika maandamano yaliyofanyika siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, na kusababisha vifo vya watu na uharibifu wa mali za umma na binafsi.
Katika hotuba yake kwa wazee wa na wazee wa Dar es Salaam pamoja na kuhutubia Taifa leo Desemba 2, 2025, Rais Samia amesema tukio hilo ni la “kutengeneza na waliotengeneza walidhamilia makubwa.”
Kauli ya Rais Samia inakuja ukiwa umepita takriban mwezi mmoja tangu, tukio hilo litokee na tayari ameshaunda tume ya kuchunguza kiini cha tukio hilo ikiwemo kubaini mzizi wa kilichosababisha vijana kuingia barabarani kwa ajili ya maandamano.
“Walidhamiria kuangusha dola ya nchi yetu,” amesema Rais Samia akibainisha kuwa vijana “walifanywa makasuku” na kuimbishwa kuwa yaliyotokea Madagascar yatokee na Tanzania bila kujua undani wa jambo hilo lililotokea katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.
Tukio hilo, amesema, ni mradi mkubwa wenye nia ovu ambao una wafadhili, washitiri, pamoja na watekelezaji lililowahusisha watu waliodhamiria kuhujumu Serikali huku wengine wakifuata mkumbo.
Rais Samia amesema kilichofanyika si maandamano bali ni vurugu kwa kuwa maandamano yanayokubalika kisheria ni lazima yawe na kibali na yaeleze yatapita wapi, kisha kuwe na ulinzi wa askari polisi wataosimamia usalama wao.
Agusia nguvu ilitumika kuzima maandamano
Katika hotuba yake, kwa mara ya kwanza Rais Samia amegusia kuhusu nguvu iliyotumika kuzima maandamano hayo inayokosolewa na wadau wa ndani na nje kuwa ilikuwa ni kubwa kuliko na kuleta madhara makubwa kwenye maisha ya watu.
Vyama vya upinzani vikiwemo Chadema na ACT-Wazalendo, asasi za kiraia na baadhi ya viongozi wa dini wamekosoa nguvu kubwa iliyotumika katika kudhibiti maandamano hayo ikiwemo matumizi ya risasi za moto.
Hivi karibuni Bunge la Umoja wa Ulaya liliishutumu Serikali ya Tanzania kutumia nguvu kupita kiasi kudhibiti maandamano huku Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) likieleza kuwa haikuwa vyema kuwaweka waandamanaji wote katika kundi la wahalifu na kuwachukulia hatua zilizosababisha vifo pamoja na majeraha.
“Tunapoambiwa tulitumia nguvu kubwa sana kwenye tukio lile, nguvu ndogo ilikuwa ni ipi? Ilikuwa tuwaangalie waandamanaji waliojiandaa kufanya mapinduzi mpaka wafanikiwe? Hapo patakuwa na dola kweli? Dola haipo hivyo,” amesema Rais Samia.
Rais Samia, aliyesisitiza kuwa nguvu iliyotumika iliendana na tukio, amesema kuwa kilichotokea Tanzania kinafanyika pia katika mataifa mengi akieleza kuwa inapobainika waandamanaji wanamwenendo usiofaa basi vyombo vya ulinzi na usalama huweka nguvu kubwa.
Tanzania imepata doa
Kutokana na tukio hilo Rais Samia amesema Tanzania imepata doa katika uga wa kimataifa ambako awali ilikuwa ikitambulika kama kisiwa cha amani ambapo pamoja na taswira kuchafuka inaweza kusababisha kukosa baadhi ya misaada na ufadhili kutoka nchi washirika na taasisi za kimataifa.
Hata hivyo, Rais Samia amewataka Watanzania kusahau yaliyopita na kuungana kwa pamoja kuponya majeraha ya tukio hilo akisisitiza kuwa ni Watanzania pekee watakaoponya jeraha lao na kuwa jambo hilo si la kwanza kutokea nchini.
“Sisi ni Watanzania, Tanzania itajengwa na Watanzania, jeraha limetokea lazima sisi Watanzania tutibu jeraha letu, na hili si la kwanza, tulipata jeraha kama hili 2001 ni sisi wenyewe tulitibu jeraha letu,” amesema Rais Samia.
‘Tumejipanga’ kudhibiti maandamano
Rais Samia ametumia mkutano huo kuwarai wazazi kuzungumza na watoto wao kuhusu uzalendo, kutorubuniwa na kuepuka kufanya vitendo vinavyoharibu nchi kwa kutafuta njia sahihi za kutatua changamoto zinazowakabili.
Hata hivyo, Rais Samia amesema amesikia minong’ono ya maandamano yanayotarajiwa kufanyika Desemba 9, mwaka huu ambapo amesema vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kukabiliana na changamoto yoyote itakayotishia hali ya usalama nchini.
Latest