Rais Samia atoa ufanunuzi wanafunzi wanaotakiwa kurudi shule
- Waliopata mimba shule za msingi wana hiari kurudi katika elimu rasmi au kwenda elimu mbadala.
- Asema suala la kurudi shule linawahusu wanafunzi wote walioacha shule.
- Ataka utulivu wakati Serikali ikitekeleza uamuzi huo.
Dar es Salaam. Rais Samia amesema fursa ya kurudi shule inawahusu wanafunzi wote waliopata changamoto za elimu huku akieleza kuwa wanafunzi wa shule za msingi wanaopata mimba wanaweza kuchagua kurudi shuleni au kwenda katika elimu mbadala.
Siku tano zilizopita Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alitangaza rasmi kuwaruhusu wanafunzi waliokatiza masomo yao kwa sababu ya kupata ujauzito wakiwa shuleni kurejea masomoni ili watimize ndoto zao.
Hata hivyo, Rais Samia leo Novemba 29, 2021 ametoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa suala hilo kwa wanafunzi waliopata mimba wakiwa shule za msingi na sekondari.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema wanafunzi waliopata ujauzito wakiwa shule za msingi wana uchaguzi wa kurudi shule katika mfumo rasmi au kwenda katika elimu mbadala ikiwemo mafunzo ya ufundi stadi.
“Kwa kawaida mtoto wa kike akishakua mama, kama amekuwa mama darasa la sita hatarudi tena darasa la sita kuendelea na shule, hiyo ndiyo kawaida,” amesema Rais wakati wa uzinduzi wa Shule ya Msingi Museveni iliyopo Chato mkoani Geita.
“Si kawaida, tuna mifano mizuri nchi nyingine zimefanya hivyo, Zanzibar wamefanya hivyo. Na kawaida wote ambao wamepata (ujauzito) wakiwa msingi hawarudi shule wanakwenda kwenye mkondo mbadala,” amesisitiza Rais huku akitaka mijadala kuhusu suala hilo ijikite katika misingi hiyo.
Baadhi ya wanaharakati na wadau wa elimu wamekuwa wakishinikiza wanafunzi wanaopata mimba wakiwa shule za msingi au sekondari waruhusiwe kurudi katika mfumo rasmi kwa sababu ni haki yao kuelimika.
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni akimkabidhi mfano wa funguo, Rais Samia Suluhu Hassan kama ishara ya makabidhiano ya Shule ya Awali na Msingi ya Museveni. Uzinduzi wa shule hiyo umefanyika wilayani Chato mkoani Geita leo Novemba 29, 2021. Picha|Ikulu.
Kuhusu wanafunzi watakaopata mimba wakiwa sekondari amesema “lakini wale wanaopata bahati mbaya wakiwa sekondari wale wanarudi na wanarudi wanaendelea masomo yao vizuri, wengine wanafika mpaka chuo kikuu.”
Kwa muda mrefu sasa Serikali ilikuwa imepiga marufuku kwa wanafunzi waliopata ujauzito kurejea shuleni baada ya kujifungua.
Msimamo huo wa Serikali ulichagizwa zaidi Juni 2017 baada ya Hayati Rais Dk John Magufuli kupiga marufuku wanafunzi wanaopata mimba mashuleni kuendelea na masomo ya shule ya msingi na sekondari akisema ndani ya utawala wake hakuna mwanafunzi aliyepata mimba na engeruhusiwa kurudi shuleni.
Pia alizitaka taasisi zinazotetea utaratibu wa wanafunzi waliopata mimba kurudi shuleni, kufungua shule zao za lakini si kuilazimisha Serikali kufanya hivyo.
Kurudi shule ni wote
Katika uamuzi mpya wa Serikali, Rais Samia amesema suala la kurudi shule haliwahusu wanafunzi walipata mimba pekee bali wanafunzi wote waliacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo utoro, ujauzito na nidhamu ili kutoa fursa kwa watoto wa Tanzania kupata elimu.
Amesema Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha utekelezaji wa uamuzi wa kuwarudisha wanafunzi shuleni huo hauathiri sekta ya elimu nchini.
Latest
