Rais Samia atengua, ateua wakurugenzi wa halmashauri

December 19, 2023 5:11 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Atengua uteuzi wa wakurugenzi wawili wa halmashauri za Mji wa Tunduma na Momba.
  • Amemteua Balozi Meja Jenerali Paul Kisesa Simuli kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uganda.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ameendelea kufanya mabadiliko ya viongozi katika ngazi mbalimbali nchini ambapo ametengua uteuzi wa wakurugenzi wawili wa halmashauri na kuteua viongozi wapya akiwemo Balozi wa Tanzania nchini Uganda.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana Disemba 18, 2023 imebainisha kuwa Rais Samia ametengua uteuzi wa Lena Martin Nkya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Tunduma ambapo nafasi yake inachukuliwa na Mariam Chaurembo.

“Amemteua Ndugu Fabian Manoza Said kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Momba. Ndugu Said anachukua nafasi ya Ndugu Butamo Nuru, Ndalahwa ambaye uteuzi wake umetenguliwa,” imebainisha taarifa ya Ikulu.

Kabla ya uteuzi huo, Said alikuwa Afisa Usimamizi Mkuu wa Mitihani, Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa na amewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu.

Aidha, Rais Samia amemteua Selwa Abdalla Hamid kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga akichukua nafasi ya Athuman Francis Msabila ambaye amesimamishwa kazi kwa shutuma za ubadhirifu.

Novemba 4, 2023 Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Mohammed Mchengerwa alimuagiza Katibu Mkuu wa Tamisemi kumsimamisha kazi Msabila baada ya kubainika kuhusika kufanya vitendo vya ubadhirifu akiwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ujiji.

Aidha, Rais Samia amemhamisha kituo cha kazi Dk Peter Maiga Nyanja, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Muleba kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe.

Dk Nyanja anachukua nafasi ya Maryam Ahmed Muhaji ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Manyara.

Mabadiliko haya ya watendaji wa Serikali yamekuja ikiwa zimepita siku tano tu tangu Rais Samia afanye mabadiliko ya viongozi wa ngazi mbalimbali za mikoa, wilaya pamoja na halmashauri nchini.


Soma zaidi : Rais Samia ateua, atengua na kuhamisha viongozi wa mikoa, wilaya, halmashauri


Huenda mabadiliko haya yanalenga kuboresha utendaji kazi wa watumishi wa umma na kuweka nidhamu katika matumizi ya rasilimali za umma na kuwahudumia vema wananchi. 

Wengine walioteuliwa 

Rais Samia amemteua Balozi Meja Jenerali Paul Kisesa Simuli kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uganda.

Meja Jenerali Simuli aliteuliwa kuwa balozi na Rais Samia Mei 22, 2023 ambapo awali alikuwa Mkuu wa Utumishi Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.

Mwingine  ni  Dk Khamis Hassan Mwinyimvua aliyeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TAA). akichukua nafasi ya Profesa LonginusRutasitara ambaye amemaliza muda wake.

“Uteuzi na uhamisho huu unaanza tarehe 18 Desemba, 2023,” imebainisha taarifa ya Ikulu.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...