Rais Samia apendekeza mbinu kuharakisha usikilizwaji kesi mahakamani

October 6, 2021 9:01 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Rais Samia Suluhu Hassan, akikata Utepe kuzindua rasmi Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki katika eneo la National Capital City Jijini Dodoma leo tarehe 06 Oktoba, 2021. Picha| Ikulu.


  • Ni kwa kutumia mifumo ya tehama.
  • Kutokukubali kirahisi kubadilisha mahakimu na tarehe za kesi husika.
  • Aagiza ubora maamuzi mahakama za mwanzo kusimamiwa vizuri.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameiagiza Mahakama ya Tanzania kuongeza kasi ya kushughulikia tatizo la ucheleweshaji wa kesi mahakamani kwa kutumia mifumo ya Tehama na kutokukubali kirahisi kubadilisha mahakimu na tarehe za kesi zilizopangwa.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza leo Oktoba 6, 2021 jijini Dodoma wakati akizindua vituo jumuishi vya utoaji haki jijini Dodoma (NCC) amesema licha ya changamoto mbalimbali za mahakama lakini suala la ucheleweshaji wa kesi linatakiwa kupewa kipaumbele kinachostahiki.

Amesema usikilizwaji wa kesi unaweza kwenda kwa haraka endapo mahakama haitokubali kirahisi kubadilisha mahakimu wa kesi walizopangiwa.

“Ninawasihi mlipe kipaumbele kinachostahiki suala la kuzisikiliza kesi haraka haraka. Msikubali kirahisi kubadilisha mahakimu au tarehe za kusikiliza kesi kwa sababu hilo nalo ni moja ambalo linafanya kesi zichelewe,” amesema Rais Samia.

Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema matumizi ya mifumo ya Tehama ndani ya mahamaka pia yanaweza kupunguza tatizo la mlundikano wa kesi kwa sababu inatoa fursa ya kuona mwenendo wa kila kesi na zipi zinatakiwa zipewe kipaumbele ili wananchi wapate haki kwa wakati.

“Mfumo wa Tehama unaotumika unampa Jaji Kiongozi kujua kesi gani imekaa kwa muda gani haijasikilizwa. Kwa hii itashtua mahakama lakini pia itashtua wale wengine wanaochelewesha wapelelezi, polisi, mawakili na magereza na wenyewe watapata msukumo kwamba kuna kesi tunaichelewesha lazima tuwajibike isikike na haki ipatikane,” amesisitiza Rais.

Amesema anafahamu kuwa licha ya mahakama kuanza kutumia mahakama mtandao (Mobile court) na Tehama bado inakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa intaneti, jambo ambalo ameagiza wizara zinazohusika zilifanyie kazi.

“Nafahamu mnakabiliwa na ufinyu wa bandwidth kutokana gharama kuwa juu. Hivi sasa mnalipia bandwidth ya Sh100 milioni kutoka kwenye mkongo wa Taifa wakati mahitaji yenu ni Sh400 milioni.

“Hivyo naelekeza Mtendaji Mkuu wa Mahakama kukutana na viongozi wa Wizara ya Mawasiliano na Wizara ya Fedha kushughulikia suala hilo,” amesema Rais na kuongeza kuwa “mtakapokwama mlango uko wazi kama mlango wa mahakama ulivyo wazi, naomba mje kwangu.” 

Amesema katika karne hii tuliyonayo, mahakama ni lazima zitumie miundombinu laini (soft infastructure) kufikisha haki kwa wananchi.
 
Aidha, ameiagiza mahakama kusimamia vizuri ubora wa maamuzi yanayotolewa katika mahakama za mwanzo ili kupungua malalamiko kutoka kwa wananchi na kuchelewa upatikanaji  wa haki.“Muungalie usimamizi wa ubora kwenye mahakama za mwanzo. 

Malalamiko mengi ya mahakama yanahusu mahakama za mwanzo, kule kutupiwe jicho vizuri sana,” amesema Rais.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV

Sakata bei ya mafuta kupanda latua BoT, Naibu Gavana atoa ufafanuzi

Sakata bei ya mafuta kupanda latua BoT, Naibu Gavana atoa ufafanuzi

Nukta TV

BoT yabakiza Riba ya Benki Kuu 5.75% kudhibiti mfumuko wa bei

BoT yabakiza Riba ya Benki Kuu 5.75% kudhibiti mfumuko wa bei

Nukta TV