Rais Samia afanya mabadiliko Baraza la Mawaziri, afuta na kuunda wizara mpya
- Wizara zilizoundwa ni pamoja na naibu waziri mkuu, wizara ya ujenzi na wizara ya uchukuzi.
- Baadhi ya mawaziri wahamishwa wizara, wengine watolewa nje ya baraza la mawaziri.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri ambapo ameunda nafasi ya naibu waziri mkuu pamoja na kufuta na kuanzisha wizara mpya ikiwemo Wizara ya Ujenzi.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu leo Agosti 30, 2023 inabainisha kuwa Rais Samia amefuta Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na badala yake ameunda wizara mpya mbili ambazo ni Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi.
Aidha taarifa hiyo inabainisha kuwa Rais Samia ameboresha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuongeza nafasi ya naibu waziri na katibu mkuu watakaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.
“Katika mabadiliko hayo Rais amemteua naibu waziri mkuu, mawaziri wanne, naibu mawaziri watano, makatibu wakuu watatu na naibu makatibu wakuu watatu. Vilevile amewabadilisha wizara baadhi ya mawaziri na makatibu wakuu,” inabainisha taarifa hiyo.
Soma zaidi
-
Matukio makubwa ya kisiasa ya kukumbukwa mwaka 2022
-
Kutana na kuku anayeuzwa Sh800,000 Tanzania
-
Rais Samia abadilisha miundo ya wizara, Kitila Mkumbo ateuliwa waziri
Mawaziri walioteuliwa
Aliyekuwa Waziri wa Madini Dotto Biteko sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Nishati pamoja na Naibu Waziri Mkuu ambapo atakuwa anaratibu shughuli za Serikali.
Wengine walioteuliwa ni Jerry William Silaa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anthony Peter Mavunde aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo kuwa Waziri wa Madini na Profesa Makame Mnyaa Mbarawa aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi amekuwa Waziri wa Uchukuzi.
“Innocent Lugha Bashungwa, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ameteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi, Godfrey Msongwe Kasekenya aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Alexander Pastory Mnyeti, Mbunge wa Jimbo la Misungwi ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, ” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi huku Judith Salvio Kapinga ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (Ruvuma) ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati; na Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Jimbo la Mkinga ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.
Waliohamishwa vituo
Jumla ya mawaziri na manaibu waziri saba wamehamishwa wizara zao ambapo January Yusuf Makamba amehamishwa kutoka Wizara ya Nishati kwenda kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, huku Stergomena Lawrence Tax akirejeshwa kwenye Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Mohamed Omary Mchengerwa amehamishwa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -Tamisemi, ambapo Angellah Jasmine Kairuki aliyekuwepo Tamisemi amekwenda kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
“Damas Daniel Ndumbaro amehamishwa kutoka Wizara ya Katiba na Sheria kwenda kuwa Waziri wa Utamaduni… Balozi Dk. Pindi Hazara Chana amehamishwa kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenda kuwa Waziri wa Katiba na Sheria,” inaeleza taarifa kutoka ikulu.
Aidha, Stephen Lujwahuka Byabato amehamishwa kutoka Wizara ya Nishati kwenda kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki atakayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu uteuzi huo umeanza mara moja, na viongozi wote wataapishwa kesho kutwa Septemba Mosi, Ikulu ndogo ya Zanzibar.
Latest



