Rais Samia aagiza kuanzishwa kwa tovuti ya nyaraka za viongozi
- Asema itasaidia kutambua michango ya viongozi kwa taifa, historia ya nchi na Bara la Afrika.
- Ni baada ya kukoshwa na tovuti ya Dk. Salim Ahmed Salim iliyozinduliwa leo.
- Chuo cha diplomasia kubadilishwa jina kuenzi mchango wa Dk. Salim katika uga huo.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameagiza kuanzishwa kwa tovuti ya Serikali ya kuhifadhi kumbukumbu za viongozi waliowahi kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali wakiwemo marais wastaafu pamoja na mawaziri wakuu.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika hafla ya wa tovuti ya nyaraka za aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Katibu Mkuu wa Umoja wa Afrika (AU) Dk. Salim Ahmed Salim, leo Septemba 30, 2023 amewaambia washiriki kuwa tovuti hiyo itasaidia kutambua michango ya viongozi, historia ya nchi na Bara la Afrika.
“Tovuti kama hizi zinasaidia kukuza na kuimarisha uelewa wa juhudi za kila mmoja wetu, historia ya nchi yetu na Bara la Afrika, shughuli hii imefungua macho umuhimu wa kufungua tovuti hizi…
…twende kwenye muelekeo huu kama wa Dk. Salim tukatengeneze tovuti ya Serikali ya kuweka kumbukumbu za viongozi wetu,” amesema Rais Samia jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Rais Samia tovuti ya Dk. Salim inaakisi safari ya maisha yake kama kiongozi, mwanasiasa na mwanadiplomasia mahiri, huku ikitoa nafasi kwa watu kufahamu historia yake,Taifa lake na Bara la Afrika.
“Binafsi nimepitia tovuti hii na nimebaini kwa mara ya kwanza kutakuwa na tovuti ya kipekee inayoakisi historia ya nchi yetu kupitia darubini na simulizi za Dk. Salim Ahmed Salim,” ameongeza Rais Samia.
Soma zaidi : Rais Samia afanya mabadiliko Baraza la Mawaziri, afuta na kuunda wizara mpya
Tovuti hiyo ni muunganiko wa hotuba, barua, makala zilizokatwa kutoka magazetini, machapisho ya kitafiti, picha pamoja na video kumhusu Dk. Salim ambavyo vinaleta shauku na chachu ya kujifunza kutoka kwake.
Hata hivyo, uwepo wa tovuti ya rasmi ya Serikali huenda ukaleta ahueni kwa kurahisisha upatikanaji wa tawasifu na historia za viongozi wa Taifa kwa kuwa kwa muda mrefu hakukuwa na utaratibu maalumu wa kuhifadhi kumbukumbu hizo.
Baadhi ya viongozi wachache hutumia njia ya vitabu kuwasilisha historia na kumbukumbu zao ambapo wakiwemo marais wastaafu wa Tanzania, Hayati Benjamin Mkapa, na Ali Hassan Mwinyi huku Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikwete akiwa mbioni kuandika kitabu chake.

Dk. Salim Ahmed Salim akihutubia katika mojawapo ya Mkutano wa Umoja wa Afrika (AU). Pichal tovuti ya Salim Ahmed Salim
Dk. Salim Ahmed Salim ni nani?
Salim Ahmed Salim ni Waziri Mkuu mstaafu wa tano wa Tanzania, aliyeshika nafasi hiyo kuanzia mwaka 1984 hadi 1985 nafasi yake ikichukuliwa na Jaji Joseph Sinde Warioba.
Baadhi ya nyadhifa ambazo amewahi kuhudumu hapa nchini ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje (1980-84) ,Naibu Waziri Mkuu (1986-89), Waziri wa Ulinzi (1986 – 1989) pamoja na kuwa Rais wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere nyadhifa anayoishikilia hadi sasa.
Kimataifa Dk. Salim anatambulika vyema katika uga wa diplomasia kwa kuwa amewahi kuwa Balozi wa Tanzania katika mataifa kama (Misri, Cuba, India, pamoja na China.
Aidha amewahi kuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa (UN) pamoja na kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Afrika wakati huo ikiitwa (O.A.U) kwa muda wa miaka 12, na alihusika kutafuta suluhu ya amani nchini Sudan mwaka 2004 – 2008.
Chuo cha diplomasia kuitwa jina lake
Ili kuuenzi mchango wake katika uga wa diplomasia Rais Samia amesema Chuo Cha Diplomasia kilichopo jijini Dar es Salaam na sasa kitaitwa Dk. Salim Ahmed Salim Center for Foreign Relations.
Latest