Rais Magufuli: Sakata la kutekwa Mo Dewji limeacha maswali mengi
- Amesema sakata hilo limeacha maswali mengi ambayo watanzania wataka kupatiwa majibu.
- Amesema mazingira aliyotekwa mfanyabiashara huyo bado yana utata na polisi mpaka leo wamekaa kimya na hakuna mtuhumiwa aliyefikishwa mahakani.
- Jeshi la Polisi limetakiwa kurekebisha dosari ndogo ndogo za utendaji linalochafua taswira ya jeshi hilo.
Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza Rais John Magufuli amezungumzia kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji maarufu kama Mo na kubainisha kuwa sakata hilo limeacha maswali mengi kwa Watanzania ambayo yanahitaji majibu kutoka kwa Jeshi la Polisi kuhusu kutekwa kwake.
MO alitekwa Oktoba 11, 2018 akiwa anaingia kufanya mazoezi katika hoteli ya Collesseum Oysterbay jijini hapa, alipatikana akiwa salama baada ya siku nane katika viwanja vya Gymkana pamoja na gari ambalo vyombo vya dola vilikuwa vikilisaka.
Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Machi 4, 2019) wakati akiwaapisha makamishna wa Jeshi la Polisi na Mawaziri wapya Professa Palamagamba Kabudi wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Balozi Dk Augustine Mahiga wa Katiba na Sheria, amesema watanzania walitajia kuona watekaji na watu wengine wanaoshukiwa kumteka Mo wangefikishwa mahakamani lakini mpaka leo hakuna maelezo ya uhakika kuhusu sakata hilo.
“Niwatolee mfano tu alipotekwa yule Mohammed (Mo Dewji) tulipata stori nyingi za maelezo ametekwa na wazungu wa aina fulani lakini lilipokuja kumalizika lile suala linaweka maswali mengi zaidi,” amesema Rais Magufuli.
Amesema maswali yanajitokeza zaidi ni katika mazingira aliyotekwa mfanyabiashara huyo na jinsi watekaji wake walivyofanikiwa kumtelekeza katika viwanja vya Gymkana pamoja na gari na silaha.
“Kwamba huyu aliyetekwa amekutwa Gymkana usiku.Watu wanajiuliza Eeh! amefikaje pale lakini alipokuwa amekutwa pale na bunduki zikaachwa pale. Unajiuliza huyu mtekaji amemleta hapa na ameamua kuondoka na aliondoka na bunduki akaziacha na angekutana na watu wanaomtafuta njiani polisi?,” amehoji Rais Magufuli na kuongeza;
“Wakajaribu kulichoma gari lakini baadaye tunamuona aliyetekwa anakunywa chai na Mambosasa (Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam).”
Zinazohusiana:
- RC Makonda aeleza mazingira ya kutekwa Bilionea Mo Dewji
- Dau la Bilioni 1 kutolewa kwa atakayefanikisha kupatikana kwa Bilionea Mo Dewji
- Polisi kumsaka Mo Dewji nje ya Tanzania.
Utata ulizidi kujitokeza zaidi baada ya polisi kubaini nyumba aliyohifadhiwa Mo na watekaji wake ambapo Rais amesema mpaka leo mwenye nyumba hayajakamatwa kusaidia polisi kuwatia nguvuni watekaji.
“Sasa ile inatoa maswali mengi ambayo hayana majibu, kesho yake wangemuona yuko mahakamani na angeweza akawataja lakini watanzania wanataka kuona huyo mmliki wa nyumba angalau akajibu hiyo nyumba yako mtu anaingia anakaa siku ngapi bila kujua walioingia kwenye nyumba yako ni nani? Hakuna majibu,” amesema.
Amesema kutokana na mambo madogo madogo kama hayo, yanalitia doa Jeshi la Polisi katika utendaji wake licha ya ukweli kuwa jeshi hilo linafanya kazi nzuri ya kulinda raia na mali zao.
“Haya hata kama watanzania watanyamaza lakini mioyo yao hataikuwa clear (amani). Sasa vitu kama hivi vinatia dosari, hizi dosari ndogo ndogo zinalichafua jeshi la polisi,” amesema.
Hata hivyo, ameliagiza jeshi la polisi kuwarekebisha maafisa wachache wanaolichafua jeshi hilo ikiwemo kuwashusha vyeo na kuwahamisha vituo vya kazi na kuendelea kufuatilia mienendo ya utendaji wao.
Latest