Rais Magufuli: Kwanini bado sijahamia Dodoma
Rais John Magufuli akiwa na mama yake Suzana Magufuli. Picha|Mtandao.
- Dk Magufuli ameeleza kuwa kilichomchelewesha kuhamia katika makao makuu ya nchi ni kwa sababu anauguza mama yake mzazi Suzana Magufuli ambaye bado yupo hospitali.
- Amesema kwa sasa hana sababu yoyote ya kumzuia na yuko njiani kuhamia Dodoma.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema amechelewa kuhamia katika makao makuu ya nchi, jijini Dodoma kwa sababu anauguza mama yake mzazi Suzana Magufuli ambaye yuko hospitali lakini muda si mrefu atakamilisha azma ya Serikali yake kuhamia katika jiji hilo.
Oktoba 14 mwaka jana alipomtembela mjane wa Baba wa Taifa, mama Maria Nyerere nyumbani kwake Masaki Jijini Dar es Salaam, alisema hadi Desemba 2018 angekuwa amehamia jijini Dodoma lakini hakufanya hivyo wakati ulipofika.
Hata hivyo, Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Aprili 13, 2019) wakati wa uzinduzi wa Mji wa Serikali uliopo eneo la Mtumba jijini Dodoma, amesema alichelewa kuhamishia shughuli zake za kiserikali katika jiji hilo kama alivyoahidi kutokana na kuuguza mama yake mzazi ambaye bado yuko hospitali akipata matibabu.
“Na mimi nataka kuwahakikishia kuwa ninakuja (Dodoma) nilichelewa kidogo baada ya kuuguliwa na mama yangu ambaye mpaka sasa hivi yuko hospitalini, hawezi kuzungumza wala hawezi kula,” amesema Rais.
Zinazohusiana:
- Rais Magufuli kuzuru Mwanza, Simiyu na Mara kwa siku saba
- Rais Magufuli awafuta kazi Tizeba, Mwijage, joto la korosho likipanda
Dk Magufulli amesisitiza kuwa kwa sasa hakuna jambo la kumchelewesha kuhamia Dodoma na yuko njiani kuhamia katika jiji hilo kwasababu mipango yote imekamilika.
“Lakini nataka niwahakikishie mimi ninakuja Dodoma kwa sababu hakuna cha kunichelewesha kuja Dodoma na ndiyo maana kila ninapokuja hapa ninapenda kukaa siku nyingi kwa ujumla nimekwisha hamia hapa Dodoma,” amesisitiza Rais Magufuli.
Mpaka sasa tayari Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wamehamia katika jiji hilo ambalo ni makao makuu ya nchi ikiwa ni hatua ya kutekeleza maono ya muda mrefu ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye leo watanzania wanaadhimisha siku ya kuzaliwa kwake.
Latest