Rais Magufuli azindua maktaba kubwa zaidi Afrika Mashariki

Maktaba mpya ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyozinduliwa leo Jijini Dar es Salaam. Picha| Ikulu.
- Imejengwa kwa gharama ya Sh93.6 bilioni ikiwa ni msaada kutoka Serikali ya China na inakuwa maktaba kubwa kuliko maktaba zote ambazo China imezijenga barani Afrika.
- Imeunganishwa na mfumo mzuri wa kielektoniki katika uhifadhi wa machapisho mbalimbali yatakayotumiwa kujisomea kwa wanafunzi.
- Pia imeunganishwa na mfumo wa umeme wa jua kwa ajili ya kuhakikisha inakuwa na umeme wa uhakika kwa muda wote.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amezindua maktaba ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) itakayowanufaisha wanajumuiya wa chuo hicho wakiwemo wanafunzi kujipatia maarifa na ujuzi kutoka katika vitabu na tafiti mbalimbali.
Uzinduzi huo umefanyika leo Novemba 27, 2018 ikiwa ni miezi 18 tangu Raisi Magufuli aweke jiwe la msingi la ujenzi wa maktaba hiyo Juni 2016.
Maktaba hiyo kubwa Afrika Mashariki na Kati imejengwa kwa gharama ya Sh93.6 bilioni ikiwa ni msaada kutoka Serikali ya China na inakuwa maktaba kubwa kuliko maktaba zote ambazo China imezijenga barani Afrika.
Katika taarifa yake Makamu Mkuu wa Chuo cha UDSM, Prof. William Anangisye amesema majengo ya maktaba hiyo yenye ghorofa mbili yamechukua eneo lenye ukubwa wa meta za mraba 20,000 yakiwa na uwezo wa kuhifadhi vitabu 800,000, kukalisha watumiaji 2,100 kwa wakati mmoja,
Pia yana kompyuta 160 zilizounganishwa na mtandao kwa ajili ya kusoma vitabu kwa njia ya kielektroniki, ofisi za wafanyakazi, eneo la wanafunzi wenye mahitaji maalum na ukumbi wa kisasa wa mihadhara wenye uwezo wa kuchukua watu 600.
Prof. Anangisye amesema maktaba hiyo ya kisasa imeunganishwa na mfumo wa umemejua wenye kilovoti 280, ambazo zitatumika katika kuwashia taa na viyoyozi ili kuhakikisha muda wote jengo linakuwa na umeme wa kutosha na mazingira tulivu ya kusomea.
Mchakato wa kujenga maktaba hiyo ulitokana na juhudi za Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mtaafu Jakaya Kikwete na viongozi wa chuo hicho waliofanya mipango na harakati za kujenga maktaba kwa msaada wa Serikali ya China.
“Naipongeza sana, Serikali ya awamu ya nne kwa kuhakikisha kunapatikana pesa ya ujenzi na maandalizi ya kujenga maktaba hii, mimi nimekuja kujenga na kuweka jiwe la msingi,” amesema Rais.
Rais ameweka bayana furaha yake kwa kumalizika kwa maktaba hiyo na kwa serikali ya China kutoa pesa bila masharti ili kuweza kufanikisha ukamilifu wa jengo hilo la maktaba.
“Shukrani iende kwa watu wa China ni marafiki zetu hawa, wanatupa msaada bila masharti lakini wengine wangetupa masharti ya kila namna,” anasema Rais.
Watumiaji wa maktaba hiyo wametakiwa kuitunza na kuhakikisha kuna vitabu vya kutosha kwa ajili ya kujisomea, ili wanafunzi waweze kusoma vizuri na kupata shahada zilizokuwa bora kwa manufaa ya nchi na jamii kwa ujumla.
Majengo ya maktaba hiyo yenye ghorofa mbili yamechukua eneo lenye ukubwa wa meta za mraba 20,000 yakiwa na uwezo wa kuhifadhi vitabu 800,000, kukalisha watumiaji 2,100 kwa wakati mmoja. Picha| Ikulu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Joyce Ndalichako ametoa shukrani za dhati kwa Rais Magufuli na wakandarasi waliofanikisha ujenzi wa maktaba hiyo, na kuweka wazi kuwa watakuwa makini katika utunzaji wa maktaba hiyo iweze kudumu kwa muda mrefu.
“Wote watakaokuwa na mipango ya kuihujumu hii maktaba tutawashughulikia,” amesema Ndalichako.
Ameweka wazi kuwa maktaba hiyo imewekewa mfumo mzuri wa kielektoniki katika uhifadhi wa machapisho mbalimbali yatakayotumiwa kujisomea kwa wanafunzi.
“Kuna machapisho zaidi ya milioni moja ya kielektroniki, hivyo maktaba hii ni chachu katika elimu inayotolewa nchini,” ameeleza Ndalichako.
Hata hivyo maktaba hiyo haitasomewa na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pekee bali na wanataaluma wengine kutoka elimu ya juu kwa utaratibu utakaowekwa na Chuo hicho, ili kila mmoja anufaike katika kujiongezea maarifa kupitia vitabu na miundombinu mingine ya kujisomea iliyopo katika maktaba hiyo.
Chuo hicho kimejipanga kutenga pesa za kutosha kwa ajili ya kununua vitabu kwa watu kujifunzia wakiwa katika maktaba hiyo ya kisasa.
“Mwaka wa fedha wa 2017/2018 tumetenga Sh1.78 bilioni kwa ajili ya mchakato wa ununuzi wa vitabu unaoendelea,” amesema Prof. Anangisye.