Rais Magufuli, Ramaphosa wajadili uwekezaji wenye manufaa
- Amesema uwekezaji huo utasaidia kupunguza gharama za kuagiza dawa za binadamu nje ya nchi.
- Itaisaidia Tanzania kutekeleza jukumu lake la kusambaza dawa katika nchi za SADC
- Rais Ramaphosa naye awakaribisha Watanzania kuwekeza Afrika Kusini.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewaalika wafanyabiashara na wawekezaji wa Afrika Kusini kuja kwa wingi nchini kwa ajili ya kuwekeza katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi wa viwanda vya dawa za binadamu.
Oktoba, 2018 Tanzania ilipewa heshima na jukumu la kununua dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwa ajili ya nchi zote 16 za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kutoa ushauri, kusimamia ununuzi wa dawa na kupokea uhitaji wa manunuzi ya dawa.
Dk Magufuli aliyekua akizungumza leo (Agosti 15, 2019) Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati wa mazungumzo yake na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amesema Tanzania na Afrika Kusini ni mataifa rafiki yenye historia ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Amesema Serikali imeendelea kuimarisha na kuweka mazingira wezeshi ikiwemo ujenzi wa miundombionu ya uhakika, pamoja na uimarishaji wa mifumo ya kitaasisi katika usimamizi wa kodi na biashara.
Amewakaribisha wawekezaji wa nchi hiyo kuja Tanzania kujenga viwanda vya dawa ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kuigiza dawa na vifaa tiba nje ya nchi, wakati huo huo kuiwezesha kukidhi mahitaji ya dawa la SADC.
“Katika Bajeti ya Serikali kwa mwaka tunatenga kiasi cha Sh270 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa madawa nje ya nchi, tunawaomba wawekezaji wa Afrika Kusini waje Tanzania wajenge viwanda vya madawa kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tumepunguza gharama kubwa za uagizaji wa madawa kutoka nchi ya nchi,” amesema Rais Magufuli.
Soma zaidi:
- Kiswahili chapendekezwa kuwa lugha rasmi SADC
- Maagizo matano ya Magufuli kukuza uchumi wa viwanda nchi za SADC
Amebainisha kuwa Tanzania imejipanga kikamilifu katika kuimarisha mfumo imara wa uchumi wake ikiwemo ujenzi wa viwanda, ambayo ndiyo dira na dhamira ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Katika hatua nyingine, amesema Tanzania ipo tayari kufanya biashara na Afrika Kusini katika ununuzi wa vifaa mbalimbali ikiwemo magari, ambayo Tanzania imekuwa ikiyanunua katika nchi za mbali, huku akitolea mfano wa pikipiki zinazotumika katika Mkutano wa 39 wa SADC zimenunuliwa kutoka nchini Afrika Kusini.
“Katika Nchi za SADC, mwaka 2018 Tanzania imeongoza katika ukanda wa SADC kwa thamani ya mauzo ya bidhaa zake Nchi ya Afrika Kusini iliyofikia thamani ya Dola milioni 742.02 na biashara baina ya Mataifa haya ilifikia thamani ya Dola 1.18 bilioni kutoka Dola 1.11 bilionimwaka 2017,” amesema Rais Magufuli.
Rais John Magufuli (kulia) akiwa na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa wakati akiwasili Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha|Michuzi.
Baada ya Rais Ramaphosa kumaliza ziara yake, ataungana na mwenyeji wake kushiriki katika mkutano wa Wakuu wa nchi utakaofanyika Agosti 17 na 18 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Rais Ramaphosa amesema ziara yake nchini Tanzania ni kielelezo cha kuendelea kuimarika kwa ushirikiano baina ya mataifa hayo na kusema Serikali yake itaweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania kwenda nchini Afrika Kusini kufanya biashara na uwekezaji.
Amesema Serikali yake inatambua umuhimu wa sekta ya biashara na uwekezaji katika kukuza uchumi katika nchi za SADC kupitia ajenda ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030 ambayo imedhamiria katika kujenga mazingira bora ya biashara katika Jumuiya hiyo.