Rais Hichilema atua Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku moja

August 2, 2022 9:29 am · admin
Share
Tweet
Copy Link

Rais Samia Suluhu Hassan akisalimiana na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Zambia Hakainde Hichilema mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Terminal one Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya ziara ya siku moja nchini. Picha | Ikulu Tanzania.


  • Ni ziara yake ya kwanza nchini Tanzania  tangu awe Rais wa Zambia 
  • Kufanya mazungumzo na Rais Samia.
  • Anatarajia kutembelea Bandari ya Dar es Salaam na reli ya kisasa ya SGR.

Dar es Salaam. Rais wa Zambia Haikande Hichilema awewasili nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku moja akitarajia kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan na kutembelea baadhi ya miundmbinu ikiwemo Bandari ya Dar es Salaam. 

Hichilema amewasili leo Agosti 2, 2022 majira ya saa 10:00 asubuhi kwa ndege ya Rais wa Jamhuri ya Zambia yenye namba TJ-9 iliyotua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es salaam. 

Rais huyo mwenye umri wa miaka 60 amepokelewa na mwenyeji wake Rais Samia, viongozi wa Serikali na vikundi vya ngoma za asili zilizokuwepo uwanjani hapo.

Mara baada ya kupokelewa Rais Hichilema alikagua gwaride la heshima baada ya  kuimbwa kwa nyimbo za Taifa za mataifa yote mawili. Baada ya gwaride hilo, Rais Samia alifanya utambulisho wa viongozi alioambatana nao katika mapokezi hayo kabla ya kuanza safari ya kuelekea Ikulu.

Kwa mujibu wa gazeti la Lusaka Times la nchini Zambia,  ziara ya Hichilema ni mwaliko wa Rais Samia ambapo viongozi hao wanatarajia kujadiliana mambo mbalimbali ikiwemo kuimarisha ushirikiano wa mataifa yote mawili katika sekta ya biashara, uwekezaji na miundombinu.

Gazeti hilo limeeleza kuwa baadhi ya maeneo yatakayojadiliwa ni pamoja na Bomba la mafuta la Tanzania-Zambia (Tazama) na mpaka wa Tunduma unaotenganisha nchi hizo mbili.

Rais Hichilema baada ya mazungumzo hayo anatarajia kutembelea Bandari ya Dar es salaam pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR unaoendelea. 

Hii ni ziara ya kwanza ya kikazi ya Rais Hichilema nchini Tanzania tangu alipoingia madarakani mnamo Agosti 24, 2022 akichukua nafasi ya mtangulizi wake Edgar Lungu ambaye alimshinda kwa takribani kura milioni 1.

Rais huyo wa saba wa Zambia aliingia madarakani kupitia chama kikuu cha  upinzani nchini humo  cha  United Party for National Development (UPND) katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali.

Tanzania na Zambia zimekuwa zikishirikiana katika masuala mbalimbali yanayolenga kukuza uchumi wa mataifa yote mawili hususan katika sekta ya miundombinu ambapo Zambia hutegemea Bandari ya Dar es salaam kupokea bidhaa zake  ambazo baadhi husafirishwa kupitia reli ya Tazara au barabara.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW