Programu ya kuwainua wasichana kielimu Tanzania yashinda tuzo Unesco

January 22, 2023 9:42 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni GLAMI inayowajenga wasichana ili wajiamini kukabiliana na changamoto katika maisha yao
  • Imeshinda tuzo ya mwaka 2022 ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) ya “Elimu ya Wasichana na Wanawake.”

Dar es Salaam. Huenda wasichana katika mikoa ya kaskazini mwa Tanzania watapata msukumo mpya wa kutimiza ndoto zao za elimu baada ya programu ya GLAMI inayowajengea uwezo wa kujiamini kushinda tuzo ya kimataifa. 

Programu hiyo inafanya kazi ya kuwajenga wasichana ili wajiamini na ambao wanaelewa jinsi ya kukabiliana na changamoto katika maisha yao huku wakiweka kipaumbele katika elimu yao.

GLAMI ni mmoja wa washindi wawili wa tuzo ya mwaka 2022 ya shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) ya “Elimu ya Wasichana na Wanawake.”

Programu hiyo iliyoanzishwa mwaka 2001, imetunukiwa tuzo kwa programu zake mbil (Binti Shupavu na Kisa) ambazo zinasaidia wasichana 7,400 katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha nchiniTanzania kuvuka kwa usalama katika viwango mbalimbali vya elimu, kumaliza masomo yao, na kujiendeleza kuwa viongozi wanaojiamini.

Kulingana na taasisi ya Unesco ya takwimu za elimu na sayansi (UIS), ni asilimia 39 tu ya wasichana wa Kitanzania ndiyo wanaokwenda shule za sekondari na chini ya asilimia 3 wanakwenda elimu ya juu.

“Wasichana nchini Tanzania wanakabiliwa na vikwazo vingi vya kumaliza elimu yao, kuanzia mahitaji ya nyumbani na shuleni hadi shinikizo la kijamii na kiuchumi,” amesema Devotha Mlay, Mkurugenzi Mwenza wa programu za GLAMI baada ya kupokea tuzo hiyo Januari 19, 2023.

Monica Swai, ambaye ni Mkurugenzi Mwenza wa operesheni wa GLAMI anasema licha ya changamoto hizo elimu ni muhimu kwa wasichana akiongeza kuwa

“Utafiti unaonyesha kuwa wasichana wanaomaliza elimu wanaweza kupata ajira bora, kulea familia zenye afya bora, na wana uwezekano mkubwa wa kutanguliza elimu kwa watoto wao. Msichana mmoja aliyeelimishwa huleta athari nzuri ya mabadiliko ambayo hujirudia kwa vizazi vingi,” amesema Monica. 

Wanafunzi katika shule ya msingi ya Zanaki jijini Dar es salaam nchini Tanzania. Picha | Sarah Farhat/World Bank.

Mambo yaliyosaidia kupataza tuzo

Programu ya Binti Shupavu au ‘Binti Jasiri’ iliyozinduliwa mwaka 2017 katika Mkoa wa Kilimanjaro, ni kozi ya stadi za maisha kwa wasichana wenye umri wa miaka 12 hadi 18 ambayo inaendeshwa katika miaka minne ya kwanza ya shule ya sekondari.

Kozi hiyo inashughulikia mada kama vile ujuzi wa kusoma, uongozi wa kibinafsi, afya, na kujiamini kwa lengo la kuongeza viwango vya kuhitimu katika elimu.

Kwa sasa kuna wahitimu 2,934 ambao wameshiriki katika mpango huo, na wasomi 5,146 wa Binti Jasiri walisajiliwa katika shule 22 mwaka 2022.

Asilimia 80 ambao wamepitia program hii hufanya kazi moja kwa moja na wasichana kupitia mikutano ya kila wiki ya klabu ambapo wanajadili mada kama vile afya ya uzazi, na mikakati ya kukabiliana na changamoto za maisha.

“Tunafanya kazi na shule washirika kuwalenga wasichana ambao wanafikiri wako hatarini zaidi na wako katika hatari ya kuacha shule. 

“Mfuko wa dharura wa GLAMI ni kwa ajili ya wanachuo wa Binti Shupavu ambao wanakabiliwa na vikwazo vikubwa ambavyo vinavyowaweka katika hatari ya kuacha shule, kulipia gharama zinazohusiana na karo, vifaa, sare za shule, afya, chakula, na vingine vingi,” anasema Devotha. 

Pia GLAMI inasisitiza kuhusisha na kujenga uhusiano na wazazi tangu binti yao anapojiunga na Binti Shupavu. Wazazi wanapoelewa kile wasichana wanachojifunza, wanasaidia binti zao kufaulu shuleni na zaidi, mitazamo yao inabadilika, na wanakuwa washiriki watendaji zaidi.


Soma zaidi:


Kujenga kujiamini

“Kisa” ni kozi ya uongozi ambayo hutayarisha wasichana wenye umri wa miaka 16 hadi 20 kuhudhuria chuo kikuu na kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao.

Kwa sasa wasichana 2,338 wameandikishwa, na wasichana 4,136 wamemaliza kozi hiyo.

Kozi inajumuisha madarasa ya kila wiki, yakiongozwa na washauri ambao wengi wao ni wahitimu wa program hiyo, pia makongamano matatu ya afya kwa mwaka, siku ya kazi, na miradi ya kila mwaka ambapo wasichana hutambua na kutatua changamoto katika jumii zao.

“Wasichana hujifunza ujuzi muhimu kutoka kwa mtaala wetu, lakini ushindi wa kweli kwa GLAMI ni kuona wasichana hawa wakikua na kufanya kazi pamoja kuweka ujuzi wao mpya katika vitendo. 

“Kujiamini kwao kunaongezeka sana kwa sababu wanajifunza katika mazingira ya kuungana mkono pamoja na wenzao, kutoka kwa mshauri mwanamke aliyeelimika wa chuo kikuu ambaye anaonyesha kile wanachoweza kufanya na kuwa,” anasisitiza Devotha.

Wasomi wa Kisa sio tu wanahitimu kwa viwango vya juu, na alama za juu za mtihani kuliko wenzao, pia wanaripoti kuwa na viwango vya juu vya kujiamini, na kujieleza mwishoni mwa programu.

Devotha na Monica wanasema tuzo ya UNESCO itasaidia programu yao huo kuendelea kukua na kuwafikia wasichana wengi zaidi.

Mwaka huu wa 2023, GLAMI itapanua wigo wa programu yake ya Binti Shupavu hadi mkoani Morogoro Mashariki mwa Tanzania, ambako kiwango cha wasichana wanaoacha shule kiko juu.

“Nia yetu ni kwamba kila msichana wa Kitanzania awe na elimu, ujasiri na uwezo wa uongozi wa kubuni maisha yake kama anavyotaka,” anasema Devotha. 


Tangazo: 


Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW