Prof. Kabudi: Kifo cha Mengi ni pigo kubwa kwa Tanzania

May 7, 2019 11:23 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Viongozi na watanzania waliojitokeza kutoa heshima za mwisho kwa marehemu Reginald Mengi katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam leo. Picha|ITV.


  • Amesema katika kipindi cha uhai wake alishiriki moja kwa moja katika ujenzi wa uchumi kwa kutoa ajira na kuvutia uwekezaji katika sekta za madini, mafuta, gesi na afya.
  • Amesema kifo chake kimekuwa cha ghafla na kimeacha masikitiko makubwa kwa familia na viongozi wa Serikali.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amesema kifo cha Dk Reginald Mengi siyo tu kimeacha pigo kwa familia na wafanyakazi wa makampuni ya IPP, bali hata kwa Serikali kutokana na mchango mkubwa alioutoa katika ujenzi wa uchumi wa nchi. 

Prof. Kabudi aliyekuwa akizungumza kwa niaba ya Rais John Magufuli leo (Mei 7, 2019) wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa marehemu katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam, amesema Tanzania imeondokewa na mtu muhimu katika utekelezaji wa majukumu na ukaribu aliokuwa nao kwa wafanyakazi wake. 

“Kwa niaba ya serikali ninatoa pole kwa uongozi wote wa makampuni ya IPP kwa kuondokewa na mtu muhimu katika utekelezaji wa majukumu yenu na yetu. Ni dhahiri kifo chake ni pigo kwenu na makampuni aliyoyamiliki na kuyaongoza,” amesema Prof. Kabudi.

Amesema katika uhai wake alifanya mambo mengi na kuwa na mchango mkubwa katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi kupitia makampuni ya IPP na biashara nyingi alizozifanya katika sekta ya gesi, mafuta, madini, kilimo na afya.

“Dk Mengi alishiriki moja kwa moja kujenga uchumi wa nchi yetu na kutoa ajira,” amesema Prof. Kabudi.  

Akimuelezea zaidi Dk Mengi, Prof. Kabudi amebainisha kuwa marehemu ameshiriki kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini na kwa namna ya pekee uzalendo kwa nchi yake uliweza kuwavutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza nchini lakini hakusita kuwasaidia wawekezaji na wafanyabiashara wazawa kuwekeza nchini. 

Pia alishiriki kuishauri Serikali katika sera za kiuchumi na wakati wote alikuwa na jawabu la jinsi gani ya kuboresha sera hizo ili zilete tija kwa wananchi. 


Soma zaidi:


Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi amesema kama ilivyo kwa familia, Serikali na dunia imepokea kwa mshtuko mkubwa, simanzi  na masikitiko taarifa ya kifo cha Dk Reginald Mengi. 

“Kwa hali hiyo, kifo cha Dk Mengi kimekuwa cha ghafla mno. Dk Mengi aliondoka nchini akiwa mzima lakini akiwa Dubai aliumwa ghafla na Mungu akamtwaa,” amesema Prof. Kabudi.

Mengi ambaye alizaliwa mwaka 1944 mkoani Kilimanjaro  alifariki dunia mjini Dubai, Falme za Kiarabu (UEA) usiku wa kumakia Mei 2 mwaka huu na anatarajiwa kupumzishwa katika nyumba yake ya milele Machame mkoani Kilimanjaro.

Rais John Magufuli leo amewaongoza waombelezaji kuuaga mwili wa Reginald Mengi katika ukumbi wa Karimjee jini Dar es Salaam. Picha|Michuzi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania (Shiwavata), Ummy Hamis ametoa wito kwa familia, marafiki, Serikali na watu walioguswa na kifo cha Dk Mengi wasiishie kulia na kutoa machozi bali waende mbele kwa kutimiza maoni ya Dk Mengi katika kazi zake ili ziendelee kuishi kizazi kwa kizazi

“Sisi watu wenye ulemavu Dk ametuachia taasisi ya Dk Mengi Foundation, wakati tunaendelea kulia tuangalie tunavyoweza kuwasaidia watu wenye ulemavu katika taasisi hii na kuwasaidia kupitia taasisi zao tupate ukombozi,” amesema Hamis.  

Disemba 7, 2018 Mengi kupitia taasisi yake inayojihusisha na masuala ya watu wenye ulemavu (Dk Reginald Mengi Persons with Disabilities Foundation) ilizindua tuzo za ‘I CAN’ yenye lengo la kuwaenzi na kuwapa motisha walemavu ya kujiona wanaweza. 

Sheria ya Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2010 inatoa haki ya kushiriki na kushirikishwa kikamilifu kwa watu wenye ulemavu katika shughuli zote za kijamii

Akiwasilisha salamu za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole amesema watamkumbuka mzee Mengi kwa sababu alikuwa Bilionea Mjamaa na kwa CCM ujamaa ni imani na Mengi ameishi imani ya CCM inayozingatia usawa wa binadamu, utu wa binadamu na ujamaa na kujitegemea. 

Mpaka umauti unamkuta, Mengi alikuwa mwanachama mtiifu wa chama  wa CCM.

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
15 Jun, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
15 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
15 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Mwenendo wa deni la serikali

Mwenendo wa deni la serikali

Nukta TV

Rais Samia: Uchumi wa nchi unapanda , lakini ukifika kwa watu hali si nzuri

Rais Samia: Uchumi wa nchi unapanda , lakini ukifika kwa watu hali si nzuri

Nukta TV

Gavana Tutuba afichua kiasi cha dhahabu kilichopo BoT thamani yake

Gavana Tutuba afichua kiasi cha dhahabu kilichopo BoT thamani yake

Nukta TV