Polisi waanika nyumba, mtu anayedaiwa kuwatorosha watekaji wa Mo Dewji
- Nyumba hiyo ya ghorofa moja iliyopo Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam inamilikiwa na mabinti wa marehemu Mwasansu.
- Watekaji wa Mo waliipanga nyumba hiyo kupitia kwa dereva wa taxi anayeshikiliwa na polisi ajulikanaye kwa jina la Twalib Mussa mwenyeji wa Tanga.
- Kamanda Mambosasa ameonyesha gari jingine dogo akidai kuwa nalo lilitumika katika kutekeleza tukio la kumteka Mo.
Dar es Salaam. Mwezi mmoja tangu kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji jeshi la polisi leo limeweka wazi nyumba inayodaiwa kutumika kumhifadhi bilionea huyo alipokuwa mateka kwa siku tisa.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa leo (Novemba 11, 2018) amewaonyesha wanahabari nyumba hiyo ya ghorofa moja iliyopo Mbezi Beach jijini hapa akieleza kuwa watekaji wa Dewji maarufu kama Mo waliipanga kabla ya kufanya tukio hilo.
Amesema watekaji wa Mo waliipanga nyumba hiyo kupitia kwa dereva wa taxi anayeshikiliwa na polisi ajulikanaye kwa jina la Twalib Mussa mwenyeji wa Tanga.
“Aliwakaribisha wafanyabiashara hao waliojitambulisha kuwa ni wafanyabishara wa madini wakiwa ni ‘Wasouth Africa’ (raia wa Afrika Kusini).
“Walihifadhiwa kwa malipo ya Dola za Marekani 1,500 (Sh3.4 milioni) kwa mwezi. Kati ya fedha hizo, Dola za Marekani 1,300 (takriban Sh3 milioni) zilipelekwa kwa mhusika wa nyumba na cha juu alikuwa anapokea bwana Twalib,” amesema Mambosasa wakati akiwaonyesha wanahabari nyumba hiyo aliyodai inamilikiwa na mabinti wa marehemu Mwasansu.
Zinazohusiana:
- RC Makonda aeleza mazingira ya kutekwa Bilionea Mo Dewji
- Dau la Bilioni 1 kutolewa kwa atakayefanikisha kupatikana kwa Bilionea Mo Dewji
- Polisi kumsaka Mo Dewji nje ya Tanzania
Taarifa hiyo ya polisi inakuja ikiwa ni majuma matatu tangu Mo apatikane baada ya kutelekezwa na watekaji wake katika viwanja vya Gymkhana jijini hapa usiku wa kuamkia Oktoba 20 mwaka huu.
Mbali na nyumba hiyo, Mambosasa ameonyesha gari jingine dogo akidai kuwa nalo lilitumika katika kutekeleza tukio la kumteka Mo na kwamba lilionekana hadi katika kamera za usalama (CCTV) wakati wakifanya uchunguzi.
Hii ndiyo nyumba inayodaiwa Mo Dewji alihifadhiwa baada ya kutekwa iko Mbezi Beach, Jijini Dar es Salaam. Picha| Vidokezo
Kamanda huyo amesema Mussa ndiye aliyewapeleka watekaji hao kupanga nyumba hiyo na alihusika kwa kiasi kikubwa katika kuwatorosha nje ya Dar es Salaam.
“Huyu bwana ameshiriki mwanzo mwisho. Amekodisha hapa (kwenye nyumba alipokuwa ametekwa Mo) na ndiye aliyetumika kuwachukua kutoka eneo walipomuacha Mo Dewji na aliwapeleka hadi Ubungo kwenda nje ya Dar es Salaam,” amesema Mambosasa.
Katika mchakato wa upelelezi wa tukio hilo la utekaji lililofanywa nje ya hoteli ya Colosseum Oyster Bay, Mambosasa amesema watu 40 walitiwa mbaroni kwa ajili ya mahojiano ya kusaidia upelelezi.
Hadi sasa, amesema bado wanawashikilia watu 13 na wengine walipewa dhamana na kila mmoja anahojiwa kutokana na namna ya ushiriki wake katika tukio hilo lililotikisha jiji hili majuma manne yaliyopita.
Huku akiwananga wakosoaji wa polisi katika tukio hilo, Mambosasa amesema kuwa uchunguzi wa jeshi hilo ndio uliofanikisha kubaini nyumba na mtu aliyehusika kuwapangisha na kuwatorosha watekaji hao.
“Kuna watu walisema hatuwezi kubaini waliotenda hili. Watu ‘walideclare’ (walitangaza) tutafute wapelelezi wa nje ya nchi,” amesema na kueleza kuwa polisi wataendelea kuwasaka wote waliohusika na kuwapeleka mahakamani.
“Kila linapotokea jambo lisilo la kawaida polisi tuachiwe tufanye upelelezi,” amesema.