Papa: ‘Samaki bubu asiyelala’

August 23, 2021 8:15 am · Nasibu
Share
Tweet
Copy Link
  • Hutomkuta papa amelala usingizi hata siku moja, yeye hutulia tu.
  • Ni moja kati ya viumbe ambao wamenyimwa uwezo wa kutoa sauti.
  • Amekuwa kivutio kikubwa kwa shughuli za utalii.

Hakuna kiumbe anaogopeka majini kama Papa!

Anapotajwa papa, vitu viwili huja akilini mwa wengi; maji na damu. Binafsi nilikuwa mmoja kati ya watu wanaoamini kwamba binadamu akikutana na papa basi amekwisha! 

Cha kushangaza zaidi ni kwamba hakuna uthibitisho kuwa papa huwinda binadamu. Papa humshambulia binadamu pale anapoona himaya yake imeingiliwa. Papa hudata na kuchanganyikiwa.

Papa tunayemuogopa huchukua maisha ya binadamu mmoja tu kila mwaka, lakini ng’ombe tusiyemuogopa huchukua maisha ya binadamu 22 kila mwaka.

Mwanabayolojia wa papa kutoka Marekani, marehemu Samuel Gruber anaweka wazi kwamba papa humuogopa binadamu kuliko viumbe wengine wote kwa sababu zaidi ya papa million 73 kila mwaka huuawa kwa sababu ya migogoro na wengine huvuliwa na binadamu na kutumika kama kitoweo.

Chakula kikuu cha papa ni samaki wadogo, ngisi na viumbe vingine vya majini, mara nyingi hachagui sana. Papa wakubwa hula viumbe wakubwa kama sili, pweza na taa.

Papa ana meno makali kama msumeno ambayo humsaidia kuwinda. Hunyata kisha hung’ata na kunyofoa kabisa sehemu ya mwili ya windo lake na kukiacha kiumbe kikivuja damu na baadaye kukirudia kipande kilichobaki akijua dhahiri kwamba windo lake haliwezi kujiokoa tena.

Kuna zaidi ya aina mia tano za papa na ukiingia chini ya bahari utajionea baadhi. Kuna papa wa ajabu kweli duniani, hutoamini kuna papa wanaofanana na farasi, paka, mamba hadi pundamilia lakini pia kuna hadi papa mwenye kichwa kimekaa kama nyundo.

Papa jike anaweza kubeba ujauzito uliochangiwa mbegu na papa dume zaidi ya wawili. Picha| Science News.

Papa anaweza kuwa mjamzito kwa miaka miwili na kati ya aina mia tano za papa, asilimia 40 hutaga mayai, asilimia 60 huzaa. Huzaa eneo ambalo amezaliwa yeye, na watoto wa papa huzaliwa na meno yao yote yakiwa yameota. Papa mkubwa huota hadi meno 50,000.

Sifa za kipekee

Papa jike ana uwezo kutunza mbegu za papa dume ambazo hazikutumika mara ya mwisho wanajaamiana na hivyo kuzitumia kipindi ambacho papa dume hayupo.

Mnyama huo wa majini ana uwezo mkubwa wa kunusa lakini pia ana uwezo kusikia mapigo ya moyo ya viumbe wengine. Siyo papa wote huishi baharini, wengine huishi kwenye maziwa na mito mikubwa.

Papa ana uti wa mgongo ambao hauna mifupa, uti wake hutengenezwa na misuli na gegedu. 

Gegedu ni mfumo wa mifupa ambayo haijakomaa, ni kama mifupa ya mtoto mchanga. Gegedu humsaidia papa kuogelea kwa spidi na kukunja kona za ghafla pale anapofukuzia windo lake.

Papa halali. Hutomkuta papa amelala usingizi hata siku moja, yeye hutulia tu na kupumzika kwenye mapango bila kuingia kwenye hali ya usingizi. 

Kutolala humfanya awe makini sana na mazingira yanayomzunguka, humfanya aone hatari inapokaribia na pia kuona fursa za mawindo zinapojitokeza.


TANGAZO


Papa ni wanyama wakongwe

Wanyama hao wamekuwepo duniani kwa miaka milioni 850 iliyopita na hapo zamani walikuwa wakubwa sana, kiasi cha kuwa na urefu wa futi 50 na tani 25. Hili ni kama lori lenye ‘semi trella’

Wapo pia papa wadogo wanaoweza kutosha kwenye kibakuli cha supu. Epuka kufuga papa kwenye tenki au bwawa moja na samaki wengine, atawafanya kitoweo bila kujali kwamba yeye na wenzake ni samaki wa mmiliki mmoja.

Papa ni mkimya na hatoi sauti hata kidogo. Moja kati ya viumbe ambao wamenyimwa uwezo wa kutoa sauti ni papa. Ububu wa papa unawafanya wasiwasiliane sana, kitu ambacho kinawafanya kuwa samaki wa kujitenga na hujumuika na pamoja wakati wa kuwinda. 

Tofauti na ilivyo kwa samaki wengi, papa hana magamba bali ana ngozi na ngozi yake siyo laini, ina manundu madogo madogo kama msasa.

Samaki hao huwasiliana zaidi kwa kutumia lugha ya mwili. Picha| Twincities.

Jinsi ya kuwaona papa

Utalii wa kuzama baharini na mitungi ya gesi ili kwenda kujionea maajabu ya dunia iliyopo chini ya bahari unaweza kukutanisha na mnyama huyo kinara wa maji.

Siku ukipata fursa ya kwenda Zanzibar au Mafia na ukafanikiwa kufanya utalii huu unaofahamika kama ‘scuba diving’ na ukakutana na papa huko chini majini, basi zingatia sana lugha yao ya mwili.

Ukiona umeingia kwenye himaya ya papa na ukawaona wametulia na muda mwingine wakawa wanaendelea na shughuli basi tambua kwamba hawawezi kukudhuru na muda mwingine wanaweza kukufata na kucheza na wewe.

Tahadhari! Ukiona papa amebinjua na kutunisha mgongo huku pia akiwa ametanua gego zake basi tambua kwamba hapo unapewa onyo, ondoka mapema la sivyo utakiona cha mtema kuni.

Ukishindwa kuwaona baharini, basi unaweza kuona vipande vya papa vikiuzwa sokoni, na kama hujawahi kula papa basi unaweza kujipatia kutoka soko lolote lililopo karibu nawe. 

Tukutane wiki ijayo kuangazia maisha ya mnyama mwingine. Atakuwa nani? Baki nasi.

Nasibu Mahinya ni mjasiriamali na Afisa Masoko wa soko la mtandaoni la utalii la TenTen Explore nchini Tanzania. Amekuwa mdau muhimu wa shughuli za utalii zinazofanyika ndani na nje ya Hifadhi za Taifa. Unaweza kumpata kupitia tovuti yake ya 

www.nasibumahinya.com

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW