Papa Francis kukaa hospitalini kwa siku kadhaa
- Amelazwa tangu jana Machi 29, 2023.
- Anasumbuliwa na tatizo la upumuaji na siyo Uviko-19.
- Huenda asihudhurie ibada za wiki ikiwemo Jumapili ya Matawi.
Dar es Salaam. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis aliyelazwa hospitalini tangu jana kwa tatizo la upumuaji ataendelea kupatiwa matibabu kwa siku kadhaa mpaka afya yake itakapoimarika.
Papa Francis (86) alipelekwa katika hospitali ya Gemelli ya Rome nchini Italia kwa vipimo siku ya Jumatano alasiri baada ya kupata shida ya kupumua katika siku za hivi karibuni.
Msemaji wa Vatican, Matteo Bruni katika taarifa yake iliyotolewa leo Machi 30, 2023 imeeleza kuwa papa huyo ambaye sehemu ya pafu moja iliondolewa akiwa kijana, hana Uviko-19 lakini atakaa hospitalini kwa siku kadhaa kwaa matibabu.
Kiongozi huyo anatarajiwa kuongoza maadhimisho ya Jumapili ya Matawi mwishoni mwa wiki hii, na haijajulikana kama hali yake ya kimatibabu itaathiri ratiba ya Wiki Takatifu itakayoishia Jumapili ya Pasaka ya Aprili 9.
Kulazwa kwake hospitalini kulikuwa kwa mara ya kwanza tangu Francis kuondolewa kwa sentimita 33 (inchi 13) ya utumbo wake na kukaa siku 10 katika hospitali ya Gemelli mnamo Julai 2021.
Baada ya upasuaji huo alikuwa amepona kabisa na anaweza kula chakula cha kawaida. Lakini katika mahojiano Januari 24 na shirika la habari la Associated Press, Francis alisema uvimbe kwenye ukuta wa utumbo “umerejea.”
Kabla ya kulazwa hospitalini Jumatano, papa alionekana katika hali nzuri wakati wa hadhira yake ya kawaida iliyoratibiwa, ingawa akitetemeka sana wakati akiingia na kutoka kwenye gari maalum (popemobile).
Papa ametumia kiti cha magurudumu kwa zaidi ya mwaka mmoja kutokana na mishipa iliyokauka katika goti lake la kulia, ingawa alikuwa akitembea zaidi kwa fimbo hivi karibuni.
Licha ya changamoto zinazomkabili, Papa Francis ameendelea kusafiri maeneo mbalimbali duniani.
Mapema mwaka huu alifanya ziara nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Sudan Kusini na mwezi ujao, anatarajiwa kutembelea Hungary.
Latest