Bosi Nukta Africa ashauri mbinu kuboresha uandishi wa habari Tanzania

September 19, 2024 7:52 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na matumizi sahihi ya Akili Mnemba (AI) pamoja na kuyaongezea thamani maudhui.

Dar es Salaam. Waandishi wa habari nchini Tanzania wameshauriwa kupata mafunzo ya mara kwa mara ikiwemo ya uthibitishaji wa habari ili kuboresha aina ya maudhui wanayoyazalisha jambo litakalosaidia kuyaongezea thamani maudhui yao na kukabiliana na mdororo wa ubora wa maudhui kwenye vyombo vya habari.

Nuzulack Dausen, Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Africa, Kampuni ya Teknolojia na Habari iliyopo jijini Dar es Salaam aliyekuwa akizungumza katika ufunguzi wa shindano la teknolojia lililoandaliwa na Ubalozi wa Marekani amesema maendeleo ya teknolojia hususan mitandao ya kijamii imechochea ongezeko la taarifa za uzushi jambo linalopunguza imani pamoja na kushusha thamani kwa vyombo vya habari pamoja na waandishi.

Kwa mujibu wa Dausen si waandishi wote wanafahamu michakato sahihi ya kufuata wakati wa ukusanyaji na uhakiki wa taarifa jambo linalosababisha kuandika na kusambaza taarifa isiyo ya ukweli, hivyo mafunzo yatawasaidia kufahamu michakato pamoja na nyenzo za kutumia ili kupata taarifa sahihi.

“Tunachokifanya hivi sasa ni kutoa mafunzo kwa wanahabari pamoja na wahariri kuanzia wanapokusanya taarifa, unaweza kuona taarifa inasambaa katika mtandao wa WhatsApp kabla hujaitumia kama chanzo cha habari je umejiridhisha ina ukweli kiasi gani?

…kwa hiyo tunawafundisha nyenzo za kubaini hilo kwa sababu matokeo ya kuchapisha taarifa ya uongo huwa ni mabaya,” amesema Dausen.

Matumizi sahihi ya akili mnemba (AI)

Dausen ameongeza kuwa, waandishi wa habari wanaweza kutumia akili bandia (AI) kuboresha maudhui kwa kufuata taratibu sahihi na miongozo inayotakiwa tofauti na sasa ambapo matumizi ya AI kwa kiasi kikubwa hulenga kupotosha umma.

Kutokana na walaji wa maudhui kutozingatia mbinu zilizotumika kuzalisha maudhui zaidi ya maudhui yenyewe Dausen amewashauri wanahabari kuongeza uwazi kwenye matumizi ya AI kwa kuitaarifu hadhira husika iwapo maudhui hayo yametayarishwa na akili bandia.

“Unaweza kusema picha hii imetengenezwa na AI na imetumika kwa ajili ya kujenga na kuongeza muktadha wa habari na si halisia kama inavyoweza kutafsiriwa, kwa kufanya hivyo tunaweza kuongeza ubora wa taarifa,” ameongeza Dausen.

Kauli ya bosi huyo wa Nukta inakuja wakati ambao matumizi ya AI nchini Tanzania yameanza kushika kasi katika sekta ya habari ambapo baadhi huitumia kuandika habari, kutengeneza picha, video pamoja na nyimbo au kusoma muhtasari ya taarifa (script).

Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Afrika, Nuzulack Dausen akifundisha wanafunzi wa uandishi wa habari wa UDSM-SJMC jinsi ya kutumia data kuongeza ubora wa habari. Picha |Mercy Masinga

Nukta Africa ni miongoni mwa taasisi inayotumia AI kwenye uendeshaji wa shughuli mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa picha zinazotumika kwenye habari zinazochapishwa.

Hata hivyo, baadhi ya watu hutumia AI kutengeneza taarifa potofu za masuala mbalimbali kama afya, uchaguzi au kiuchumi  jambo linalosababisha uwepo wa taharuki kwenye jamii ambapo mafunzo ya namna ya kutambua maudhui yaliyotengenezwa kwa akili mnemba yanayotolewa na Nukta Afrika yanaweza kusaidia kukabiliana na changamoto hiyo.

Kuyaongezea thamani maudhui

Aidha, Dausen amesema kutokana na uwepo wa mitandao ya kijamii taarifa nyingi zinawafikia walaji kwa wakati jambo linalosababisha wanahabari kurudia kitu kile kile na kusababisha thamani yake kushuka.

Ili kuondokana na changamoto hiyo Dausen ameshauri ni vyema mwandishi kujibu swali la “ hii maana yake nini? Ambalo majibu yake yanaweza kuwa kitu kipya kwa walaji wa maudhui hayo na hivyo unakuwa umeyaongezea thamani.

“Hapo sasa unaweza kuzungumza na wachambuzi wakakuambia je hiyo ni fursa au ni changamoto, unaweza kuhusisha matumizi ya takwimu hiyo itamsaidia mlaji wa maudhui hayo kufanya maamuzi sahihi,”  amesisitiza bosi huyo ambaye pia ni mkufunzi.

Kwa zaidi ya miaka mitano Nukta imekuwa ikitoa mafunzo kwa wanahabari na wahariri katika uandishi wa habari za takwimu, uandishi wa habari za kidijitali, uandishi wa habari za bionuai pamoja na uthibitishaji wa habari.

Kwa mujibu wa Dausen kwa mwaka 2024, Nukta imepanga kuwafundisha wahariri na wanahabari 1,000.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks