Ni wakati gani unatakiwa kupata ‘booster’ ya Uviko-19?

February 8, 2023 10:46 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kupata chanjo kwa maelekezo ya daktari.
  • Booster huongeza ufanisi wa chanjo mwilini.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ya Tanzania ikijiandaa kuzindua ‘Booster’ ya dozi ya Uviko-19 ili kuwaongezea kinga watu waliopata chanjo ya ugonjwa huo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa utaratibu wa namna afua hiyo inapaswa kutolewa. 

“Booster” ni dozi ya ziada au dozi za chanjo ambazo hutolewa kwa mtu ambaye tayari amepata chanjo ya Uviko-19 na ulinzi wake umeanza kupungua. Dozi hiyo husaidia kumuongezea kingamwili dhidi ya maambukizi mapya ya ugonjwa huo, hii ni kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC).

 

Ni mara ngapi upate ‘booster’?

Mkurugenzi wa Kinga na Chanjo wa WHO, Dk Kate O’Brien amesema ni muhimu kufuata miongozo iliyowekwa na nchi husika ili kufanikisha suala hilo.

“Kila nchi ina sera zake za namna wanavyoendesha zoezi la chanjo,” amesema Dk O’Brien na kubainisha kuwa booster hutolewa kwa awamu kulingana na mahitaji ya watu.

Mtaalam huyo amesema dozi hiyo anapewa mtu ambaye tayari amepata chanjo ya Uviko-19 kuimarisha kinga yake na atapatiwa kwa awamu kulingana na hali yake. 

Dk O’Brien anasema mtu akipata booster ya kwanza inashauriwa akae miezi sita kabla hajapata ya pili hasa kwa wale walio katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa huo.

Hata hivyo, muda wa kupata booster ya kwanza na ya pili hutegemeana na aina ya chanjo aliyopata mtu. 

WHO inapendekeza kuwa afua hiyo itolewe kwa mtu baada ya kupata ushauri wa daktari ambao utatokana na tathmini ya afya yake.

Booster ikitumika vizuri ni afua muhimu kukabiliana na ugonjwa wa Uviko-19. Picha | Los Angeles Times.

Kwa nini ‘booster’?

Wanasayansi wanaeleza kuwa ufanisi wa chanjo ndani ya mwili wa binadamu hupungua kwa muda fulani, hivyo kuna haja ya kuiongezea nguvu ili iendelee kutoa kinga kwa mtu husika. Awali booster (viongezeo vya mapema) iliitwa “monovalent” kwa sababu iliundwa kumlinda mtu dhidi ya virusi vya asili vinavyosababisha Uviko-19. 

Pia hutoa ulinzi fulani dhidi ya virusi vya ugonjwa huo aina ya Omicron.Kwa sasa booster inaitwa “bivalent” kwa sababu inatoa ulinzi dhidi ya virusi vya asili vinavyosababisha Uviko-19 na lahaja za Omicron BA.4 na BA.5.


Soma zaidi:


Utegemee nini mara baada ya kupata ‘booster’

Mara baada ya kupata afua hiyo unaweza kupata madhara hafifu ya kiafya ikiwemo homa, kuumwa kichwa, uchovu na maumivu sehemu uliyochomwa sindano. 

Jinsi ya kupunguza madhara hayo

Licha ya kuwa madhara hayo hayadumu kwa muda mrefu lakini unaweza kutumia njia hizi kupunguza maumivu:

  • Weka kitambaa kisafi kilicho na maji ya baridi eneo ulilochomwa sindano.
  • Hakikisha unachezesha mkono wako.
  • Ikiwezekana, pata mapumziko ya kutosha
  • Kunywa maji ya kutosha
  • Vaa nguo zisizobana mwili
  • Ongea na daktari wako kama anaweza kukupatia dawa za kutuliza maumivu 
Enable Notifications OK No thanks