Ni uzushi: Huwezi kupata maambukizi ya Corona kwa kuchangia damu
- Unaruhusiwa kuchangia damu hata katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa Corona.
- Huwezi kupata maambukizi ya ugonjwa Corona kwa kuchangia damu.
Dar es Salaam. Kama wewe ni miongoni mwa watu ambao uliyekutana na habari zinazokataza watu kuchangia damu kwa kuogopa kuambukizwa ugonjwa wa virusi vya Corona, basi fahamu kuwa umedanganywa.
Wazira ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeeleza kuwa hakuna uhusiano kati ya kujitolea damu na kupata virusi vya COVID-19.
“Hapana, tunaruhusiwa kujitolea damu hata kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa Corona. Huwezi kupata maambukizi ya ugonjwa wa Corona kwa kuchangia damu,” kimeeleza kituo cha taarifa na maarifa cha wizara hiyo.
Zoezi la uchangiaji damu ni salama na linaendeshwa kwa kufuata misingi na kanuni za afya.
“Unapojitolea damu unasaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji. ahitaji ya damu katika hospitali zetu, kwa makundi ya watu kama vile kina mama wajawazito, kina mama wanaojifungua, watoto, majeruhi wa ajali na wagonjwa wanaohitaji huduma ya upasuaji,” imesema Wizara hiyo.
Zinazohusiana
Nalo Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema magonjwa yanayoambukizwa kwa mfumo wa upumuaji, hayawezi kuambukizwa kwa njia ya damu na suala la kujitolea damu kuambukiza COVID-19 ni nadharia ambazo hazijathibitishwa.
“Hatari ya Covid-19 kuambukizwa kwa kuchangia damu kwa sasa ni nadharia na zaidi ni ndogo. Lakini kwa uzoefu wa magonjwa mengine ya mlipuko yanayohusiana na virusi vya Corona, kutakuwa na changamoto katika usambazaji wa damu kunakosababishwa na kupungua kwa uchangiaji damu,” imeeleza WHO katika mwongozo wake wa COVID-19.