Ni uzushi: CAF haijapongeza kiwango cha Simba Twitter

August 7, 2019 2:23 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Mara ya mwisho CAF kutwiti kwa akaunti hiyo inayodaiwa kuisifia Simba ni Agosti 3, 2019.
  • Twiti hiyo ni ya kutengeneza ikionekana kuwa na madhumuni ya kuwanyong’onyesha Yanga.

Dar es Salaam. Hapana shaka kuwa mchuano wa mashabiki wa timu za soka za Tanzania Simba na Yanga umeanza kuzalisha habari potofu zinaonekana kupamba upande mmoja ama mwingine bila kuwa na ukweli.

Leo Agosti 7, 2019 kuna picha inayosambaa kwa kasi mitandaoni yakiwemo makundi ya Whatsapp ikidai kuwa Shirikisho la Soka Africa (CAF) limeisifia Simba kwa kiwango chake kizuri jambo ambalo ni uzushi.

Picha hiyo ambayo ni twiti inayodaiwa kuwa ni twiti ya CAF (@CAF_Online) imeandikwa kwa Kiingereza “big up to @SimbaSCTanzania next levels…now your going to be a giant of Africa congratz boys” (Hongereni @SimbaSCTanzania kwa kiwango…sasa mnaenda kuwa miamba ya Africa, hongereni vijana).

Picha inayosambaa kwenye makundi ya mitandao ya kijamii inayoonyesha CAF kuipongeza simba. Picha|Mtandao.

Simba ilivaana jana na timu ya soka ya nchini Zambia ya Power Dynamos katika maadhimisho ya kilele cha Siku ya Simba katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo timu mwenyeji iliibuka na ushindi wa mabao matatu kwa moja.

Uchunguzi wa Nukta (www.nukta.co.tz) umebaini kuwa twiti hiyo inadaiwa kuwa ilichapishwa saa 3:47 usiku Agosti 6, 2019 ni uzushi au kwa lugha za vijana wa mtaani ni famba.

Hakuna mahali popote ambapo @CAF_Online imetwiti kuhusu Simba mwezi huu wala uliopita. Mara ya mwisho akaunti hiyo ya CAF ilitwiti Julai 30, 2019 ikiwashukuru wote waliofanikisha mashindano ya kombe la Africa mwaka 2019.

Mbali na twiti hiyo ya mwisho, jambo la mwisho kufanywa na akaunti hiyo ya Twitter ya CAF ni kuritwiti twiti za Katibu Mkuu wa Fifa, Fatma Samoura Agosti 3, 2019. 

Picha hiyo ni uzushi na imetengenezwa huenda kwa madhumuni ya kuwanyong’onyesha mashabiki wa Yanga kutokana na mtengenezaji huyo kuweka majibu ya Yanga katika twiti ikilalamika kuonewa na CAF.

Maeneo yanayoleta mashaka

Kiingereza kibovu

Ni dhahiri kuwa twiti hiyo imejumuisha Kiingereza kilichoandikwa bila kufuata sarufi jambo ambalo haliwezi kufanya na CAF. Uchunguzi wa twiti zote za CAF unaonyesha kuwa wakati wote wanaandika kwa ustadi na kufuata taratibu za lugha kwa kila kitu wanachokifanya.

Hakuna mahali Yanga imejibu

Katika matumizi ya mtandao wa Twitter ni rahisi kubaini iwapo mtu alijibu katika twiti iwapo utafuatilia twiti ya kwanza au ya akaunti iliyojibu. Katika twiti hiyo inayosifia Simba hakuna eneo lolote unapoona Yanga ilihusika kujibu.   

Enable Notifications OK No thanks