Nchi 10 zenye wakimbizi wengi Duniani
- Nchi hizo ni pamoja na Syria, Congo DRC,Columbia, Afghanstan na Yemen.
- Zinachaangia karibu nusu ya wakimbizi wote duniani.
Dar es Salaam. Wakati ukifurahia kuanza mwaka ukiwa karibu na familia au watu uwapendao kuna mamilioni ya watu ambao wanalazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo migogoro ya kisiasa.
Kwa mujibu wa Kituo cha Kimataifa Kinachofuatilia Watu Wanaoyakimbia Makazi Yao (IDMC) mpaka kufikia mwishoni wa mwaka 2021 kulikuwa na jumla ya wakimbizi milioni 59.1 waliyoyakimbia makazi yao duniani kote.
IDMC inasema chanzo kikuu cha kuongezeka kwa wakimbizi hao ni migogoro na uonevu pamoja na majanga ya kiasili ikiwemo ukame, njaa, mafuriko na vimbunga.
Migogoro pekee imechangia asilimia 90 ya watu wanaohama makazi yao ambayo ni sawa na watu milioni 53.2 huku majanga yakichangia asilimia 10 tu ya wakimbizi wote wanaokimbia makazi yao sawa na milioni 5.9.