NBS kutoa taarifa ya mfumuko wa bei za bidhaa, huduma Novemba 11
- Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) leo imeahirisha kutangaza mwenendo wa mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka unaoishia Oktoba 2019 kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake.
- Badala yake itatangaza jumatatu ya Novemba 11.
Dar es Salaam. Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) leo imeahirisha kutangaza mwenendo wa mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka unaoishia Oktoba 2019 kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake, badala yake itatangaza jumatatu ya Novemba 11.
Kawaida, NBS hutoa takwimu za mfumuko wa bei tarehe nane ya kila mwezi na imekuwa ikifanya hivyo kwa muda mrefu sasa.
Taarifa iliyotolewa leo (Novemba 8, 2019) na Mtakwimu Mkuu wa NBS, Albina Chuwa imeeleza kuwa kwa mwezi huu, takwimu za mfumuko wa bei hazitotolewa leo na badala yake zitatolewa Jumatatu ya Novemba 11, 2019.
“NBS inapenda kutaarifu wateja wake kuwa; toleo la taarifa ya mfumuko wa bei kwa mwezi Oktoba, 2019 zilizotakiwa kutolewa Novemba 8, 2019 zimeahirishwa hadi jumatatu ya Novemba 11, 2019 kuanzia saa 7:00 mchana,” ameeleza Chuwa katika taarifa hiyo.
Zinazohusiana
Kwa mwezi uliopita wa Oktoba, taarifa hiyo ilitolewa kama ilivyo kawaida huku ikionyesha kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini ulishuka hadi kufikia asilimia 3.4 kwa mwaka ulioishia Septemba 2019.
Kilichochangia hayo yote ni kupungua kwa bei za bidhaa zisizo za vyakula zikiwemo mafuta ya taa, petroli na majiko ya gesi.