NBS: Ajira zimeongezeka Tanzania
- Imesema idadi ya watu walio na ajira Tanzania imeongezeka kutoka milioni 20 mwaka 2014 hadi milioni 22 mwaka 2018.
- Imesema ajira 137,054, sawa na asilimia 25 ya ajira zote nchini, zilizozalishwa na sekta binafsi zimepungua kutoka ajira 239,017 mwaka 2016/17 hadi ajira 137,054.
Dar es Salaam. Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema idadi ya watu walio na ajira Tanzania imeongezeka kutoka milioni 20 mwaka 2014 hadi milioni 22 mwaka 2018.
Katika taarifa ya NBS iliyotolewa leo (Agosti 14, 2019), ambayo ilikuwa ikitoa ufafanuzi kuhusu kusambaa kwa habari kuwa ajira za Serikali zimepungua na kueleza kuwa ajira zimekuwa zikiongezeka kila mwaka.
Ikielezea ripoti yake ya Tanzania in Figure 2018 iliyotolewa Juni mwaka huu, NB imeeleza kuwa mwaka 2017/18 kulikuwa na ajira 552,063 zilizozalishwa nchini ikilinganishwa na ajira 453,466 kwa mwaka 2016/17.
Kiasi cha ajira kwa mujibu wa NBS ni sawa na ongezeko la ajira 98,597 sawa na asilimia 21.7 kati ya mwaka 2016/17 na mwaka 2017/18.
“Kati ya ajira 552,063 zilizozalishwa nchini mwaka 2017/18, ajira 415,009 sawa na asilimia 75 zilikuwa ni ajira kutoka Serikalini; ajira hizi zinajumuisha ajira 18,000 kutoka Serikali Kuu na ajira 397,009 kutoka katika miradi ya maendeleo kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17 hadi 2020/21,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Soma zaidi: Serikali yapendekeza mabadiliko makali Sheria ya Takwimu
Aidha, NBS imesema hali hiyo inatokana na ukweli kuwa, wananchi wengi huajiriwa kwenye miradi ya kimkakati ya maendeleo inayoendelea hapa nchini ambapo Serikali imejikita kwa dhati kuitekeleza kwa ajili ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na kupunguza umaskini.
Katika hatua nyingine, NBS imeeleza kuwa ajira zilizozalishwa na sekta binafsi, zimepungua kutoka ajira 239,017 mwaka 2016/17 hadi ajira 137,054. Ajira hizo 137,054 zilizozalishwa na sekta binafsi ni sawa na asilimia 25 ya ajira zote nchini zilizozalishwa mwaka 2017/18.
Imebainisha kuwa takwimu zilizowekwa kwenye ripoti ya Tanzania in Figure 2018 zinazotokana na taarifa za kiutawala (administrative records) ambazo zinasaidia kupata takwimu za ajira ambazo hazikusanywi kwenye tafiti za kawaida.
Takwimu hizo hutumika pia kama kigezo cha kufanya maoteo ya hali ya ajira (proxy indicators) katika vipindi ambavyo hakuna tafiti zilizofanyika ili kutoa hali ya soko la ajira katika vipindi vifupi vifupi, NBS imeeleza.
Latest
