Namna umemejua, tungamo taka vinavyoweza kuboresha maisha ya wafugaji Tanzania
- Inasaidia kuongeza thamani ya maziwa, kipato cha kaya na mnyororo wa thamani wa bidhaa hiyo.
- Wafugaji washauriwa kupata ushauri wa kitaalamu kabla ya kutumia ili kuepuka gharama zisizo za lazima.
- Inafaa zaidi wafugaji wanaofuga mifugo sehemu moja kuliko wale wanaohama hama.
Dar es Salaam. Ripoti ya matumizi ya nishati safi inaeleza kuwa ikiwa wafugaji wa Tanzania na Kenya watawezeshwa kutumia vifaa vya kuhifadhia maziwa vinavyoendeshwa na nishati jadidifu watapunguza upotevu wa bidhaa hiyo na kuongeza kipato katika kaya zao.
Ripoti hiyo iitwayo Gharama na Faida za Teknolojia ya Nishati safi katika Maziwa, Mboga na Mnyororo wa Thamani wa Mchele ya mwaka 2018 iliyotolewa na Shirika la Chakula Dunia (FAO), inaeleza kuwa maziwa yanayozalishwa na wakulima vijijini, ambao hawajapitiwa na gridi ya Taifa ya umeme, yanapotea na kuharibika kabla ya kufika sokoni.
Sababu kubwa ni kuwa wafugaji hao hawana teknolojia rahisi ya kuwawezesha kuhifadhi bidhaa hiyo muhimu kwa afya ya binadamu na uzalishaji viwandani.
“Maziwa yanaharibika haraka kama hayajapozwa (chilled), bado maeneo mengi ya vijijini hayana vifaa vya kutosha vya kuhifadhia maziwa,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Hata hivyo, ripoti hiyo ambayo pia inaeleza faida za kiuchumi za kutumia mifumo ya kuhifadhia maziwa, imebainisha kuwa matumizi ya teknolojia ya nishati jadidifu katika uhifadhi, yanaweza kusaidia kudhibiti upotevu wa maziwa bila kutumia hewa ukaa (GHG emissions) katika uhifadhi.
Nishati jadidifu ambayo inaweza kuleta ufanisi ni pamoja na umemejua na tungamo taka (biogas) hasa inayotaka na kinyesi cha wanyama, kwa mujibu wa ripoti hiyo.
Nishati ya tungamo taka hupatikana kutokana mabaki ya bidhaa mbalimbali ikiwemo kinyesi cha wanyama ambacho huifadhi kwenye shimo maalum na kisha nishati hiyo hutengenezwa.
Kwa Kenya na Tanzania, ili kiunga cha kuhifadhia maziwa nyumbani kinachoendeshwa na nguvu ya tungamo taka kitengenezwe, unahitajika uwekezaji wa Dola za Marekani 1,600 (Sh3.6 milioni).
Kama kitaweza kufanya kazi ipasavyo kinaweza kutengeneza faida za moja kwa moja za binafsi ikiwemo upatikanaji wa maziwa bora na mauzo kuongezeka kwa wakulima.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa wafugaji wa nchi hizo mbili wanaweza kupata dola za Marekani za ziada kati ya 1.96 na 2.17 (kati ya Sh4,511 na Sh4,995) kwa siku moja kwa kuvuna na kuhifadhi vizuri maziwa nyakati za jioni.
Wakati huo huo, kwa kutumia kiunga cha maziwa cha tungamo taka hutengeneza thamani ya ziada ya dola za Marekani 531 (Sh1.2 milioni) kwa Kenya na dola 128 (Takriban Sh295,000) kwa Tanzania katika mnyororo wa thamani wa bidhaa hiyo.
Ili mfugaji afaidike na nishati hiyo, inahitajika kuwa na uhakika wa kupata kinyesi cha wanyama, ambapo wafugaji wanaofugia mifugo eneo (zero grazing) wanajiweka katika nafasi nzuri ya kufaidika na teknolojia hiyo kuliko wale wanaohama hama. Picha|Mtandao.
Teknolojia hiyo inasaidia kuongeza ajira na kuboresha afya za wafugaji kwa kupunguza hewa chafu ya ndani inayotokana na matumizi ya kuni na mkaa.
Kwa kupunguza upotevu wa maziwa, teknolojia hiyo ina uwezo wa kuokoa takriban lita milioni moja na maji lita milioni tatu kwa mwaka.
Kwa mujibu wa Kitabu Cha Hali ya Uchumi wa Taifa mwaka 2018 kilichotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), uzalishaji wa maziwa nchini uliongezeka hadi kufikia lita bilioni 2.4 ikilinganishwa na lita bilioni 2.09 mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 15.
Licha ya Tanzania kuzalisha maziwa mengi kila mwaka kutokana na mifugo iliyopo, bado wafugaji hawajafaidika ipasavyo kutokana na kutumia teknolojia duni katika uzalishaji wa maziwa.
Mtaalam wa matumizi endelevu ya nishati (PUE), Fredrick Mushi kutoka taasisi ya Elico Foundation anasema nishati ya jotoardhi inaweza kutumiwa na wafugaji kupata nishati ya kupikia na mwanga.
“Faida zake ni kubwa sana, kuendeshea hizi chillers (viunga vya kuhifadhia maziwa) kuwa na uwezo wa kuongeza thamani ya maziwa yao pamoja na kupata mbolea kwa ajili ya mashamba au bustani zao. Mbolea hii pia inaweza ikauzwa na kuingiza kipato kama mfugaji husika hajiusishi na kilimo,” anasema Mushi.
Soma zaidi:
- Maoni: Tunaweza kuwapatia furaha watanzania wengi zaidi kwa nishati jadidifu
- Wadau wahimiza uwekezaji, uendelezaji nishati jadidifu Tanzania
- Namna umeme vijijini unavyoweza kutumika kuchochea maendeleo
Wafugaji wanaoweza kufaidika na nishati hiyo
Ili mfugaji afaidike na nishati hiyo, inahitajika kuwa na uhakika wa kupata kinyesi cha wanyama, ambapo wafugaji wanaofugia mifugo eneo (zero grazing) wanajiweka katika nafasi nzuri ya kufaidika na teknolojia hiyo kuliko wale wanaohama hama.
Hata hivyo, Mushi anasema gharama za kufunga mitambo ya kuhifadhi maziwa ziko juu hasa kwa sababu kinahitajika kifaa cha kubadili gesi ya kinyesi kuwa umeme.
Gharama hizo pia zinaweza kupungua ikiwa wafugaji watawezeshwa kutumia nishati ya umemejua hasa katika maeneo yenye gridi ndogo ya umeme (min-grid areas) ambayo inaweza kuendesha viunga vya kuhifadhia maziwa.
“Changamoto kubwa ni gharama za awali za uwekezaji kuweka hiyo solar system (mfumo wa umemejua) inayoweza kuendesha kiunga cha kuhifadhia maziwa. Japo kwa mfugaji mmoja mmoja (hususani wadogo) inaweza kuwa changamoto wakifanya kama kikundi itakuwa affordable (watamudu),” anasema Mushi.
Mtaalamu huyo anaeleza wafugaji watakiwa waelimishwe na kupata utaalamu wa kuwasaidia kujua mahitaji ya kiunga na mfumo wa umeme unaohitajika ili viende sambamba na kuleta tija.
Latest
