Namna mabadiliko ya teknolojia ‘yalivyozipoteza’ simu za mezani Tanzania

November 1, 2018 6:54 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Licha ya watumiaji wa simu za mezani kupungua bado zitaendelea kuwepo kwa muda mrefu ujao kwasababu ya usalama na umuhimu wake katika jamii. 
  •  Simu hizo ni kiunganishi cha familia, taasisi na mashirika mbalimbali.
  • Zinaendelea kuboreshwa kukidhi mahitaji na mabadiliko ya teknolojia ya mawasiliano.

Dar es Salaam. Kwa sehemu kubwa ya Watanzania kwa sasa simu janja (smartphones) ndiyo habari ya mjini. Mabadiliko ya teknolojia ya mawasiliano yanayochochewa zaidi na matumizi ya intaneti yamezifanya simu za mkononi kuwa sehemu muhimu kwa maisha ya binadamu na ndiyo njia kubwa ya mawasiliano kwa sasa.

Miaka 20 iliyopita ilikuwa ni bahati nasibu kumkuta mtanzania wa kawaida akimiliki simu ya mkononi hata ile ya kawaida maarufu kama ‘kitochi’ kwa wakati huo habari ya mjini ilikuwa ni simu za mezani. 

Nyakati hizo za miaka ya 1990 watu wengi hawakutegemea kama dunia ingepitia mabadiliko makubwa ya jinsi watu wanavyowasiliana kwa urahisi na haraka wakiwa popote ulimwenguni. 

Na kama wewe ulikuwa na simu ya mkononi mwaka 2007 basi ulikuwa miongoni mwa watu wawili kwa kila 100 waliokuwa wanatumia simu nchini. 

Ripoti ya mawasiliano ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya Juni 2007 inaonyesha kuwa mwaka 1995 Tanzania ilikuwa na watumiaji wa simu za mkononi  2,198 tu ukilinganisha nawatumiaji 88,000 wa simu za mezani.

Hiyo ni sawa na kusema watumiaji wa simu za mkononi walikuwa ni asilimia ya 2.43 ya watumiaji wote wa simu. Kwa kipindi hicho cha mwaka 1995, watumiaji wa simu za mezani nchini walikuwa mara 40 ya wale wanaotumia simu za mkononi. 

Kutokana na umuhimu wa mawasiliano watu wengi walijitokeza kuchangamkia huduma ya simu za mezani ambayo ilikuwa inatolewa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) lakini ongezeko lake halikuwa kubwa kutokana na kuanza kuibuka kwa teknolojia ya simu za mkononi ambayo ilijipatia umaarufu miongoni mwa watu wengi.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa miaka 12 iliyofuata hadi kufikia Juni 2007 watumiaji wa simu za mezani walifikia 169,135 ikiwa ni ongezeko la asilimia 6 kila mwaka. Lakini katika kipindi hicho idadi ya watumiaji wa simu za mkononi ilikuwa inaongezeka kwa kasi na ikifikia watu milioni 6.8. 

“Simu za mkononi zinaongoza soko kwa kuwa na watumiaji wanaofikia asilimia 98 ukilinganisha zimu za mezani (2%),” inaeleza ripoti ya mawasiliano katika kipindi cha mwaka 2007. 

Hata hivyo, bado ongezeko hilo la watumiaji wa simu lilikuwa dogo kwasababu idadi kubwa ya watu walikuwa hawajaunganishwa na mifumo ya kisasa ya mawasiliano. Walitegemea zaidi barua za kuandikwa kwa mkono kama njia rahisi ya kuwasiliana na wapendwa wao au ofisi. 


Mambo yamebadilika

Kutokea hapo upepo ulibadilika idadi ya watumiaji wa simu za mezani ikaanza kuporomoka huku simu za mkononi zikaanza kupata muitikio mkubwa kwa watanzania hasa baada ya bei zake kupungua mwaka hadi mwaka ambapo katika kipindi hiki ni mara chache kumuona mtu akitumia simu ya mezani nyumbani labda kwa shughuli za kiofisi pekee.

Mambo yamebadilika na maisha ya teknolojia yanaenda kasi. Takwimu hizo za TCRA zinaonyesha mpaka mwishoni mwa mwaka 2017 ni asilimia 0.31 tu ya watumiaji wa simu wapatao milioni 40 wanatumia simu za mezani. Hii ina maana kuwa katika kila watumiaji wa simu 10,000, ni watu 31 tu wanatumia simu za mezani.

Tafsiri yake ni kuwa watu wanakimbilia mifumo rahisi ya mawasiliano ambayo inapatikana mahali popote ukilinganisha na simu za mezani ambazo hazihamishiki kirahisi.


Huu ndiyo mwisho wa simu za mezani?

Kama unafikiri simu za mezani hazihitajiki tena basi utakuwa unajidanganya, bado zinatumika na watu wengi licha ya mabadiliko makubwa ya teknolojia ya mawasiliano yanayojitokeza. 

Kwa mujibu wa shirika la Du County Telecom la nchini Marekani linaeleza kuwa umuhimu wa kuendelea kutumia simu za mezani unatokana na ukweli kuwa ni rahisi kutumia kwa sababu zinaambatana na gharama ndogo za kupiga na kupokea simu ndani na nje ya nchi. 

Pia zinamuhakikishia usalama na usiri mtumiaji kwa sababu ni vigumu kuingiliwa na wahalifu wa mtandaoni kama ilivyo kwa simu za mkononi ambazo zimeunganishwa na mtandao wa intaneti. 

Kupotea kwa mtandao wakati ukitumia simu ya mkononi nayo ni sababu nyingine ya ofisi au familia kuwa na simu ya mezani hasa katika maeneo ya vijijini ambako kuna changamoto ya mawasiliano. Simu ya mezani inakuhakikishia mawasiliano yako na umpendaye au wateja wako bila kupoteza ubora au kuingiliwa na sauti za mawimbi ya radio.


Zinazohusiana:


Wataalam wa teknolojia ya mawasiliano hapa nchini wanabainisha kuwa kupitia simu ya mezani, mpigaji anaweza kutambua kwa haraka eneo alipo mtu anayezungumza naye kwasababu kila namba ya simu inayotolewa huambatana eneo husika tofauti na simu za mkononi. 

“Simu ya mezani ni identity (kitambulishi) ya biashara na ofisi,” anasema Clemence Kyara, Mhandisi wa kompyuta kutoka kampuni ya Code for Africa.  

Kyara anabainisha kuwa simu ya mezani inaweza kuwa njia sahihi ya kutunza nidhamu mahali pa kazi hasa katika kuhakikisha wafanyakazi wanakuwepo ofisini katika muda waliopangiwa kukamilisha majukumu yao. 

Simu hizo pia ni kiunganishi muhimu cha mahusiano ya familia wakati huu ambao ndoa zinapitia misukosuko ya kimaadili na kupungua kwa uaminifu kunakosababishwa na utandawazi hasa matumizi ya simu za mkononi. 

“Simu za mezani ni za muhimu sana, ni connection (kiunganishi) pekee ya kuwasiliana, inahudumia watu kwenye familia ambapo ni simu pekee inayokuunganisha na walioko nyumbani moja kwa moja,” anasema Nicodemus Mushi, Afisa Mahusiano na Mawasiliano kutoka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

Mushi anasema simu za mezani ni muhimu kwa taasisi na mashirika ya umma ambayo yanatakiwa yawe sehemu moja kwa ajili ya kutoa huduma pale mtu anapotaka kupata taarifa fulani.

“Watumiaji wakubwa wa simu za mezani ni taasisi kama vile hospitali, shule, polisi, vituo vya afya ambazo zinazoa huduma kwa jamii na familia zenye uelewa kuhusu umuhimu wa mawasiliano ya simu za mezani,” anasema Mushi.

Simu ya mezani inamuhakikishia salama na usiri mtumiaji kwa sababu ni vigumu kuingiliwa na wahalifu wa mtandaoni. Picha| ATD.

Licha ya kuonekana zimepitwa na wakati, simu za mezani zitaendelea kuwepo kwa muda mrefu ujao ikizingatiwa kuwa zimefanyiwa maboresho makubwa ikiwemo kutumia laini za mitandao yote, betri ya kuchaji, ujumbe mfupi wa maneno (sms) na kitabu cha orodha ya majina ya watu unaowasiliana nao na baadhi zina uwezo wa kuunganishwa na intaneti.  

Maboresho haya yanalenga kuzifanya simu za mezani kuendelea kuwa kifaa cha kuaminika kuwaunganisha watu katika nyanja mbalimbali za maendeleo. 

“Tunafanya mabadiliko makubwa, sasa badala ya kutumia waya ambazo muda mwingine zinaharibika au kukatwa sasa tumekuja na simu zinazotumia huduma za ‘wireless’,” anasema Mushi. 

Hata hivyo watoa huduma ya simu za mezani bado wana kazi kubwa ya kuhimili ushindani wa kampuni za simu za mkononi ambazo zimetawala soko la mawasiliano nchini. 

“Tuna kampeni ya kutangaza huduma mbalimbali tunazofanya nchi nzima ili wananchi waweze kujua umuhimu wa simu za mezani,” anasisitiza Mushi.

(Nyongeza na Zahara Tunda)

Enable Notifications OK No thanks