Namna habari za mtandaoni zinavyoweza kubadili maisha
Dar es Salaam. Ndani ya miaka mitano ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la habari za mtandaoni kutokana na kukua kwa teknolojia ya dijitali. Kiwango hicho cha habari za mtandaoni kinatarajiwa kukua zaidi miaka ijayo kutokana na kuendelea kwa ugunduzi wa njia bora za ukusanyaji, uchakataji na usambazi wa habari.
Kasi hii ya mabadiliko ya teknolojia ya dijitali siyo tu imebadilisha namna watu ambavyo hupata habari au taarifa bali hata muda na vifaa wanavyotumia kupata habari husika.
Miaka 10 tu iliyopita redio na televisheni ndiyo angalau vilikuwa vyombo vya habari vinavyotegemewa kwa habari za haraka.
Kama umekosa habari katika redio na televisheni ulikuwa huna budi kusubiri magazeti kesho yake ambayo kwa sehemu kubwa yalikuwa mkombozi wa wengi japo yalikuwa hayafiki sehemu kubwa nchini.
Lakini sasa kila kitu kimebadilika. Ujio wa mtandao hususan blogu, tovuti na mitandao ya kijamii kama Facebook na Twitter ulifanya watu wapate mbadala wa habari badala kusubiri kwenye redio, televisheni na magazeti.
Kwa sasa msomaji anaweza kuwa “mwanahabari” kwa kuchukua picha au video na kuandika maneno machache kuelezea kilichotokea na kuchapisha Facebook au Twitter na wakati mwingine kufanya kitu hicho kuwa mada ya kitaifa. Matukio mengi ya ajali nchini na hata ziara za kwanza za Rais John Magufuli nyingine zilianza kuwekwa mtandaoni kwanza na kisha baadaye katika vyombo vya habari.
Kuna fursa zaidi
Watu wengi wanatumia simu sasa kupata habari kuliko kipindi cha nyuma shukran kwa ujio wa simu janja (Smartphone) za bei rahisi zenye uwezo wa intaneti.
Hadi Desemba mwaka jana, takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha watumiaji wa intaneti walilkuwa milioni 19.86 sawa na asilimia 40 ya upatikanaji wa huduma hizo nchini, takriban mara nne ya watumiaji milioni 5.31 wa mwaka 2011. Kati ya watumiaji hao wa intaneti takriban milioni 20, TCRA inaeleza kuwa tisa kwa kila 10 wanatumia intaneti inayohamishika (Mobile internet) ambayo hutumiwa zaidi na vifaa kama simu na tablet.
Takwimu hizo ambazo huenda mwaka huu zikawa zimeongezeka zaidi, zinaonyesha namna upatikanaji wa habari kwa njia za dijitali utakavyokuwa unaongezeka kwa kasi siku zijazo iwapo mwenendo utaendelea kukua.
Pamoja na kuwa mabadiliko ya teknolojia yameanza kuathiri biashara ya televisheni na magazeti, tunaamini uwekezaji katika habari za dijitali unahitajika kwa sasa kuliko wakati wote iwapo lengo la kusaidia wananchi kukua kiuchumi na kijamii litabaki kipaumbele.
Kama ambavyo teknolojia ya magazeti na televisheni zilivyoleta fursa zinazoonekana sasa dijitali nayo itaanzisha mianya yake ya kupatia fedha na tunaamini wananchi wengi Tanzania watafikia hatua ya kununua habari mtandaoni zinazosaidia kubadilisha maisha yao.
Habari za dijitali zilizo za kweli zinapunguza mwanya katika ya wanaopata na wasiozipata habari hizo na kuwapatia taarifa za fursa nyingi za kiuchumi kwa haraka zinazowasaidia kufanya maamuzi.
Mabadiliko ya soko mara nyingi huwa ni ya haraka hususan katika ulimwengu wa utandawazi hivyo habari za dijitali zinaweza kuwafanya wananchi kuchukua hatua stahiki kukabiliana au kutumia fursa zinazokuwa zimejitokeza.
Vita dhidi ya habari za uzushi
Mbali na kutoa habari zenye fursa lukuki, habari za dijitali zimekuwa zikikumbwa na wimbi la taarifa za uzushi maarufu kwa Kiingereza kama ‘Fake News”.
Wimbi hili la habari za kutungwa limefanya baadhi ya nchi ikiwemo Tanzania kuchukua hatua kali za kudhibiti mitandao jambo ambalo halikutakiwa kuwepo iwapo teknolojia ingetumika kusambaza habari na chambuzi za kina zenye manufaa kwa umma.
Ni mambo hayo makuu mawili—kubainisha fursa zilizopo nchini na duniani kwa ujumla kwa Watanzania na kukabiliana na habari za uzushi—yaliyofanya tuanzishe nukta.co.tz.
Tovuti hii ambayo pia ni rafiki zaidi katika simu au tableti itakuwa ikikuletea habari na makala ya uchambuzi ambayo yatakuwa yakilenga kuwasaidia Watanzania na ulimwengu mzima kukua katika kila nyanja ya maisha yao. Ndiyo maana tunasema kuwa tunakupa yale “Yanayokuhusu”
Kwa miezi sita tumekuwa katika majaribio na tumeona sasa tumefikia hatua ya kuanza kutekeleza wazo letu kuanzia Januari, 2018 ili kuleta kitu tofauti katika upatikanaji wa habari mtandaoni nchini.
Bila shaka utatufuatilia na kufurajia maudhui yaliyopo katika tovuti yetu na app yetu. Tufuate kwenye Facebook: @NuktaTanzania na Twitter: @NuktaTanzania.
Karibu sana.
Timu ya Nukta.co.tz