Mwelekeo mpya Mpango wa Uwazi serikalini Tanzania

May 11, 2023 12:37 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni maandalizi ya Tanzania kurejea katika jumuiya ya Uwazi Serikalini (OGP).
  • Wadau wakutana kujadili watakavyotekeleza malengo ya mpango huo. 
  • Malengo hayo ni pamoja na kujenga jamii ya wanamageuzi na kuchagiza uwazi katika taasisi za Serikali.

Dar es Salaam. Asasi za kiraia nchini Tanzania (Azaki) zimeaimeinisha malengo matano mahususi yanayotarajiwa kutekelezwa na Tanzania katika mpango wa Jumuiya ya Uwazi Serikalini (OGP) ikiwemo kujenga jamii ya wanaharakati wa wamageuzi na vinara wa Serikali inayokua, iliyodhamiria na iliyounganishwa.

Malengo hayo yameainishwa wakati wa maadhimisho ya Wiki ya OGP uliowakutanisha wadau wa Azaki, wanaharakati na  wanahabari, ambayo ni sehemu ya mpango mkakati wa utekelezaji wa OGP pamoja na  maandalizi ya Tanzania kurejea katika jumuiya hiyo ambayo ilijitoa mwaka 2017.

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze amewaambia washiriki kuwa kupitia malengo hayo mahususi wanatarajia kuwa na Serikali za wazi zinazofanya kazi na asasi za kiraia na wananchi moja kwa moja, kuimarisha demokrasia na kutoa matokeo bora ya kijamii na yanayoonekana.

“Lengo la kwanza ni kujenga jamii ya wanamageuzi, kupanua wanaharakati na vinara wa Serikali ya uwazi inayokua, iliyodhamiria na iliyounganishwa,” amesema Eyakuze jijini Dar es Salaam leo Mei 11, 2023.

Eyakuze ameongeza kuwa uwazi ngazi na matawi yote ya Serikali yanapofanya kazi na kutimiza vipaumbele vyake ni lengo lao la pili la mkakati huo ili kubadilisha tabia za viongozi kuanza kuzingatia uwazi katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Lengo la tatu  la mkakati huo ni kulinda na kupanua uhuru wa kiraia, ambao utatibu tatizo la kuporomoka kwa demokrasia jambo ambalo limetokea si Tanzania pekee bali katika mataifa mbalimbali duniani,” amesisitiza Eyakuze.

Wadau mbalimbali walioshiriki maadhimisho ya OGP wakijadiliana namna ya kukamilisha malengo ya programu hiyo. Picha l Esau Ng’umbi/Nukta Africa

Malengo mengine yaliyoainishwa na mkurugenzi huyo ni pamoja na kuhamasisha maendeleo ya pamoja juu ya uwazi Serikalini pamoja na kuwa kitovu cha hamasa ya ubunifu wa uwazi, ushahidi, rasilimali na simulizi.

Eyakuze ameongeza kuwa mwaka 2023 utakuwa mwaka wa mpito katika mfumo wa uwazi Serikalini ambapo wanashughulikia maboresho katika sehemu mbalimbali pamoja na kusubiri Serikali itekeleze dhamira yake ya kurejea kwenye jumuiya ya OGP.

Itakumbukwa Machi 2023, Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa akihutubia kwa njia ya mtandao katika mkutano wa pili wa kilele wa Demokrasia (Summit for Democracy) alitangaza kuwa Tanzania ina dhamira ya kurudisha uanachama wake katika jukwaa la OGP.

“Ningependa kuuhakikishia mkutano huu kwamba Tanzania itaendelea kusimamia demokrasia, haki za binadamu na utawala bora ndani na nje ya nchi, na tunalifanyia kazi suala  la Tanzania kurudi katika jumuiya ya Open Government Partnership (OGP) katika wakati muafaka,” alinukuliwa Rais Samia.

Tanzania ilikuwa mwanachama wa OGP kuanzia Septemba 2011 hadi Julai 2017 wakati ilipojiondoa na kutaja sababu kuwa  tayari imeshajiunga katika mpango mwingine uitwao Africa Peer Review Mechanism (APRM), ambao una malengo sawa na yale ya OGP.


Soma zaidi


Faida za OGP 

Baadhi ya mafanikio ambayo Tanzania iliyapata ikiwa mwanachama wa OGP katika kipindi cha miaka sita ni kuongezeka kwa uwazi ambapo tovuti za Serikali ziliboreshwa ikiwemo nifanyeje.go.tz, kuanzishwa kwa kituo cha takwimu wazi (open data) na kujazwa takwimu muhimu kutoka Serikalini pamoja na uchapishaji wa nyaraka muhimu za bajeti Kuboreshwa.

Open Government Partnership (OGP) ni nini?

Open Government Partnership (OGP) ni jumuiya ya kimataifa inayofanya jitihada kuzisaidia serikali na asasi za kiraia kufanya kazi pamoja kwenye masuala mbalimbali yanayoendana na vipaumbele vya nchi husika.

Katika mpango huu, asasi za kiraia, idara na taasisi mbalimbali za serikali hukaa na kutengeneza kwa pamoja mpango kazi wa kitaifa na hatua za kuchukuliwa na kujitolea, vyote vikiisaidia kuipa Serikali dira na mbinu mahususi katika kuwatumikia wananchi kwa ufanisi zaidi.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW