Mwanza na mapambano dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu
- Wafanyabiashara waeleza tahadhari wanazozichukua kupambana na kipindupindu.
- Viongozi wa Serikali wasema hakuna atakayeachwa nyuma.
Mwanza.Siku chache baada ya kuthibitishwa kwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu jijini Mwanza, Serikali na wananchi wa mkoa huo wameanzisha jitihada mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa huo ikiwemo kufanya usafi.
Jitihada hizo za mapambano dhidi ya kipindupindu jijini Mwanza zinajiri wakati kukiripotiwa visa 34 vya ugonjwa huo kutoka wilaya za Magu, Ilemela na Nyamagana.
Kutoka na hali hiyo, Nukta Habari imetembelea katika soko la Msuka lililopo kata ya Nyamanoro wilayani Ilemela na kushuhudia wafanyabiashara wa nafaka, chakula, mbogamboga na matunda wakichukua tahadhari mbalimbali kukabiliana na ugonjwa huo.
“Nachemsha maji ya moto ya kunawa wateja, chakula nahakikisha kinakuwa cha moto na kinafunikwa,” amesema Amina Matiku, Mama lishe sokoni hapo.
Afisa afya kata ya Nyamanoro Janeth Abraham (katikati) akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Msuka jijini Mwanza.Picha|Abdulshakur Mrisho
Amina amesema baada ya Kipindupindu kuingia mkoani humo, ameongeza tahadhari za kiafya kabla na baada ya kuandaa chakula ili kujilinda na kuwalinda wateja wake.
Naye Ruta Mshayja, Katibu wa soko hilo amesema kuwa usafi katika uandaaji wa chakula unaendana na usafi wa mazingira ambao hufanyika kila mwisho wa mwezi katika soko hilo.
“Tunasisitiza usafi wa maeneo yakiyotuzunguka, kila jumamosi na mwisho wa mwezi tunafanya usafi kwa pamoja, changamoto ni kuchelewa kwa wanaofuata taka baada ya sisi kuzikusanya” amesema Mshayja.
Kwa mujibu wa Afisa afya kata ya Nyamanoro Janeth Abraham, mpaka sasa wilaya Ilemela imeripoti wagonjwa wawili wa kipindupindu huku mmoja akitokea kata ya Nyamanoro ambapo soko hili linapatikana.
Soma zaidi:Waliougua kipindupindu Mwanza wafikia 34
Hakuna atakayeachwa nyuma
Aidha, Diwani wa Kata wa Nyamanoro George Maganiko, amesema kuwa mapambano ya ugonjwa huo yanayoenda sambamba na utolewaji wa elimu kwa wananchi hayatamuacha mtu nyuma ilikunusuru maisha ya jamii nzima.
“Tutapoteza watu wengi kata ya Nyamanoro tushirikiane kufanya usafi, tukimruka mtu ugonjwa ukianzia kwake hatutabaki salama,” amesema Mganiko.
Kiongozi huyo amewataka wafanyabiashara kuendeleza jitihada za kusafisha soko la Msuka na kuacha kutupa takataka katika mto uliokatiza sokoni.
Hamasa inayoendelea kutolewa na Diwani huyo ni muendelezo wa jitihada zilizoanzishwa na Mkuu wa mkoa huo Amos Mkalla Januari 10 mwaka huu aliyeagiza kutolewa kwa elimu pamoja na kudhibiti ugonjwa huo.
“Mkasimamie maeneo yote ya vilabu vya pombe ya kienyeji ili visiwe chanzo cha maambukizi ya ugonjwa huo lakini pia suala la usafi wa mazingira kuanzia masokoni na sehemu nyingine yapewe kipaumbele,” alisema Makalla katika kikao cha tahadhari ya ugonjwa wa kipindupindu.
Latest
