Muziki uliotafutwa zaidi mtandaoni mwaka 2021

January 19, 2022 10:43 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Orodha imeongozwa na wimbo kutoka kwa  mwanamuziki Olivia Rodrigo.
  • Wengine ni Lil Nas X, Walker Hayes na kundi la SB19.

Dar es Salaam. Kila mtu ana sababu za kutumia mtandao. Wapo ambao kwao mtandao ni mwalimu anayejibu kila swali analouliza, wengine ni soko la kila bidhaa wanazohitaji na pia wengine mtandao umewaajiri.

Matumizi hayo ya mtandao hurahisisha upatikanaji wa bidhaa, maarifa na kusaidia watu kutatua baadhi ya changamoto na wengine ukisaidia kuwasahaulisha matatizo kwa kutoa burudani. 

Kwa mwaka 2021, burudani ya muziki nayo haikuwa mbali kwani mtandao wa Google umetoa orodha ya vitu vilivyotafutwa zaidi mtandaoni na kati yake ni muziki.

Takwimu za mwenendo wa utafutaji (Google Search Trend) zinaonyesha kuwa wa mwaka 2022, burudani ya muziki imeshikiliwa na wasanii wa kimataifa akiwemo Olivia Rodrigo, SB19 na Lil Nas X.

Ngoma kali zaidi mwaka 2021 zilizotafutwa katika kitafutio hicho:

05: MAPA

SB19 ni kundi la wanamuziki wa kiume la huko nchini Ufilipino. Wimbo uliowaweka kwenye chati wanamuziki hawa ni “MAPA” ulioingia mtandaoni miezi nane iliyopita.

Wimbo huo umesikilizwa zaidi katika nchi za Venezuela, Nikaragua, Slovakia na Guatemala ambazo kiwango cha usikilizaji ni kati ya alama 90 hadi 100 ambapo alama 100 ni kiwango cha juu kwa vipimo vya Google Trends.

Hadi leo (Januari 19, 2022) Mapa umesikilizwa na watu milioni 63.8 kwenye mtandao wa YouTube na watu zaidi ya 924,000 duniani wamefurahishwa na wimbo huo.

           

04: Fancy Like

Kibao cha “Fancy Like” cha Walker Hayes ndicho kilichomweka Hayes hapa baada ya kusikilizwa zaidi huko nchini Marekani, Canada na New Zealand ukitamba kwa alama 27 hadi 100 kwa kipimo cha Google Trends.

Wimbo huo umeingia mtandaoni Juni4, 2021 na hadi leo umetazamwa na watu milioni 61.7 katika mtandao wa Youtube huku watu 495,000 wakiupenda wimbo huo.

Kilele cha Fancy Like kilikuwa wiki ya Septemba 12 hadi Septemba 18 2021 ambapo kiwango cha usikilizwaji kiligota kwenye alama 100.

03: Industry Baby

Hapa ngoma ya “Industry Baby” yake Lil Nas X akimshirikisha Harlow ndiyo mahala pake.

Ngoma hi imeingia mtandaoni tangu Julai 23, 2021 na hadi kufikia leo imetazamwa na watu milioni 281.6.

Wimbo huu umetafutwa zaidi wiki ya Julai 25 hadi Julai 31 ambapo kiwango cha utafutwaji kilifikia alama 100.

Wimbo huu umesikilizwa zaidi nchini Ghana, Nigeria na Zambia kwa kiwango cha kuanzia alama 86 hadi 100.


Soma zaidi:


02: Montero

Wimbo huu unamtambulisha Lil Nas x kwa mara nyingine kwenye orodha hii. Montero ama “Call me by your name” ni kati ya nyimbo zilizoibua mijadala kwenye mitandao ya kijamii kutokana na maudhi yake pamoja na video yake. 

Hata hivyo, hiyo ni mada nyingine, kwa leo, tusonge na takwimu. Wimbo huu umesikilizwa zaidi nchini Bolivia, Costa Rica na Uhispania.

Kilele cha wimbo huu kilikuwa wiki ya Machi 28 hadi Aprili 2 mwaka jana ambapo usikilizwaji wake ulifikia alama 100.

Montero umesikilizwa na watu milioni 424.2 na watu milioni 9.7 waliupenda.

01: Driver’s License 

Hii ni ngoma kutoka kwake Olivia Rodrigo, Mwanamuziki wa nchini Marekani ambaye ngoma hii kwa mujibu wa chaneli yake ya YouTube ni ngoma yake ya kwanza. 

Drivers License ambayo hadi leo imesikilizwa na watu milioni 334.8 tangu iingie YouTube Jan 8, 2021 na ulikuwa kwenye kilele cha alama 100 wiki ya Januairi 10 hadi Januari 16.

Wimbo huo umetamba zaidi nchini Marekani, Ufilipino, Jamaica na Afrika Kusini.

Mwaka 2021 ni wa kipekee kwa Rodrigo mwenye umri wa miaka 18 ambaye wimbo wa kwanza kutoa umemfanya atambe duniani kote.

Enable Notifications OK No thanks