Mtaala wa takwimu kwa viongozi serikali za mitaa wazinduliwa

December 6, 2021 2:05 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Utawasaidia kutumia takwimu katika mipango ya maendeleo.
  • Pia utaongeza chachu ya maendeleo kwa jamii.

Dar es Salaam. Maabara ya Takwimu nchini Tanzania (Tanzania Data Lab) imezindua mtaala wa takwimu na uongozi unaolenga kuwasaidia viongozi wa serikali za mitaa kutumia takwimu kwa usahihi katika shughuli za maendeleo wanazozisimamia.

Mtaala huo umezinduliwa katika tamasha la takwimu (Data Tamasha) linalofanyika kwa siku tatu (Disemba 6-8, 2021) jijini Dar es Salaam lenye lengo la kuchechemua matumizi ya takwimu katika kufanya maamuzi sahihi yanayohusu maendeleo.

Mtaala huo umengenezwa na DLab ikishirikiana na Taasisi ya Mafunzo ya Serikali za Mitaa (LGTI) ambao utakuwa msaada mkubwa kuwajengea uwezo viongozi kutumia takwimu katika mipango hasa inayohusu huduma za kijamii.

Mkurugenzi wa masuala ya Ushiriki wa Jamii wa DLab, Omar Bakari amesema hamasa kubwa nyuma ya mtaala huo ni kurahisisha utoaji wa wa huduma za jamii na kuwaletea wananchi maendeleo.

Bakari amesema, maamuzi mengi ya maendeleo yanafanyika katika ngazi ya serikali za mitaa, hivyo kuna umuhimu wa viongozi wake kuwa na uwezo wa kutumia vizuri takwimu ili kufanya maamuzi yenye maslahi kwa jamii.

“Baada ya ushirikiano wetu na serikali za mitaa tukaona ni kwamba kuna umuhimu wa kuwajengea uwezo waheshimiwa madiwani na inawezekana baadaye tukaenda kwa waheshimiwa wabunge kwa sababu wao ndiyo wanafanya maamuzi,” amesema Bakari. 

Amesema nia na madhumini ni kuhakikisha maamuzi wanayoyafanya yanazingatia uhalisia ili rasilimali zinazowafikia zinatumika vyema kuleta matokeo yanayotakiwa.

Tamasha hilo linafanyika kwa siku tatu kuanzia leo (Disemba6, 2021). Picha| Data Lab.

Tamasha la takwimu limeanza kufanyika nchini tangu mwaka 2017 ambapo lilihudhuriwa na watu zaidi ya 300 na mwaka 2019 lilipohudhuriwa na watu zaidi ya 800 kutoka nchi mbalimbali.

Kwa mwaka huu, wadau mbalimbali wanahudhuria katika mijadala na maonyesho ya bidhaa na taasisi zinazohusu matumizi ya data.

Kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa inayomiliki tovuti ya habari ya www.nukta.co.tz ni miongoni mwa washiriki wa tamasha hilo. 

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Masauni amesema, matumizi ya takwimu yatasaidia nchi kupata majawabu kwa kutumia mifumo ya kidijitali katika kupeleka utumishi mbele zaidi na kutatua  changamoto za Watanzania kufikia maendeleo endelevu.

“Takwimu hizi zinazoenda kutoa majawabu ya changamaoto zilizopo katika sekta ya uchumi zisambazwe inavyotakiwa ili kuwafikia walengwa kwa wakati katika ngazi zote za utawala. Hapa nchini,” amesema Masauni.

Amewasihi wadau wa takwimu kuandaa mpango kazi ili takwimu zisambazwe na zitumike na watunga sera na wanasiasa katika kupanga mipango endelevu ya wananchi.


Soma zaidi


Matunda ya takwimu

Matumizi ya takwimu yameendelea kuonyesha umuhimu wake katika nyanja mbalimbali. 

Mathalan, katika hotuba ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliyoitoa Septemba 14, 2021 wakati wa uzinduzi wa mkakati wa uelemishaji wa sensa Dodoma, alisema takwimu ni muhimu kwa serikali katika ugawaji wa rasilimali.

Kiongozi huyo wa nchi alisema, endapo Serikali haina hesabu au takwimu sahihi, haiwezi kugawa rasilimali na kutoa huduma kwa haki, uwiano na inavyopaswa zitolewe.  

“Tumeweka tozo ya makazi. Makazi yale kulipiwa kiasi fulani cha fedha lakini hatukuwa na idadi sahihi ya nyumba na makazi ya Watanzania nchini,” alisema rais Samia.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW