Msimamo wa Tanzania uhifadhi wa Ziwa Tanganyika

February 10, 2022 12:11 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Yakubali kutekeleza miradi inayoanzishwa na mamlaka ya bonde la ziwa hilo.
  • Miradi hiyo ya kijamii inalenga kuwatoa wananchi katika umaskini.

Dar es Salaam. Serikali imeahidi kuunga mkono utekelezaji wa awamu ya pili ya programu ya kikanda ya hifadhi ya mazingiraya Bonde la Ziwa Tanganyika kutokana na umuhimu wa programu hiyo kwa wananchi wa nchi nne ikiwemo Tanzania.

Nchi nyingine zinazofaidika na programu hiyo ni Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (Congo DRC), Rwanda na Zambia.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba ametoa ahadi hiyo leo Jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Sekretarieti ya Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA) uliofika ofisini kwake kuomba idhini ya Serikali ya kuanza kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Amesema kuwa Serikali inaunga mkono kuanza kwa Awamu ya Pili ya Programu ya Kikanda ya Hifadhi ya Mazingira ya Bonde la Ziwa Tanganyika (PRODAP II) baada ya Awamu ya kwanza ya program hiyo iliyokamilika mwaka 2014 kuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wanaozunguka Bonde la Ziwa Tanganyika katika nchi hizo nne za Kikanda.

“Katika kuandaa mradi wa awamu ya pili tumekubaliana kuwa sisi kama Wizara ya Fedha na Mipango tutaratibu Wizara nyingine ili tupate vipaumbele ambavyo tutaviwasilisha katika taasisi yake ili iweze kuviunganisha na vile vya nchi wanachama kisha kuiwasilisha katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)

miradi hiyo ikitekelezwa itaenda sambamba na malengo ya kupunguza umasikini kwenye jamii inayozunguka eneo hilo.

Alisema kuwa katika Awamu ya kwanza, Mamlaka ya Hifadhi ya Ziwa Tanganyika ilitekeleza mradi wa ujenzi wa masoko eneo la Kibirizi mkoani Kigoma ambapo wameweka vifaa mbalimbali vya uhifadhi wa samaki na dagaa, maeneo ya kukaushia samaki na maghala ya kuhifadhia samaki.

Tutuba amesema kuwa miradi mingine iliyotekelezwa ni ujenzi wa vyumba vya  madarasa katika shule 22, vyoo kwenye shule 18, miradi mitano ya vituo vya afya, nyumba za watumishi kwenye vijiji viwili na zahanati moja na miradi 10 ya maji katika vijiji vinavyozunguka Ziwa Tanganyika.

Miradi mingine ni ujenzi wa kilomita 65.6 za barabara, madaraja mawili na kufanya kampeni 180 za kujikinga na magonjwa ya kuambukiza ukiwemo Ukimwi.

Miradi iliyotekelezwa kupitia ushirikiano huo imeleta maendeleo uendelevu ya mazingira katika Ziwa Tanganyika na inagusa sekta mbalimbali za kuondoa umasikini kwa wananchi.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba, akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Burundi Mhe. Dk Jilly Maleko na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), Tusang Sylvain Tusanga baada ya kikao kilichofanyika jijini Dodoma. Picha| Wizara ya Fedha na Mipango.

Balozi wa Tanzania nchini Burundi, ambaye anasimamia maslahi ya Tanzania katika Sekretarieti ya Mamlaka ya Ziwa Tanganyika yenye makao yake makuu nchini Burundi, Dk Jilly Maleko, amesema kuwa lengo la ziara ya Sekretarieti hiyo nchini ni kufanya mazungumzo kuhusu uwezekano wa kupata mkopo kutoka AfDB kwa ajili ya kutekeleza awamu ya pili ya Programu ya Kikanda ya Uhifadhi wa Mazingira ya Bonde la Ziwa Tanganyika (PRODAP II).

Alisema kuwa awamu ya kwanza ya mradi huo kwa upande wa Tanzania ulitekelezwa chini ya uratibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa gharama za dola za Marekani milioni 7.2 (Sh16.6 bilioni) kupitia ufadhili wa AfDB.

Mamlaka ya LTA imefanya mazungumzo na AfDB kuhusu uwezekano wa kutekelezwa kwa PRODAP II kwa msaada au mkopo wa masharti nafuu na tayari sekretarieti hiyo imefanya mazungumzo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Zambia ambazo zimeonyesha nia ya kuendelea na utekelezaji wa programu hiyo kwa awamu ya pili.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika, Tusang Sylvain Tusanga amezishukuru nchi wanachama hususani Tanzania kwa kuonyesha nia thabiti ya utekelezaji wa miradi hiyo na kutoa michango yake ya kila mwaka kikamilifu tangu mwaka 2000.

Amesema ushirikiano huo umeleta tija katika Bonde la Ziwa Tanganyika na kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi miundombinu ya barabara, afya, elimu, uvuvi na hifadhi ya mazingira. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW