Moto wazidi kudhibitiwa Mlima Kilimanjaro

October 13, 2020 8:51 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Vikosi vinavyoshiriki zoezi la kuzima moto Mlima Kilimanjaro vikiendelea na kazi. Picha|Tanapa.


  • Helikopta hiyo inayoruka juu ya mlima inaangalia ukubwa wa eneo lililoathirika na maeneo ambayo bado yanaweza kuzuka kwa moto upya.
  • Nguvukazi ya watu 500 inaendelea kuudhibiti moto huo usisambe eneo kubwa.
  • Tanapa bado haijaweka wazi chanzo cha moto huo. 

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hifadhi za Taifa nchini Tanzania (Tanapa) imesema moto uliozuka juzi Mlima Kilimanjaro umeendelea kudhibitiwa hasa katika maeneo hatarishi yenye kushika moto haraka, huku ikiongeza nguvukazi ikiwemo matumizi ya helikopta kuzima moto huo. 

Moto huo ulizuka Jumapili Oktoba 11, 2020 katika eneo la Whona ambacho ni kituo cha kupumzikia wageni wanaotumia njia ya Mandara na Horombo kupanda mlima huo mrefu kuliko yote Afrika.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Mawasiliano wa Tanapa, Pascal Shelutete katika taarifa yake amesema moto huo unaendelea kudhibitiwa na vikosi vinavyoshiriki zoezi hilo likiwemo Jeshi la Zimamoto. 

Amesema jumla ya nguvukazi ya watu 500 wako eneo la tukio kukabiliana na moto huo ambao kwa sehemu kubwa tayari umedhibitiwa. 

“Eneo ambalo kwa sasa limebaki na moto ni eneo maarufu la Mlima Kifunika na eneo la mashariki kuelekea Wilaya ya Rombo,” amesema Kamishna Shelutete katika taarifa yake leo Oktoba 13, 2020. 


Soma zaidi:


Ili kuhakikisha wanafanikisha zoezi la kuzima moto huo, pia wanatumia helikopta ambayo  inaangalia eneo liliathirika na kufuatilia maeneo mengine yanayoweza kushika moto. 

“Kampuni ya State Aviation inayohusika na usafiri wa anga imetoa msaada wa helikopta yake inayoruka juu ya mlima kuangalia ukubwa wa eneo lililoathirika na maeneo ambayo bado yanaweza kuzuka kwa moto upya,” amasema Kamishna huyo.

Amesema bado wanafanyia kazi taarifa ya chanzo cha moto huo lakini nguvu kubwa imeelekezwa kuuzima moto huo kwanza. 

Hata hivyo, Tanapa imesema inachukua tahadhari zote ili kuhakikisha usalama wa wageni na vifaa vyao unaimarika bila kuathiri shughuli za utalii ambazo zinaendelea kama kawaida hususan njia ya Marangu iliyoathirika na moto husika.

Mamlaka zinaeleza kuwa wastani wa watu 50,000 hupanda mlima huo kila mwaka. 

Enable Notifications OK No thanks