Mjadala gharama, ubora wa mabehewa SGR washika kasi Tanzania
- Baadhi ya watu mtandaoni wahoji bei, ubora na muonekano wake.
- Ni mabehewa 14 ya treni yaliyonunuliwa na Serikali hivi karibuni.
- Serikali yawatuliza ikisema mabahewa hayo ni mapya.
Dar es Salaam. Mjadala mkali wa juu ya mabehewa mapya ya reli ya kisasa (SGR) yaliyoingia nchini hivi karibuni umeshika kasi mtandaoni hasa Twitter huku baadhi ya watu wakihoji gharama na hali ya mabehewa hayo.
Novemba 25, 2022, Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilitangaza kupokea mabehewa 54 kutoka Korea Kusini ikiwa ni mkakati wake wa kuanza kutoa huduma ya usafiri katika reli hiyo inayojengwa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na baadaye kuelekea mkoani Kigoma.
Tangu kupokelewa kwa mabehewa hayo kumeibuka maoni mbalimbali juu ya muonekano, ubora, na uimara wa usafiri huo huku baadhi wakihoji uhalisia wa gharama zilizotumika kununua mabehewa hayo na muonekano wake.
Mmoja wa wachangiaji wa hoja hiyo kwenye mtandao wa Twitter ni aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangalla aliyedai kuwa mabehewa hayo siyo mapya bali yametumika.
“Hili behewa moja (tena used) limenunuliwa kwa Sh ngapi? Tumeambiwa yapo haya mabehewa 54, yamenunuliwa kwa dola za kimarekani milioni 59…. Kwa nini wamenunua used?,” ameandika Dk Kigwangalla katika ukurasa wake wa Twitter.
Behewa ya mizigo imenunuliwa kwa TZS 209m, ya abiria ya Escape from Sobibor imenunuliwa kwa 2.2b; kilichoongeza thamani kwa zaidi ya mara 10 hapo ni nini? Makochi? AC? Taa? Vyoo? Vioo vya madirisha? Ama ni nini? Juzi niliwaambia tufundishe watoto wetu ‘critical thinking!’? pic.twitter.com/QlQnUxEmYk
— Dr. Hamisi Kigwangalla (@HKigwangalla) December 5, 2022
Watumiaji hao wa mitandao ya wanaeleza kuwa muonekano wa mabehewa hayo haudhihirishi kuwa ni mapya. Pia muundo wake siyo wa kuvutia na kisasa.
“Hayo mabehewa hatuyataki ni mabaya Sana hayavutii kwani muundo wake ni wa kizamani Sana, hivi mnatuonaje lakini?? Hii nchi,” amesema fredricktaus, mtumiaji wa Instagram.
Mtumiaji mwingine wa mtandao huo ameeleza hoja zake kuwa mabehewa hayo ni mpya kutokana Serikali kuonyesha hatua zote za utengenezaji mpaka kuingia nchini.
“Hayo ni mapya na yalionyeshwa yakitengenezwa kiwandani,” anasema mtumiaji wa Twitter aliyetambulika kwa jina la Luno.
“Mama alituambia tutanunua used (vyenye hali njema) na tutaanza navyo tukisubiri vipya hapo badae, TRC wanatuambia hivi vilivyokuja ndio vipya, wadau wanasema hivi sio vipya, sasa sisi wananchi wa kawaida tusimame upande upi?,” amesema Dr Mmbaga (@ZakayoMmbaga) wa Twitter.
Soma zaidi:
Mabehewa ni mpya?
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa ametoa ufafanuzi juu ya kauli na mijadala iliyopo mitandaoni kuhusu mabehewa hayo na kusema siyo ya mtumba na gharama yake ni halisi.
“Yale mabehewa sio ya mtumba wala used ni mabehewa mapya, sasa anayezungumza mnaweza kumuuliza vyanzo vyake ni wapi anapata, ni mabehewa yaliyokuwa yakitengezwa kwa miaka miwili, katika manunuzi kuna sheria ambapo lazima kabla hamjasema huyu hapa tunaenda nae lazima kuwe na ulinganifu wa bei,
“Sasa mtu anapoibuka tu na kuanza kusema mabehewa yana kiasi fulani ni jambo la ajabu kidogo ila mtamuuliza yeye,” amesema Kadogosa jana Desemba 5, 2022.
“Kuhusu bei ya Mabehewa yapo 59 na sio 14 yamekuja kwa awamu ya kwanza, mwaka kesho Mei tutapata mengine 45 jumla yatafanya kuwa 49 na bei aliyoitoa bei ni Dola Milioni 55.6 (Sh129.7 bilioni) ndiyo bei ya Mabehewa,” amesema Kadogosa.
Mabehewa yaliyowasili nchini ni mpya kwa mujibu wa TRC na yametengenezwa na kampuni ya Sung Shin Rolling Stock Technology Limited ya nchini Korea Kusini.
Moja ya behewa liliwasili hivi karibuni kutoka Korea Kusini. Mabahewa hayo yameibua mjadala mkali kuhusu bei na ubora huku baadhi wakisema siyo mapya. Picha | TRC.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa Novemba 25 alitoa ufafanuzi kuhusu aina ya treni zinazokuja nchini Tanzania na kueleza kuwa taratibu zote za ununuzi zimefuatwa.
“Serikali imeagiza vichwa vya treni ya umeme kwa ajili ya kuvuta behewa hizi, katika treni za umeme kuna vichwa vya treni aina 3 ambavyo ni ‘Electric Locomotive’ kazi yake ni kuvuta behewa kama hizi 14 zilizokuja, ‘Electric Multiple Unit’ (EMU) kichwa cha treni ya aina hii kimeungwa na behewa pamoja, na aina ya tatu kichwa cha treni ni kile ambacho kinatumika mahususi kwa ajili ya mwendo kasi wa hali ya juu,” alisema.
Waziri huyo aliweka wazi kuwa “kwenye utaratibu wa treni za umeme, treni inayokwenda mwendokasi zaidi ya kilomita 200 kwa saa treni hiyo inaitwa ni ya mwendokasi, na zile treni ambazo mwendo wake ni chini ya kilomita 200 kwa saa zinaitwa treni za kawaida. Hivyo treni yetu ya Tanzania ni treni ya umeme ya kawaida inayokwenda kilomita 160 kwa saa.”
Serikali imetoa Dola za Marekani million 295.74 (Sh690.1 bilioni) kwa kampuni ya Hyundai Rotem ya Korea Kusini kwa ajili ya ununuzi wa vichwa vya treni vya umeme 17 na seti za treni za kisasa (Electric Multiple Unit – EMU) 10 na ‘locomotive simulator’ 1 ya umeme.
Pia kuna mabehewa 1,430 ya mizigo ambayo yako katika matengenezo.
Msemaji wa Serikali aingilia kati
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa aliyekuwa akihojiwa kwenye kipindi cha The Big Agenda kinachorushwa na Star Tv amesema anasikitishwa na uzushi unaendelea na kuwaomba wanahabari, wananchi kuacha mara moja kusambaza uzushi na upotoshaji huo kuhusu mabehewa hayo.
“Serikali imeyanunua mabehewa hayo kwa Sh55.6 bilioni na siyo dola milioni 59…Serikali imeyanunua kwa kufuata taratibu za manunuzi ambapo zabuni inatangazwa na anayeshinda kwa mujibu wa vigezo anashinda,” amesema Msigwa.
Msigwa amesema mabehewa hayo yaliyonunuliwa ni mapya na yamekidhi vigezo vyote vya ubora, tofauti na maoni yanayotolewa na watu mtandaoni wakiwemo wanasiasa.