Microsoft sasa jino kwa jino na Google katika utoaji wa taarifa

December 4, 2019 8:28 am · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link
  • Imefanya maboresho ya kitafutishi chake cha Microsoft Edge ili kuwapa wateja wake uwezo mkubwa wa kupata vitu wanavyotafuta mtandaoni.
  • Hatua hiyo inaweza kuleta ushindani mkubwa na kampuni nyingine za teknolojia kama Google inayomiliki kitafutishi cha Chrome.

Dar es Salaam.Kampuni ya teknolojia ya Marekani ya Microsoft imefanya maboresho ya kitafutishi chake (Web Browser) kiitwacho Microsoft Edge ili kuwaleta karibu watumiaji wa bidhaa zote zinazotumia mfumo wa Microsoft katika kutafuta mambo mbalimbali kwenye mtandao.

Kampuni hiyo imeamua kutanua matakwa ya wateja wao na kuwawezesha kupata matokeo mengi zaidi kama ilivyo katika kitafutishi cha Chrome kinachomiliwa na kampuni shindani ya Marekani ya Google.

Huenda hatua hiyo ikaleta mashindano makubwa kati ya kampuni hizi mbili baada ya Microsoft kuamka na kuwapa wateja wake kile walichokuwa wanakikosa hapo awali.

Maboresho hayo yameenda sambamba na mwonekano mpya wa kitafutishi hicho kwa kubadili nembo yake. 

Baadhi ya wataalamu wa maswala ya teknolojia wanasema maboresho hayo yataleta ushindani mkubwa kwa kampuni hizi mbili akiwemo mtaalamu wa kujitegemea katika maswala ya teknolojia, Tonny Gerald.

“Hayo maboresho yaliyofanyika  yana maana kubwa sana. Huu ni mwanzo wa kampuni hizi mbili kuingia ushindani baada ya wateja wengi wa Microsoft kuhama kwa sababu ya ufinyu wa huduma kulingana na Browser zingine (Vitafutishi) kama Firefox, Chrome na nyingine,” amesema Tonny.

Mabadiliko yake huenda yakarudisha wateja wote waliopote. Picha | Mtandao.

Ukweli ni kwamba wateja wengi wa Microsoft walikuwa wanachukizwa na hali ya kutokupata matokeo wanayotaka katika kitafutishi hicho mpaka wafanye mchakato mrefu wakuingia kwenye kitafutishi cha Google ndipo wapate wanachokitaka.

Jambo hilo lilifanya watu wengi watanie kuwa Microsoft Edge ilikuwa ni mlango tu wa kupakua programu ya Chrome mara baada ya mtumiaji kununua kompyuta mpya au kufunga mfumo endeshi mpya katika kifaa chake. 

Sarah Mwalukama ni mmoja wa watumiaji walioamua kuhama kutoka matumizi ya simu janja ya Nokia Lumia mpaka Samsung kutokana na baadhi ya mambo likiwemo hili la kutokuwa na uwezo wa kupata baadhi ya matokeo kwenye kitafutishi mtandaoni.

“Moja ya sababu kwanini nilihama na kuacha Nokia ni hilo, hivyo kama kuna maboresho hayo naamini ni moja ya hatua ya kuwavuta wateja wake karibu zaidi”,” amesema Mwalukama.


Zinazohusiana:


Mabadiliko huenda yakaleta manufaa makubwa kwa watumiaji wa Microsoft kwani wataweza kupata kila wanachotafuta mtandaoni kama ilivyo kwa kampuni nyingine za teknolojia kama Google.

Pia inaweza kuifaidisha kampuni hiyo kujitanua kimasoko ili kuwafikia wateja wengi duniani kwa kuwa bidhaa nyingu zinazotumiwa na watu wengi.

Enable Notifications OK No thanks