Microsoft kuwezesha upigaji simu kwa kompyuta
Unaweza kupokea na kupiga simu kwa kutumia kompyuta yako, kuangalia simu zilizoingia na kutoka kwenye simu yako na hata kuangalia watu wako unaowasiliana nao. Picha| Windows.
- Imebuni programu maalum itakayowawezesha watumiaji wa simu kupiga na kupokea simu kwa kutumia kompyuta zao.
- Programu hiyo itakuwa inatumika na programu za “Windows insiders”
- Itasaidia kupunguza usumbufu wanaopata kwa watu wenye shughuli nyingi kwenye kompyuta.
Dar es Salaam. Ni usumbufu pale unapokuwa unafanya kazi zako kwenye kompyuta na simu inaita, jambo linalokulazimu kuacha kufanya unayoyafanya ili uongee na simu yako.
Siyo kupokea simu tu, hata pale unapohitaji kupiga simu au kuangalia namba muhimu, unahitaji kuachana na kompyuta yako ili uongee na simu, jambo linalosimamisha kwa muda shughuli zako muhimu.
Usumbufu huo umeifanya kampuni ya programu za kompyuta ya Microsoft kutafuta njia rahisi ya kutatua changamoto hiyo kwa kuwezesha mawasiliano ya simu kufanyika moja kwa moja kwenye kompyuta.
Programu hiyo itawafaidisha wamiliki halali wa programu tumishi ya “Windows 10” (Windows insiders) kuunganisha simu zao na kompyuta na kufanya mawasiliano yote ya simu kwenye kompyuta.
“Windows insider” ni mtumiaji wa programu za windows za kampuni ya Microsoft ambaye ana leseni thabiti ya “Windows 10” na “windows server 2016” ambapo akijisajili, anaweza kupata na kutumia programu hata zilizo kwenye majaribio ambazo zinatumika na waendeleza programu (developers).
Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo ya Marekani, “insider” hatolazimika kutumia simu na kompyuta kwa wakati mmoja hasa katika masuala ya mawasiliano.
Kupitia programu hiyo (preview build 18999 for insiders (201H1)), unaweza kupokea na kupiga simu kwa kutumia kompyuta yako, kuangalia simu zilizoingia na kutoka kwenye simu yako na hata kuangalia watu wako unaowasiliana nao (contacts) endapo tu umeiunganisha na kompyuta yako na kama simu yako inatumia programu wzeshi ya Android 7 na kuendelea.
Zinazohusiana
Hata hivyo, Microsoft imeonya kuwa programu hiyo ipo kwenye majaribio na huenda isiwe salama ukilinganisha na zile ambazo zimeruhusiwa kutumika rasmi.
“Kama ilivyo kawaida ya programu zilizo kwenye majaribio, programu hizi zinaweza kuwa na virusi vinavyoweza kusababishia matatizo baadhi ya watumiaji,” imeeleza Microsoft katika taarifa yake.
Ugunduzi huu ni mwendelezo wa Microsoft kuwapatia wateja wake kilicho bora kwa kutafuta suluhisho la matatizo yao.
Hivi karibu, kampuni hiyo ilitangaza nia ya kuingiza sokoni kifaa kinachofanana na kufanya kazi kama simu kitakachokuwa kinatumia programu endeshi ya Android badala ya Windows iliyozoelekeka ma watumiaji wake.