Michezo ya bahati nasibu ya Taifa: Burudani ya enzi na enzi

July 6, 2024 7:36 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Kampuni ya nchini Afrika Kusini ITHUBA Africa kwa kushirikiana na kampuni ya Kitanzania, SF Group wametangaza rasmi kuingia katika soko la Tanzania.
  • Hatua hiyo ni ya kufufua michezo ya bahati nasibu ya Taifa ambayo imepotea kwa muda mrefu.

Ukisikia neno bahati na sibu ya Taifa unakumbuka nini?

Kwa baadhi wanaweza hisi ni michezo “ya kubeti” ambayo vijana wengi wa sasa wanafanya lakini kwangu mimi ni zaidi ya hilo.

Kwangu mimi, jina bahati nasibu ya Taifa limebeba makuzi, malezi na historia ambayo huenda vijana wengi wanaweza wasielewe.

Turejee 2000

Nikisikia bahati na sibu ya taifa, binafsi akili yangu inanirudisha miaka ya 2000. Nilikuwa nikiwaona wajomba na kaka zangu wakiwa kwenye televisheni wameshikilia vikaratasi wakitazama wachezeshaji kwenye runinga waliokuwa wakichezesha michezo ya kubahatisha. 

Michezo hiyo ilichezeshwa kwa namna mbalimbali lakini ninayokumbuka ni kuona kitu kama gurudumu kubwa lenye mipira midogo midogo ya rangi ya njano yenye namba. Baada ya kuzungushwa, mpira wenye namba uliotoka ndio ulibeba namba ambayo ingeendana na namba moja iliyopo kwenye tiketi za wachezaji.

Mtu ambaye namba yake ingeendana na namba ya mpira ndiye aliyeibuka kama mshindi.

Kwa umri niliokuwa nao, sikuelewa kitu. Nilihisi ni michezo ya watu wazima na sikuwa na haja nayo lakini nakumbuka mara moja moja kusikia watu wakisimuliana kupata zawadi baada ya namba za tiketi zao kutajwa.

Michezo ya bahati nasibu ya Taifa ni moja ya nyenzo za burudani hasa kwa vijana na chanzo cha mapato kwa Serikali. Picha: Microsoft Designer. 

Historia iliyopotea

Kwa mimi kijana wa miaka hiyo ndilo nililolifahamu lakini wapo ambao wanasema michezo ya bahati nasibu ya Taifa ilienda nyuma zaidi. Enzi ambazo mitandao ya kijamii haikuwepo Tanzania, enzi za redio. 

Mariam Samora (45) anasema wazazi wake walikuwa wachezaji michezo ya kubahatisha. 

“Mama yangu alikuwa akinunua tiketi na kukwangua na kutega masikio yake redioni ili kuona kama ameshinda au laah!. Kwenye tiketi yake, niliona namba zote za mwanzo zikitajwa sawa sawa ila namba ya mwisho tu ndo inakataa. Nilisikia akisema kwa uchungu, aaaaaah!,” anasema Samora.

Hata hivyo, baada ya muda, sikusikia tena kuendelea kwa michezo hiyo. Kwa baadhi wanaweza kuikumbuka kama Lotto.

Afrika Kusini kuirejesha

Hivi karibuni, kampuni ya nchini Afrika Kusini ITHUBA Africa kwa kushirikiana na kampuni ya Kitanzania, SF Group wametangaza rasmi kuingia katika soko la Tanzania.

Hatua hiyo ni ya kufufua michezo ya bahati nasibu ya Taifa ambayo imepotea kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kampuni ya ITHUBA, hatua hiyo imekuja baada ya kukabidhiwa rasmi leseni ya uendeshaji wa mchezo wa Bahati Nasibu ya Taifa kwenye hafla fupi iliyofanyika Juni 28, 2024 katika ofisi za Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania jiijni Dar es Salaam. 

Mkurugenzi Mtendaji wa ITHUBA, Charmaine Mabuza alisema, kuunganishwa kwa teknolojia yao na uzoefu wa SF Group katika soko la Tanzania kutawezesha Watanzania kushiriki katika michezo ya kipekee kupitia jukwaa lililoundwa maalumu kwa ajili ya soko la Tanzania.

Ili kufanikisha hilo, ITHUBA imedhamiria kufanya uwekezaji wa dola za Marekani milioni 20 ambayo ni takribani Sh53.1 bilioni.

“Washiriki watapata fursa ya kucheza michezo mipya ya kusisimua na kupata ofa mbalimbali ambazo pia zitachangia katika kuleta mabadiliko kwenye uchumi wa jamii,” alisema Mabuza.

Manufaa ya kiuchumi kwa Watanzania

Kupitia ujio wa uwekezaji huo, yapo manufaa mbalimbali ya kiuchumi ambayo yatakuwa katika ngazi ya kitaifa na hata binafsi kwa Watanzania.


Soma zaidi >> Michezo ya kubahatisha, bia kugharamia bima ya afya kwa wote


Wafanyabiashara watanufaika na malipo ya kamisheni na pia kuvutia wateja zaidi katika maduka yao kutokana na mauzo ya tiketi za bahati nasibu. 

Kwa upande wa serikali, makusanyo ya kodi yanapatikana katika uuzaji wa tiketi hizo yatasaidia taifa katika ujenzi wa uchumi na kuendeleza miradi mbali mbali ambayo inaendelea nchini.

Mwenyekiti wa Bodi ya Michezo ya Bahati Nasibu nchini Tanzania, Balozi Mero amesema ujio wa ITHUBA ni muendelezo wa usukumwaji wa gurudumu la michezo hiyo nchini.

“Ubia wao ni fursa nzuri ya kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini kupitia mapato yatakayotokana na michezo ya bahati nasibu ya taifa. Tuna shauku kubwa kufanya kazi kwa ukaribu na ITHUBA ili kuleta mabadiliko chanya na kuboresha maisha ya Watanzania,” amesema Mero.

Historia inayojirudia

Kurudi kwa michezo ya kubahatisha ya Taifa, kunanirudisha enzi za utoto wangu na enzi ambazo nilikuwa nikiona watu wakisubiri jioni kuona kama wameshinda au laah.

 Hamasa, msawasha na kelele za ushindi zilikuwa zikinisisimua na kunipa hamasa ya kucheza lakini sikuwa na uelewa wa nini kilikuwa kikiendelea.

Kwa jinsi teknolojia ilivyokua, ninahamu na hamasa ya kuona teknolojia ambayo ITHUBA italeta kuendeleza mchezo huu.

Enable Notifications OK No thanks