Mhandisi Nditiye atoa ufafanuzi usajili wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole

April 23, 2019 7:56 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Mfumo wa usajili simu kwa kutumia alama za vidole utasaidia kupata takwimu sahihi za watumiaji wa simu za mkononi na huduma za fedha kwa ajili ya kuweka mipango sawa ya kuendeleza sekta na uchumi wa Taifa. Picha|Mtandao.


  • Amesema mfumo huo haulengi kuwazuia wananchi kutumia laini zaidi ya moja lakini unakusadia kudhibiti utitiri wa laini na uhalifu. 
  • Mtumiaji anayetaka kutumia laini zaidi ya moja kwa mtandao mmoja atalazimika kutoa taarifa ya maandishi. 
  • Mfumo huo utasaidia kuboresha huduma za mawasilino na upatikanaji wa taarifa sahihi za watumiaji wa simu. 

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema mfumo mpya wa usajili laini za simu kwa kutumia alama za vidole haulengi kuwazuia wananchi kutumia laini zaidi ya moja lakini unakusadia kudhibiti utitiri wa laini za simu na uhalifu wa mtandao.

Mhandisi Nditiye ametoa ufafanuzi huo leo (Aprili 23, 2019) bungeni wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Rombo, Joseph Selastine ambaye amesema mfumo huo utawazuia wananchi kuwa na laini zaidi ya moja katika maeneo ambako baadhi ya laini hazipatikani. 

“Ni kweli tumezielekeza kampuni za mawasiliano ya simu za mkononi kuanza utekelezaji wa usajili wa alama za vidole na zoezi hilo litaanza kuanzia tarehe 1 Mei,” amesema Nditiye.

Hata hivyo, amekanusha uvumi unaendelea katika mitandao ya kijamii kuwa baada ya utekelezaji wa zoezi hilo mtu hataruhusiwa kumiliki laini zaidi ya moja lakini ukweli ni kuwa mtumiaji atakuwa na laini moja kwa mtandao mmoja na endapo atataka kuwa na laini zaidi ya moja kwa mtandao mmoja atalazimika kutoa taarifa ya maandishi katika mamlaka husika. 

“Pia niwahakikishie wabunge kwamba hakuna sehemu ambako nilizungumza kwamba mtumiaji atakuwa na laini moja tu ya simu hapana! Nilichozungumza ni kwamba tunatamani kila mtanzania awe na laini moja ya simu kwa mtandao mmoja,” amesisitiza Mhandisi Nditiye. 

Katika hatua nyingine amemuomba Spika wa Bunge, Job Ndugai kuruhusu watoa huduma za simu za mkononi kupeleka madawati maalum ili kuwezesha wabunge kufanya usajili wa laini za simu kwa kutumia lama za vidole. 

Amesema mfumo huo mpya pia utasaidia kupunguza utitiri wa laini za simu zisizofuata utaratibu uliowekwa na kutumika katika matukio ya uhalifu ikiwemo wizi wa fedha kwa njia ya mtandao. 

Wakati akiuliza swali, Selastine amesema, “Mheshimiwa Waziri amenukuliwa katika vyombo vya habari kuanzia Mei 1 kutakuwa na usajili mpya wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole ameendelea zaidi kusema kwamba hakutakuwa hakuna ruhusa ya kumiliki zaidi ya laini mbili mpaka ruhusa maalum ya maandishi.” 

“Sasa unafahamu kuwa kuna maeneo mengine laini hazipatikanani. Hamuoni kwamba mtawatesa wananchi ambao katika maeneo yao baadhi ya huduma za laini hazipatikani?,”


Soma zaidi:


Hata hivyo, baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamesema ni vema mamlaka hizo zikatumia taarifa za vitambulisho vya Taifa (Nida) na vitambulisho vya kupigia kula ambazo zipo tayari ili kuepusha usumbufu kwa wananchi kwenda katika maeneo ya usajili. 

Mfumo wa kusajili laini kwa kutumia laini za vidole (Biometric Registration) ulizinduliwa Machi 1, 2018 na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)  baada ya kuwapo vitendo vya watumiaji wa huduma hiyo kugushi vitambulisho au kutumia vitambulisho vya watu wengine.

Mfumo huo ilifanyiwa majaribio katika mikoa sita ya Dar es Salaam, Tanga, Singida, Pwani, Iringa na Zanzibar ambapo kila mkoa ulikuwa na kituo kimoja cha usajili.

TCRA wanatekeleza mfumo huo kwa kushirikiana na watoa huduma za simu za mkononi na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) ambapo utasaidia kupata takwimu sahihi za watumiaji wa simu za mkononi na huduma za fedha kwa ajili ya kuweka mipango sawa ya kuendeleza sekta na uchumi wa Taifa. 

Enable Notifications OK No thanks