Mfumuko wa bei ya bidhaa wang’ang’ania kiwango cha Oktoba
- Mfumuko wa bei kwa Novemba 2022 umebaki kuwa asilimia 4.9
- Mfumuko kwenye huduma za chakula, vinywaji, usafiri wazidi kupaa
Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Novemba 2022 umeendelea kubaki kama ilivyokuwa Oktoba mwaka huu jambo linaloonyesha mwenendo imara wa mabadiliko ya bei katika kipindi hicho.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Novemba 2022 ulikuwa asilimia 4.9 ikiwa ni sawa kabisa na kiwango kilichorekodiwa katika mwaka ulioishia Oktoba 2022.
Taarifa ya NBS iliyotolewa leo Novemba 12, 2022 inaeleza hali hiyo inamaanisha uwepo wa usawa kwenye kasi ya mabadiliko ya bei ya bidhaa kati ya mwaka unaonishia Oktoba na Novemba.
“Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba, 2022 imekuwa sawa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba,” imesema taarifa ya NBS.
Soma zaidi:
Licha ya mfumuko wa jumla kutobadilika, taarifa hiyo inaeleza kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka unaoishia Novemba 2022 umeongezeka kufikia 9.5 kutoka asilimia 9.1 iliyorekodiwa mwaka unaoishia Octoba 2022.
Mbali na bei za bidhaa za chakula na vinywaji, bidhaa nyingine ambazo zimeguswa na mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia Novemba 2022 ni pamoja na usafiri, samani, vifaa vya nyumbani na ukarabati wa makazi pamoja na migahawa na huduma za malazi.
Kwa upande wa huduma za usafiri mfumuko wa bei umepaa kwa asilimia 6.1, samani, vifaa vya vyumbani na ukarabati wa makazi umepaa kwa asilimia 4.1 na migahawa na huduma za malazi mfumuko wa bei umeongezeka kwa asilimia 2.6.
Licha ya mfumuko wa bei kubaki pale pale, bado rekodi hiyo ya kiwango cha Novemba ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa nchini tangu Oktoba 2017.
Kwa mujibu wa tovuti ya Trading Economics. Oktoba 2017 mfumuko wa bei za bidhaa na huduma ulikuwa asilimia 5.1.

Latest
