Mfuko wa bei washuka kwa mara ya tatu mfululizo Tanzania

June 8, 2020 11:00 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Umeshuka hadi kufikia asilimia 3.2 kwa mwaka ulioishia Mei 2020 kutoka asilimia 3.3 iliyorekodiwa Aprili mwaka huu.
  • Umechagizwa zaidi na kupungua kwa gharama za bidhaa za chakula na zisizo za chakula.
  • Hiyo ni mara ya tatu mfululizo kushuka kama ilivyokuwa mwezi Machi na Aprili baada ya kung’ang’ania katika kiwango kimoja Januari na Februari.

Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini Tanzania imeendelea kushuka kwa miezi mitatu mfululizo hadi kufikia asilimia 3.2 kwa mwaka ulioishia Mei 2020 ikichagizwa zaidi na kupungua kwa gharama za bidhaa za chakula na zisizo za chakula.

Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.

Mfumuko wa bei wa Mei umeshuka kutoka asilimia 3.3 iliyorekodiwa Aprili mwaka ambapo pia ilishuka kutoka asilimia 3.4 ya mwaka ulioishia Machi. 

Ripoti ya mfumuko wa bei ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyotolewa leo (Juni 8, 2020) imeeleza kuwa kushuka kwa mfumuko wa bei mwezi Mei kumechangiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei za bidhaa za chakula na zisizokuwa za chakula ikilinganishwa na Aprili mwaka huu. 

Mfumko wa bei  wa bidhaa zisizo za chakula ambazo umeshuka ni pamoja na mafuta ya taa ambayo yamepungua kwa asilimia 14.5, dizeli kwa asilimia 12.9 na petroli kwa asilimia 10. 


Zinazohusiana: 


Kwa upande wa bidhaa za vyakula na vinywaji, mfumuko wa bei umeshuka hadi asilimia 4.4 kutoka asilimia 4.6 iliyorekodiwa Aprili 2020.

“Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizopungua bei kwa mwezi Mei 2020 ni pamoja na matunda kwa asilimia 5.8, viazi mviringo kwa asilimia 5.5, viazi vitamu kwa asilimia 8.8 na ndizi za kupika kwa asilimia 3,” imeeleza ripoti ya NBS. 

Kushuka kwa mfumuko wa bei kwa miezi mitatu mfululizo kumetokea baada ya kasi yake kung’ang’ania katika kiwango kimoja kwa miezi ya Januari na Februari mwaka huu. 

Mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Februari 2020 ulikuwa asilimia 3.7 ikiwa ni sawa kabisa na kiwango kilichorekodiwa katika mwaka ulioishia Januari 2020.

Enable Notifications OK No thanks