Mfahamu Given Edward, mtanzania aliyeshinda tuzo mbili za kimataifa katika sekta ya elimu

December 17, 2018 3:37 pm · Zahara
Share
Tweet
Copy Link

Novemba 30, 2018 Mtabe ilishindana na wabunifu washindi kutoka bara la Asia na bara la Ulaya. Mtabe ilishinda kama mshindi wa jumla na kutunukiwa tuzo ya ubunifu mora kutoka katika mabara hayo matatu. Picha| Given Edward


  • Tuzo hizo ni ile ya Vijana ya Umoja wa Ulaya ya mwaka 2018 na ya Malkia wa Uingereza kwa viongozi vijana ya mwaka 2015 ambazo zinatambua mchango wake katika sekta ya elimu Tanzania.
  • Ni mwanzilishi wa programu mbili za simu za elimu (Apps) za MyElimu na Mtabe zinazofanya kazi kama majukwaa yanayowakutanisha wanafunzi, walimu kujadiliana na kupata masomo ya darasani.
  • Awashauri vijana kujitahidi kusogeza mbele jamii na kufanya kile tunachoweza kwa kutumia kile walichonacho.

Dar es Salaam. Wakati tukielekea kufunga mwaka, jina la Tanzania limeendelea kusikika na kuvuma katika anga za kimataifa hasa katika sekta ya elimu, hii ni baada ya mtanzania Given Edward kushinda tuzo ya Vijana ya Umoja wa Ulaya (European Youth Awards- 2018) inayowatambua vijana wanaotumia teknolojia kuleta matokeo chanya katika jamii.

Given ameshinda tuzo hiyo kupitia programu yake ya simu (App) ya Mtabe  inayowasaidia wanafunzi wa shule za sekondari kujifunza masomo ya darasani kwenye viganja vyao hata pasipo kuunganishwa na mtandao wa intaneti. 

Nyota yake iling’aa zaidi mwaka 2015 alipopata tuzo ya Malkia wa Uingereza kwa viongozi vijana (The Queens Young Leaders) ambayo hutolewa kila mwaka kama njia moja ya kuitambua kazi inayofanywa na vijana katika jamii mbalimbali za mataifa ya Jumuiya ya Madola.

Ushindi huo ulitokana na App yake ya MyELimu  kufanya vizuri kama jukwaa la mtandaoni linalowaunganisha walimu na wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari kukutana na kujadili pamoja masomo. 

Mtanzania huyo anayebobea katika sayansi ya kompyuta, bado anaendelea kukuna kichwa ili kutanua wigo wa kuwafikia wanafunzi wa Tanzania wanaokabiliwa na changamoto za ujifunzaji shuleni. Bado hajakata tamaa ya kufikia malengo yake licha vikwazo vinavyomrudisha nyuma.

Ungana na Nukta kufahamu safari ya Given alikotoka na matarajio aliyonayo katika kutumia teknolojia rahisi kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira: 

Nukta: Hongera sana Given kwa kile unachofanya hasa kwa tuzo mbili za kimataifa ulizozipata, naamini mafanikio hayo sio bure ulianzia wapi?

Given: Nilisoma shule ya sekondari Tegeta alafu nikamalizia masomo yangu ya kidato cha tano na sita katika shule ya Kibasila (za jijini Dar es Salaam) nikichukua masomo ya Sanaa.

Nukta: Masomo ya Sanaa hadi kuwa mtaalam kwenye masuala ya kompyuta iliuwaje?

Given: Nilikuwa napenda kusoma masomo ya sayansi ya kompyuta lakini nilipoomba wakati naingia chuo sikupata nafasi na nikapata nafasi ya kusoma masuala ya sayansi ya siasa na uongozi katika Khuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM), baada ya mwaka mmoja nikapata scholarship (Ufadhili) katika chuo cha Africa Leadership University, sasa nasomea masomo ya sayansi ya kompyuta.

Nukta: Tunafahamu wewe ni mwanzilishi wa programu mbili za simu za MyElimu na Mtabe. Leo tuzungumzie App ya Mtabe ambayo imekuwezesha kupata tuzo ya Umoja wa Ulaya kwa mwaka 2018. Wazo la kuanzisha Mtabe app lilianzia wapi?

Given: Miaka minne iliyopita, nilianzisha MyElimu – Mtandao ambao unaunganisha wanafunzi walio mbali ili kukutana na kujadiliana masomo ya shule wakiwa sehemu zao tofauti.

Hata hivyo, MyElimu ilikuwa inahitaji intaneti kwa ajili ya wanafunzi kujadili, hapo ndipo nilipotengeneza Mtabe ambayo inafanya kazi hata bila mtandao wa intaneti ili kusaidia wanafunzi wa sekondari.

 Hitaji la elimu Tanzania ni kubwa, na nilihitaji namna ya kuweza kuwajibu na kuwafikia wanafunzi wengi zaidi kwa wakati mmoja. Teknolojia ya “artificial intelligence” (mashine isiyoendeshwa na binadamu) inaniwezesha mimi kufanikisha hilo.

Kuhusu kujifunza, nilijifunza mwenyewe kwenye laptop (kompyuta mpakato) yangu.


Zinzaohusiana: Emanuel Feruz: Mtaalam wa Tehama aliyegeukia ujasirimali wa kupigaji picha

                          Rahma Bajun: Mjasiriamali anayetamba kimataifa


Nukta: Ilichukua muda gani hadi Mtabe ilipokamilika na kuanza kazi rasmi?

Given: Mtabe imekuwa kwenye matengenezo kwa miezi 14 sasa. Imefanyiwa kazi Mauritius (nchini Mauritania), imefanyiwa kazi Afrika Kusini kwa miezi zaidi ya 4, na tunaendelea kuiboresha sasa tukiwa hapa Tanzania.

Nukta: Uliwezaje kupenya na kuwa miongoni mwa watu waliojinyakulia tuzo ya mwaka huu ya Umoja wa Ulaya?

Given: Mashindano yalianza Machi 2018, ambapo shindano hilo lilifanyika Tanzania kutafuta wabunifu watatu  watakaowakilisha Taifa na kwenda kushindana Accra, Ghana kwenye mashindao ya Afrika.

Katika mashindano hayo, ubunifu wa Mtabe ulishinda kwenye fainali za Afrika na kuwa moja ya bunifu tatu kati ya 12 Afrika nzima zilizochaguliwa kuiwakilisha Afrika katika mashindano ya dunia.

Mtabe ilishindana na wabunifu kutoka Kenya na Senegal na baada ya majaji kufanya uchambuzi, Mtabe kutoka Tanzania ilipigiwa kura nyingi na kuchaguliwa rasmi kuwa ubunifu bora zaidi kutoka kwa vijana Afrika.

Tarehe 30 mwezi wa 11, tulishindana na wabunifu washindi kutoka bara la Asia na bara la Ulaya. Mtabe ilishinda kama mshindi wa jumla na kutunukiwa tuzo ya ubunifu mora kutoka katika mabara hayo matatu.

Given akiwa na wenzake ambao kwa namna moja au nyingine wanamchango katika kuhakikisha Mtabe inakuwa. Picha|Given Edward.

Nukta: Nini matarajio yenu katika kuhakikisha mnachokifanya katika sekta ya elimu kinazidi kukua na kuwafikia watu wengi zaidi nchini na Afrika kwa ujumla?

Given: Mpaka sasa timu yetu tupo watu nane.  Najivunia timu yangu, wanajitoa sana katika kuhakikisha tunafanya kitu kizuri na kusaidia wanafunzi. Tunategemea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo na ubunifu. Kwa yoyote atakayetaka kushirikiana nasi, anaweza kutuandikia kupitia info@mtabeapp.com

Nukta: Unaiona wapi Mtabe miaka 10 ijayo?

Given: Tutakuwa katika nchi nyingi za Afrika na kubadilisha maisha ya watu hasa katika sekta ya elimu.

Nukta: Una ushauri gani kwa vijana wabunifu katika teknolojia ambao hawazichangamkii fursa zilizopo katika mitandao au kwenye jamii ambazo zingeweza kuwainua katika kazi zao?

Given: Tujitahidi tu kama vijana kusogeza mbele hii jamii yetu, tufanye kile tunachoweza kwa kutumia kile tulichonacho; vijana wenzetu kutoka nchi nyingine hawana tofauti na sisi isipokuwa nia na kiu ya kujifunza.

Tusisikilize wanaosema hatuwezi kushindana na vijana wengine wa nje, tunaweza na tutashinda.

Enable Notifications OK No thanks