Mayele awa gumzo kwa mashabiki, Yanga ikitua Mwanza
Kocha wa Yanga, Nasredine Nabi akiwasili Uwanja wa ndege wa Mwanza. Picha| Klabu ya Yanga.
- Itakipiga na Mbao FC Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
- Ni katika kuwania Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).
- Mayele awa gumzo kwa mashabiki.
Dar es Salaam. Kikosi cha klabu ya Yanga kimetua leo jijini Mwanza kwa ajili ya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Mbao FC utakaopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Yanga imewasili katika Uwanja wa ndege wa Mwanza saa 1:30 asubuhi na kupokelewa na mashabiki wengi waliojitokeza uwanjani hapo kuwashuhudia nyota wao wakiwasili.
Shauku kubwa ya mashabiki ilikuwa kumuona staa wa timu hiyo Fiston Mayele ambaye amekuwa akiwakosha kwa kutupia mabao na kuteka mashabiki kwa aina yake ya ushangiliaji.
Kabla hata ya ndege haijawasili anga la Mwanza, mashabiki walisikika wakisema tumekuja kumuona Mayele na ndege ilipoanza kukaribia wengine wakasikika wakisema ‘Mayele amepanda mule’.
Baada ya msafara kuanza kupita kutoka kwenye eneo la ukaguzi shangwe la mashabiki lilisikika likiwashangilia mastaa wao huku Mayele akiwa wa mwisho na kocha Nasredine Nabi kuonekana na kuibua shangwe kubwa wakitaja jina lake na kumsindikiza kwenye gari.
Baada ya kumshuhudia Mayele akikanyaga ardhi ya Jiji la Mwanza kwa mara ya kwanza na kukonga nyoyo zao mashabiki hawakuridhika kwani walianza kumuulizia Msemaji wa timu hiyo Haji Manara wakisema ‘Tunataka kumuona Manara, yuko wapi Manara’.
Afisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema timu hiyo inafanya mazoezi kwenye uwanja wa CCM Kirumba huku akiwaomba wanachama kujitokeza uwanjani hapo kuandikishwa kwa mfumo wa kidigitali katika zoezi linaloendelea kwenye uwanja huo.
Latest
