Maumivu watumiaji machinjio ya Vingunguti Dar
- Watalazimika kusubiri mpaka Manispaa ya Ilala iombe upya fedha za kujenga machinjio ya kisasa baada ya kukiuka makubaliano ya awali ya ujenzi.
- Machinjio iliyopo sasa inakabiliwa na uchakavu wa miundombinu, changamoto za usafi na mazingira na mrundikano wa watu wanaofuata huduma.
- Manispaa ya Ilala yadai kukwama kwa mradi kunatokana na kuchelewa kufanya ununuzi na mabadiliko ya mara kwa mara ya kiufundi kutoka kwa mtaalam mshauri wa mradi huo.
Dar es Salaam. Siku moja baada ya Serikali kuinyang’anya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam Sh3 bilioni ilizoipatia kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kimkakati wa machinjio ya kisasa wa Vingunguti kutokana na kushindwa kutekeleza kwa wakati mradi huo, baadhi ya watumiaji wa machinjio hiyo wamesema uamuzi huo utaendelea kuathiri mwenendo wa biashara na afya zao.
Mradi huo ulibuniwa kwa ajili ya kutatua changamoto za mazingira na utendaji wa machinjio iliyopo sasa ya Vingunguti ambayo kwa sehemu kubwa miundombinu yake imechakaa na haiendani na mahitaji kwa sasa.
Uamuzi wa kuinyang’anya pesa manispaa hiyo ulifikiwa jana (Februari 19, 2019 na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo, ambapo alisema Serikali ilitoa kiasi cha Sh3 bilioni kati ya Sh8.5 bilioni tangu Mei, 2018 lakini chakushangaza hadi sasa fedha hizo hazijatumika hata senti moja.
“Fedha haziwezi kukaa kwa mwaka mzima bila matumizi ilihali kuna maeneo mengine ambako fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi, hivyo tunazichukua fedha hizi na Manispaa ya Ilala mtalazimika kuomba upya mtakapokuwa mmejipanga,” alisema Dk Kijaji.
Alibainisha kuwa utaratibu wa fedha za Serikali zinazopelekwa kwenye miradi zinatakiwa zianze kutumika ndani ya miezi mitatu lakini Manispaa ya Ilala haijazitumia fedha hizo huku karibu mwaka wa fedha wa 2017/2018 ukikaribia kumalizika.
Soma zaidi: Mpina apania kujenga viwanda vya samaki, nyama nchini
Watumiaji wa machijio hiyo wakiwemo wafanyabiashara, wachinjaji na wanunuzi wa vitoweo wameiambia Nukta kuwa uamuzi huo wa Serikali utawasubirisha kwa muda mrefu kupata huduma bora na uhakika za machijio kwasababu mazingira ya sasa siyo rafiki kwa afya na biashara zao.
John Kikoko ambaye ni mchinjaji wa ng’ombe amesema changamoto inayowakabili ni miundombinu mibovu ya mirefeji na barabara ambapo wakati wa mvua huziba na kutuwamisha maji machafu, jambo linalosababisha kuwepo kwa harufu kali na vimelea vya magonjwa.
“Kama unavyoona mwenyewe usafi bado ni changamoto lakini tunapambana kuendelea kupata ridhiki,” amesema Kikoko ambaye amekuwa akifanya shughuli hiyo kwa zaidi ya miaka miwili.
Kutokana na miundombinu iliyopo kuwa ya zamani inaelemewa na idadi kubwa ya watu wanaokuja kupata huduma jambo linalozua fujo za mara kwa mara za watu hasa nyakati za usiku wakigombania kupata huduma
Mwananchi mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe, ameiambia Nukta kuwa Aprili 2018 Manispaa ya Ilala iliweka utaratibu mzuri wa kuratibu shughuli za uchinjaji wanyama na kuviondoa vikundi vya wafanyabiashara ambavyo awali vilikuwa vinasimamia usalama wa watu na mali, lakini haijaondoa tatizo kwasababu ya muingiliano mkubwa wa watu.
Licha ya changamoto zilizopo katika machinjio ya Vingunguti bado, wananchi wameendelea na shughuli zao za kujipatia kipato kwa chinja wanyama mbalimbali wa kufugwa wanaopelekwa katika eneo hilo. Picha|Daniel Samson.
Kutopatikana kwa machinjio mpya kumegusa pia biashara ya wauza ng’ombe na mbuzi ambapo wanakosa eneo la kutunza wanyama hao wakati wakisubiri kuwachinja kutokana na eneo lililopo sasa kuwa ni dogo.
Venance Jackson ambaye ni muuzaji wa mbuzi anasema wanalazimika kuwaweka mbuzi barabarani na mitaani karibu na machinjio hiyo kabla ya kuwauza kwa wachinjaji.
“Eneo ni dogo haturuhusiwi kuingiza mbuzi huko ndani mpaka upate mteja anayetaka kuchinja labda utaingia nao,” amesema Jackson.
Anasema wakati mwingine wanalazimika kukodi vyumba maeneo ya jirani ili kuwahifadhi wanyama hao ambapo kila mtu huchanga Sh20,000 kulingana na idadi yao kama malipo ya mwenye nyumba kwa mwezi mmoja.
Hali hiyo imekuwa ikiwaumiza kutokana na kubadilika kwa bei ya soko la mbuzi na gharama za kuwasafirisha kutoka mnadani hadi machinjioni.
“Kwa sasa bei ya mbuzi siyo ya kuridhisha kabisa imeshuka; kwa mbuzi tuliyekuwa tunauza Sh100,000 sasa tunauza Sh70,000 mpaka Sh50,000. Sasa hapo hupati faida ukijumuisha na gharama za kuwahifadhi wakifika hapa,” amesema mfanyabiashara wa mbuzi, Shabaan Mtanga.
Muonekano wa sehemu ya kuuzia nyama katika machinjio ya Vingunguti Jijini Dar es Salaam ambayo inakabiliwa na changamoto ya ubovu wa mbiundombinu. Picha| Daniel Samson.
Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wakwamisha mradi
Afisa Mipango wa Manispaa ya Ilala Ando Mwankuga, amekiri kuwa kulikuwa na ucheleweshaji wa kuanza kutekeleza mradi huo kwa kile alichodai ni kuchelewa kwa mchakato wa kufanya ununuzi na mabadiliko ya mara kwa mara ya kiufundi kutoka kwa mtaalam mshauri wa mradi huo.
“Ucheleweshaji huu si wa makusudi bali ilikuwa ni kuhakikisha tunafuata taratibu zote za ununuzi na kuhakikisha kuwa mradi utakaojengwa uwe na ubora unaotakiwa na unaolingana na thamani ya fedha na tunatarajia kuanza kuutekeleza Machi 10, 2019,” Mwankuga katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango jana.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa kabla ya kuomba fedha za miradi ya kimkakati ni lazima masuala yote ya upembuzi yakinifu yawe yamefanyika na kama hayakufanyika basi Manispaa ilidanganya wakati wa makubaliano.
Manisapaa ya Ilala, ilikuwa miongoni mwa Halmashauri na Manispaa 17 nchini zilizopatiwa ruzuku na Serikali cha zaidi ya Sh147 bilioni katika awamu ya kwanza katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati itakayochochea upatikanaji wa mapato ya ndani na miradi hiyo ilitakiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 18.