Maumivu, kicheko kwa wasanii mabadiliko chati za muziki Youtube
- Mtandao huo umefuta kigezo cha kulipia matangazo ya video kama kiwezeshi cha kuingia kwenye chati ya nyimbo zinazofanya vizuri katika mtandao huo.
- Sasa msanii ataingia kwenye chati hiyo kwa kuhamasisha watu waangalie wimbo wake kwa kusambaza viunganishi katika mitandao mbalimbali (Organic Viewership)
- Wadau wa muziki watoa maoni tofauti kwa mabadiliko hayo.
Dar es Salaam. Wanamuziki wa Tanzania wanaotumia YouTube kuuza kazi zao watalazimika kutafuta njia nyingine ya kutangaza kazi katika mtandao huo baada ya kufanyika mabadiliko katika kipengele chake cha orodha ya nyimbo na video zinazofanya vizuri.
YouTube imebadilisha vigezo vya wanamuziki, nyimbo na video zinazoingia katika orodha bora zilizo na watazamaji wengi (Music Charts & Insights)
Kipengele hicho “music chats” ni sehemu inayotumiwa na Youtube kuonyesha msanii gani na nyimbo gani ni maarufu zaidi na kuzipanga kwa mtiririko wa ubora kulingana na idadi ya watazamaji.
Awali, mtandao huo ulitumia vigezo vya nyimbo yenye watazamaji wengi zaidi kuingia kwenye orodha yake bila kujali ni namna gani wasanii wenye video hizo walipata watizamaji hao.
Wasanii walitumia matangazo ya kulipia, nyimbo zinazofanya vizuri (Trending) na zinazotokea kwenye ukurasa wa mtandao huo (home page) kama ngazi ya msanii kujinyakulia wadhifa kwenye chati zake za ubora ambapo kwa sasa, kigezo cha matangazo ya kulipia kimetolewa.
Kwa upande wa matangazo, msanii aliweza kulipia video yake ili itangazwe kwa watu wengi na hivyo kujinyakulia watazamaji wengi ndani ya muda mfupi mara tu baada ya kuachia video yake na hivyo kufanikiwa kuingia kwenye orodha ya ubora ya YouTube kwa muda mfupi.
“Hatuhesabu kutazamwa kwa video zinazolipiwa kwa kufanyiwa matangazo kwenye mahesabu ya chati za ubora za YouTube. Wasanii na muziki bora sasa vitataainishwa kwa kuhesabu watizamaji wa moja kwa moja wa video zao,” inaeleza sehemu ya taarifa ya mtandao huo.
Wasanii walitumia matangazo ya kulipia, nyimbo zinazofanya vizuri (Trending) na zinazotokea kwenye ukurasa wa mtandao huo (home page) kama ngazi ya msanii kujinyakulia wadhifa kwenye chati zake za ubora ambapo kwa sasa, kigezo cha matangazo ya kulipia kimetolewa. Picha|Mtandao.
Hata hivyo, mabadiliko hayo hayamzuii msanii kutangaza video yake bali msanii atakayelipia matangazo hatoweza kuingia kwenye orodha ya nyimbo bora za mtandao huo.
Youtube imeeleza kuwa mabadiliko hayo yana lengo la kuongeza ufanisi katika kutoa vyeo vya wasanii na nyimbo bora kama ilivyo kwenye orodha zingine maarufu zikiwemo orodha za Billboard na Nielsen.
Baada ya mabadiliko hayo, ili msanii aingie kwenye chati za ubora, atahitajika kuhamasisha watu kutafuta wimbo wake kwenye mtandao huo, kusambaza kiunganishi (Link) cha wimbo wake ama kuambatanisha link ya wimbo huo kwenye mitandao mingine kama Instagram ambapo mtu atautazama moja kwa moja.
“Video zitakazofuzu kuingia kwenye mahesabu ya rekodi za masaa 24 ni zile zenye kutazamwa zaidi moja kwa moja ndani ya masaa 24 baada ya video kutolewa rasmi,” inaeleza taarifa ya YouTube.
Zinazohusiana
- Youtube yaleta mbinu mpya ya kudhibiti maudhui ya watoto mtandaoni
- YouTube yajipanga kuzuia matangazo ya biashara kwenye video za watoto
Mabadiliko hayo ni “fimbo kwa watengeneza maudhui”
Mabadiliko ya Youtube, huenda yakabadilisha taswira ya muziki wa Bongo fleva na kuingiza sura mpya kwenye chati hizo baada ya njia ya matangazo kuondolewa kama kigezo cha nyimbo kuwa bora.
Wadau mbalimbali wa muziki wametoa maoni yao juu ya mabadiliko hayo na namna gani yanagusa maslahi ya wasanii wa Tanzania ambao mtandao huo umekuwa sehemu ya kujipatia kipato na umaarufu.
Mkurugenzi wa kampuni ya Serengeti Bytes ambaye pia ni Mtaalam wa masuala ya mahusiano ya umma na mitandao ya kijamii, Kennedy Mmari anasema mabadiliko hayo yanaweza kuwa “fimbo kwa watengeneza maudhui” hasa wanaotegemea mtandao huo kama sehemu ya kujipatia kipato.
Amesema iwapo msanii au mzalishaji maudhui yoyote alitegemea njia hiyo kuingia kwenye chati bora za mtandao huo basi ataathirika moja kwa moja.
“Wapo wasanii, wazalishaji maudhui na makampuni mbalimbali ambao wanatumia njia hii kufikia watu wengi na kuingia kwenye chati. Maamuzi haya ni fimbo kwao,” amesema Mmari.
Orodha ya nyimbo za wasanii wa Tanzania ambazo zina katika chati ya juu ya Youtube ambazo zimetazamwa na watu wengi zaidi. Picha|Youtube.
Hata hivyo amesema hana imani kama maamuzi hayo yana athari zozote kwa mtandao wa YouTube kwani hayajazuia fursa ya mtandao huo kupata matangazo.
“Watoa matangazo wengi wanachoangalia ni tangazo lao kufikia watu wengi. Siyo kuingia kwenye chati wala kutrend (kupata umaarufu),” anasema Mmari.
Hata wasanii ambao walikuwa hawana fedha za kulipia matangazo ili nyimbo zao zitazamwe na watu wengi, huenda ikawa ni furaha kwao kujipatia umaarufu kama watafanya juhudi za kusambaza links za nyimbo zao mtandaoni.
Mabadiliko hayo yatawapa uwanja sawa wa ushindani wa nyimbo za kupanda chati na kujipatia umaarufu katika mtandao huo.
Msanii wa Bongo Fleva anayechipukia, Salum Nyangumwe (Golden) anasema maamuzi hayo ni mazuri na yatamsaidia yeye kujua ni kwa namna gani anakua kimuziki na kuifikia dunia.
Amesema kupitia namna gani watu wanafuatilia muziki wake bila “kuboost” itaonyesha uhalali wa ukuaji wake na hivyo kuongeza motisha juu ya muziki anaofanya.
“Kwa kubonyeza “link” (kiunganishi cha mtandao) inakuonyesha ni jinsi gani unakua tofauti na kununua watazamaji. Unaweza kujihisi ni mkubwa kwa kiasi hicho kumbe hujafikia ukubwa huo,” anasema Golden.
Latest



